Wednesday 18 November 2020

IJUE MILANGO YA CHANGAMOTO NA JINSI YA KUIFUNGA



Habari ndugu msomaji wa blogu  yetu pendwa  , karibu tena katika mwendelezo wa masomo yetu


Kama sio kila siku basi pengine haishi wiki bila kukutana na changamoto au kumsikia mtu akilalimika dhidi ya changamoto anazopambana nazo,hivi umewahi kaa chini ukajiuliza kwa nini changamoto zikuandame? .


Ni kawaida kukutwa na changamoto  haijalishi ni changamoto za aina gani lakini huwezi kuishi bila kukutana na aina yoyote ya vikwazo ( changamoto) na hii ni kwa sababu ili  tuwe watu wapya ni lazima tusafishe vikwazo vilivyo katika njia zetu la sivyo itakuwa ngumu kusonga mbele, je changamoto hupitia wapi mpaka kutufikia sisi? 


Ipo milango ya changamoto ambapo asilimia kubwa ya changamoto kupitia huko hivyo ni muhimu kujua milango hiyo ili ikiwa kuna uwezekano basi marekebisho yafanyike kuzipunguza aina hizo za changamoto, bila shaka umewahi kuandamwa na aina fulani tu ya changamoto au umewahi kusikia mtu fulani akilalimika kusumbuliwa na aina fulani tu ya changamoto hayo ni matokeo ya kuacha mlango fulani wazi wa changamoto ndio maana changamoto hujirudia za aina fulani. 



Sifa uliyonayo, una sifa gani?  yaweza kuwa cheo, uzuri, upole  , utajiri  n.k , hapo nazungumza sifa yoyote ile ya mtu uliyonayo usipojitambua na kujidhibiti lazima kuna aina fulani za changamoto zitakufuata kwa sababu ya kuwa na sifa hiyo .Upole ni sifa  na kuna watu fulani watakufanyia mambo mabaya wakijua ikiwemo kukudhulumu pesa wakijua kwa upole wako utakaa kimya hivyo na wewe ukiendekeza upole wako basi utaandamwa na changamoto za kudhulumiwa kila siku , kuna watu wakijitambua wazuri huanzisha tabia fulani ya dharau  ambapo matokeo yake ni kuandamwa na changamoto za kukimbiwa na marafiki . Sifa yoyote uliyonayo yafaa kuiidhibiti isikupe maamuzi kwani itakuwa ndio mlango wako wa changamoto. 



Ufahamu wako, Karibu kila mtu endapo angeongezewa ufahamu zaidi pengine asingefanya maamuzi anayojutia leo kumbe tunafanya maamuzi kutoksna na ufahamu wetu wa sasa  hivyo ufahamu wako ni mlango wa changamoto fulani kwako  mfano  ukiona mtu anaandamwa na changamoto kujutia maamuzi yake kuna uwezekano mkubwa akawa na shida kwenye ufahamu anaotumia kufanyia maamuzi. Jitahidi kujiongezea ufahamu wa kutosha kwenye eneo ambalo unataka kulifanyia maamuzi la sivyo utakuwa unatumia taarifa chache kutoa hitimisho na kesho ukipata taarifa nyingine ndipo unaanza kujutia kuwa hitimisho uliyofanya sio sahihi. 


Mtindo wa maisha ( life style) , karibu kila mtu ana mtindo wake wa maisha yaweza kuwa ndivyo umezaliwa hivyo au ni uchaguzi wako umefanya kuishi hivyo lakini huo ndio mtindo wako wa maisha, mtindo wako ni upi? .Nakumbuka kipindi nipo shule nilikuwa na mtindo wangu wa maisha unaotakana na asili yangu ya kuumbwa na mtindo huo ilikuwa ni kupenda kutojichanganya  na watu nilikuwa mtu wa kukaa sana peke yangu mtindo huo ulifanya nikutane na changamoto za kukosa habari nyingi ikiwemo kukosa makundi ya kufanya nao mijadala  ya kimasomo ( discussion), nilikaa chini nikaona huo mtindo wangu utafanya nifeli hivyo nikajilizamisha kuwa mtu wa jamii ( social) ili tu nipunguze changamoto za kufeli masomo kwa kukosa watu wa kujadili nao.Nimekushirikisha mtindo wangu wa maisha bila shaka utakuwa umejitafakari ukaona kuna changamoto nyingi hazikuachi kwa sababu ya mtindo wako maisha , mtindo wako maisha  ni upi ? Kuna changamoto zinakufata kwa kuvutiwa na namna unavyoishi?  Jitafakari uchukue maamuzi ya kurekebisha mtindo wako inawezekana. 


Utakubaliana na mimi kuwa kama sio sifa yako basi itakuwa mtindo wako wa maisha au ufahamu wako ndio chanzo cha aina fulani ya changamoto zilikukuta au zinazoendelea kukufuata hivyo ni kazi kwako kujifanyia mabadiliko katika maeneo hayo ili kuzipunguza changamoto za aina fulani kukufuata muda wote .


Makala hii imeandikwa na Saul Kalivubha , Mwanasayansi tiba katika maabara za binadamu na mwalimu. 


0652 134707