Monday 3 October 2022

 USISUBIRI PESA IPUNGUE NDIO UWEKE NIDHAMU YA MATUMIZI

Matumizi ya pesa bado ni changamoto kwa watu wengi na matokeo yake hujikuta katika ukosefu wa pesa wa mara kwa mara na hii sio kwa waajiwa tu hata waliojiajiri kwenye mambo yao binafsi  bado hujikuta kwenye kipindi kigumu cha ukosefu wa pesa sio kwa sababu haikuwepo la hasha ni kwa sababu ilikuwepo lakini ikatumiwa bila kuzingatia matumizi sahihi kutokana na kipato. Ukipata muda tulivu ukajitafakari utagundua kuwa pindi upatapo pesa matumizi yako yanakuwa juu na hupungua kadri pesa inavyopungua yaani kwa lugha rahisi  ni kuwa nidhamu yako ya matumizi ya pesa inaongezeka kadri unavyoishiwa pesa. 

Pesa ni nguvu ya kihisia ambapo usipoitawala itakutawala yenyewe kwa kukupa maamuzi mengi na hapo utakosa utulivu hali ambayo itafanya upoteze nidhamu ya matumizi ndio maana mshahara ukiingia unaweza jikuta unafanya manunuzi bila kuangalia ukubwa wa gharama kwa sababu unajua pesa ipo lakini ukianza kusikia mfuko umepwaya ndio utarudisha makini wa matumizi kwa mfano mwanzo ulilipwa laki tano na ilipofikia mfukoni umebaki na laki moja ndio utaanza kuipigia mahesabu hiyo laki moja kuangalia kama itakufikisha mwezi mwingine, je kwa nini hukufikiria hivyo tangu ukiwa na laki tano? 

Nidhamu ya pesa ni kuheshimu pato lako kwanza na pili ni kuheshimu matumizi sahihi yaliyo ndani ya kipato chako kama ulipanga kununua kitu cha shilingi mia ndio itakuwa sawa kulingana na kipato chako basi fanya hivyo lakini ulinunua kwa shilingi Mia mbili ujue umekula na pesa ya siku fulani hivyo jiandaye siku hiyo kukosa pesa la sivyo iwe ni dharura ndio tumia lakini kama si dharura yatakiwa ujidhibiti dhidi ya matumizi ya pesa pale tu unapoipata, changamoto ya pesa ni kuwa ukitumia pesa ndogo unaona kawaida tu lakini mwisho wa siku ukijumlisha unakuta kama ungehifadhi ungekuwa mbali sana kifedha hivyo nidhamu ukianza na kuheshimu matumizi yako yaliyo ndani ya kipato chako utakuwa kwenye kiwango kizuri cha kuweka akiba. 

Nidhamu binafsi katika matumizi ya pesa inajengwa na lengo kuu ulilonalo la kesho hapo ndio utakuwa unatumia pesa ukikumbuka kesho hivyo utakuwa ukijikumbusha kila kabla ya matumizi ambayo si salama kulingana na kipato chako na utakuwa na nidhamu muda wote, lazima uwe na nidhamu au ukose nidhamu lakini ukubali kupoteza lengo kuu la kesho na njia nzuri nyingine ni kuigawa pesa yako kwa siku utagundua unaingiza shilingi ngapi kila siku na kisha angalia matumizi yako kila siku yanaendana na pato lako la siku? Kwa kuanzia na hapo utajirekebisha kimatumizi na utaheshimu matumizi sahihi ya pesa. 

Pesa ikiwa nyingi itakupa upofu wa kuamini kuwa huwezi kuishiwa hivyo kila matumizi yakujiayo kichwani utayafanya na hapo ndio mwanzo wa kutumia hovyo pesa  mpaka baadaye ikipungua ndio itakutoa upofu uone kuwa kuna hatari itokanayo na ukosefu wa pesa kwa sababu pesa uliyonayo haitoshi kukufikisha msimu mwingine wa pesa kumbe kuna kuna nguvu kubwa inatakiwa uwe nayo awali ili kudhibiti hisia za pesa zisikutawale. 

Kujua unataka nini pia ni moja wapo wa ujenzi mzuri wa nidhamu ya pesa kwa sababu utajizuia dhidi ya matumizi ambayo sio ya msingi kwako na hayapo ndani ya bajeti yako kwa kipato chako na aina yako ya safari uliyonayo, kutojua nini unataka itakuingiza kwenye matumizi yasiyo sahihi kwa sababu kila utakachokiona kinavutia utahitaji kukinunua. Pesa isikuendeshe bali unatakiwa wewe ndio uipangie majukumu  na ukiona unalemewa basi jitahidi usiwe unatembea na pesa nyingi mfukoni hii ni njia nzuri pia ya kuitawala pesa kwa sababu huwezi kufanya manunuzi yasiyo na mpangilio, tunafanya manunuzi yasiyo na mpangilio kwa sababu tunakuwa na pesa au urahisi wa kuipata pesa. Usikumbushwe na matatizo bali jikumbushe mwenyewe kuwa kuna siku changamoto zitatokea na uhitaji wa pesa utatakiwa na sio usubiri matatizo yakufikie ndio uone umuhimu wa kutunza akiba kabla. 

Njia nyingine nzuri itakayokifanya uwe na nidhamu ya pesa wakati wote ni kupunguza matumizi yasiyo na lazima na kujenga utaratibu wa kununua vitu vya jumla kuliko vya reja reja  na pia kusimamia lengo kuu kwa msimu kwa mfano kila mwaka uwe na lengo kuu la kufanya hivyo kwa namna yoyote utajibana ubaki na pesa ya kufanikisha lengo hilo  maana ukitumia hovyo pesa basi uwe tayari pia kulipoteza lengo hilo 


Mwanasayansi Saul Kalivubha 

0652 134707