Friday 26 January 2024

WANAVYUO TUSIISHI KAMA HATUTAHITIMU

 WANAVYUO TUSIISHI KAMA HATUTAHITIMU. 

Habari ndugu msomaji wa gazeti letu pendwa na karibu tena katika safu hii , leo tuangazie wasomi wa vyuo na hasa vyuo vikuu na hatima za maisha yao mtaani( baada ya kuhitimu)

Zama zimebadilika sana kiasi kwamba muhitimu wa chuo wa sasa ni kawaida kukaa nyumbani zaidi ya mwaka akisubiria ajira ambapo kipindi cha miaka kadhaa ya nyuma muhitimu alimaliza na kupitiliza kwenye ajira , ajira ilikuwa ni uhakika tofauti na sasa ajira imebaki ni bahati.Mabadiliko hayo ni ya kawaida sana sio Tanzania tu hata nchi za wenzetu huko ulaya dimbwi la wanachuo kukosa ajira linaongezeka kila siku tukiachana na tekinolojia kuchukua nafasi za ajira zetu mfano mgunduzi wa robot unachukua nafasi ya mtu kutenda kazi lakini pia idadi ya wasomi inazidi kuongezeka sana tofauti na zama zile unakuta mtaa mzima mwana chuo ni mmoja mtaani sasa mtaa mzima kuna zaidi ya wanavyuo ishirini na zaidi. 

Nimekuwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha afya na sayansi shirikishi muhimbili kwa miaka yangu kuishi pale kama mwanafunzi kuna jambo muhimu nilijifunza pengine kwa uliyehitimu tayari linaweza lisikusaidie tena lakini kwa aliye mwanafunzi sasa likamsaidia kwa kusoma makala hii au wewe kuwa balozi wa kufikisha ujumbe kwa anaye husika na umfundishe. 

Kumaliza chuo sio tukio la dharura ni wazi kuwa unaenda chuo leo na baada ya miaka kadhaa utarudi tena mtaani kuendelea na maisha mengine kwa kuitumia elimu yako kukupa pesa ili maisha ya kawaida yaendelee sasa utaishije?.

Ishi kama utahitimu chuo, vyuoni kuna makundi yanayonufaika na mikopo ya serikali yaweza kuwa mkopo ukawa wa 100% au pungufu ya asilimia hizo lakini bado ni mkopo hivyo lazima utaulipa tu sasa unautumiaje mkopo huo kumudu maisha yako ya chuo na kubaki na ziada kwa ajili ya kuendeshea maisha baada ya chuo?. Kuishi maisha chini ya kipato chako hii ni mbinu bora zaidi katika kuijali kesho yako , sio wanavyuo wote lakini wapo wanavyuo maisha yao ni kama tayari wamehitimu na wana kazi zao au wanaishi kama ule mkopo ni bure na wana uhakika kuwa siku wanamaliza tu na ajira watapata hivyo kuanzia utaratibu wa chakula chao, mapambo ya vyumba vyao na uvaaji wao ni gharama kubwa sana kulinganisha na mkopo wanaopewa na muda mwingine hujikuta wakiwa kwenye madeni ya kutosha tu kabla ya kupokea bumu jingine kwa mfumo huo si hata nauli ya kukurudisha kijijini baada ya kuhitimu utaikosa? 

Baada ya kuhitimu kuna maisha kabla ya kupata ajira na maisha hayo tukiachana na kula na kuvaa pamoja na sehemu ya kulala pia kuna kupeleka barua za maombi katika ofisi husika au kuzituma kwa njia ya barua pepe bila kusahau gharama za kwenda pale ulipoitwa mahojiano ( interview) na maisha yote hayo yanahitaji pesa sasa ikiwa una mkopo chuoni achana na imani kuwa pesa haitoshi wewe simamia na kufanya mambo chini ya pesa unayopewa angalia utunze hata elfu hamsini kwa kila ingizo ( bumu) hapo ukimaliza utakuwa na ziada ya kukusukuma kutafuta ajira au namna nyingine ya maisha, jiulize ikiwa utamaliza chuo na ukapata kazi sawa na ingizo la mkopo kwa mwezi maisha yatakushinda? kuna wafanyakazi mnalipwa nao thamani sawa ya pesa lakini maisha yanaendelea na ziada wanabaki nayo kwa nini ushindwe? Chunguza maisha yako kwa siku unaishi kwa gharama za zaidi ya elfu nane miatano? ( ingizo la mkopo kwa siku) jibane sana uishi hata kwa elfu tano basi ili ubaki na elfu tatu miatano itakusaidia hiyo siku ukimaliza mafunzo. 

Kuna fursa kubwa sana ambayo kwa sasa ndio ina nafasi kubwa sana katika kusaidia watu kupata ajira nayo hiyo ni kujitolea, sasa watu wanaojitolea wengi wao ndio huingizwa kwenye mfumo wa ajira iwe taasisi binafsi au za kiserikali na pia katika kujitolea kuna uzoefu unapata katika taaluma yako lakini usisahau kuwa maana halisi ya kujitolea ni kufanya kazi bila malipo ya kifedha sasa utaweza kweli kujitolea ? Kwa namna yoyote ile ukiweza jitahidi utoke chuo ukiwa na pesa ya kukufanya uishi mtaani kwa miezi sita hivyo hata ukipata pa kujitolea nina amini ndani ya miezi sita watakuwa wameshakufikiria kukulipa ndio maana nimesema angalau utoke na ziada ya miezi sita, tumia mkopo wako kwa nidhamu huku ukiishi maisha ya maandalizi. 

Makala hii imeandikwa na Saul Kalivubha , Mwanasayansi. 

+255652 134707