Tuesday 8 December 2020

WASHABIKI WA MICHEZO TUWE NA KIASI



Habari za kwako ndugu msomaji wa blogu yetu pendwa karibu tena katika safu hii tuweze kuwekana sawa katika mambo halisi ya maisha yetu ya kila siku. 


Watafiti wa takwimu wanaendelea kuja na takwimu zenye kuongezeka kila siku katika mchezo wa mpira wa miguu kuwa na washabiki wengi zaidi Duniani,unweza usiwe mshabiki wa mpira lakini utakuwa tayari umeshangazwa na taarifa kadhaa kuhusu matukio ya washabiki wa mpira  mfano kujiua, kupigana mpaka kuvunja urafiki sababu tu ya upenzi wa mpira.Zamani hayo tuliyasikia katika nchi za ulaya lakini sasa mpaka nchini kwetu tayari kuna visa kadhaa vya kushangaza kutoka kwa mashabiki wanaojiita kindakindaki. 


Nimeona vyema kuchagua eneo la mpira wa miguu kwa sababu ndiko visa vingi hutokea huko lakini upo ushabiki wa aina nyingi mfano ushabiki wa ndondi, muziki nk, ikiwa sio mshabiki wa mpira lazima kuna eneo jingine unashabikia kwani ushabiki ni moja ya hitaji la kihisia la kila mtu hivyo lazima kuna eneo tu wewe ni mpenzi. 


Ushabiki ni eneo la kihisia ambalo humpa utulivu wa kihisia mshabiki wa eneo hilo  mfano mshabiki wa timu fulani hujisikia vizuri pindi anaposikia taarifa za kupendeza kuhusu timu yake na hujisikia vibaya pindi akisikia taarifa zisizo pendeza kuhusu timu yake anayoshabikia ndio maana tunasema ushabiki ni eneo la kihisia na lenye uraibu ( addiction ) hivyo kadri unavyozidi kuwa karibu na eneo unaloshabikia ndivyo unazidi kuwa kupoteza uwezo wa kujizuia na hatimaye kufikia kiwango cha kufanya jambo lolote la kushangaza kisa ushabiki,bila shaka umewahi kusikia watu wakitembea utupu kwa sababu tu wamefunga au kufungwa.


Eneo lolote linalotawaliwa na hisia huwa linahitaji uwezo mkubwa sana wa kujizuia pia kwani maamuzi ya kihisia huwa ni ya kushangaza siku zote na ndio maana somo letu leo linasema tuwe na Kiasi kwenye ushabiki,ushabiki uwepo lakini usiathiri maisha mengine kuendelea mpaka kuvunja urafiki na undugu. 


Kuwa mshabiki kwa wakati na baada ya hapo endelea na maisha mengine ya kawaida kwa mfano ikiwa kesho timu yako inacheza  basi leo endelea na mambo yako mengine kawaida kabisa na ikifika kesho muda stahiki nenda kashabikie uwanjani,kibanda umiza au redioni na rafiki zako pengine na baada ya mchezo kuisha kaendelee na miasha yako mengine kabisa bila kuathiriwa na matokeo ya mchezo na hapo utakuwa tayari umejipa kiasi katika ushabiki. 


Kwa nini uwe na kiasi katika ushabiki ? Kama sio wewe basi utakuwa umewahi kusikia au kushuhudia mtu siku moja kabla ya timu yake kuwa uwanjani anakuwa bize na timu hiyo na kuacha shughuli zake nyingine za ki uzalishaji kwa siku nzima na kesho pia hivyo hivyo na ikitokea timu yake pengine inafungwa basi mpaka kesho kutwa yake bado atakosa msukumo wa kuendelea na shughuli zingine za ki uzalishaji,kwa hali hiyo tayari huna kiasi bali mtumwa wa ushabiki .


Malipo ya ushabiki sio pesa bali ni msawazo tu wa kihisia,ukilijua hilo nafikiri utakuwa na kiasi cha ushabiki kwani kuna maisha mengine yataendelea yanoyohitaji pesa sasa ukiacha shughuli kwa siku tatu utakuwa umepotea kiasi gani? Matajiri wengi Duniani ni washabiki wa mpira lakini utakubalina na mimi kuwa wana kiasi katika ushabiki ndio maana ukifuatilia huwa wanajitokeza au kuongea sana siku ya tukio na baada ya hapo watakuwa kimya kuendelea na maisha mengine ya ki uzalishaji pengine ikiwa ni wameajiriwa kushabikia na wanalipwa pesa ndio muda wote wote watakuwa ki ushabiki kwa sababu ndio eneo lao la ajira. 



Pengine ulianza taratibu kuwa mshabiki na sasa umefikia hatua ya uraibu kiasi cha kukosa kiasi katika ushabiki basi tambua kurudi kuwa na kiasi inawezekana pia japo sio kazi ya siku moja lakini unaweza kuanza na kanuni hii kubwa isemayo kwamba sio lazima kila mchezo uhudhuria au kuangalia ,yaani uwe na uwezo wa kuacha kufuatilia ushabiki na sio uwe na uwezo wa kuacha shughuli uende kushabikia hivyo siku michezo ukichezwa na wewe upo kibandani kwako kibiashara basi endelea na biashara bila kuathiriwa  na matokeo ya kutokwenda kwako uwanjani kwa maneno mengine ushabiki uwe ni sehemu tu na sio sehemu kamili katika maisha yako.


Makala hiii imendikwa na Saul Kalivubha,Mwanasayansi tiba katika maabara za binadamu kitaaluma na mwalimu. 


0652 134707