Tuesday 8 December 2020

WASHABIKI WA MICHEZO TUWE NA KIASI



Habari za kwako ndugu msomaji wa blogu yetu pendwa karibu tena katika safu hii tuweze kuwekana sawa katika mambo halisi ya maisha yetu ya kila siku. 


Watafiti wa takwimu wanaendelea kuja na takwimu zenye kuongezeka kila siku katika mchezo wa mpira wa miguu kuwa na washabiki wengi zaidi Duniani,unweza usiwe mshabiki wa mpira lakini utakuwa tayari umeshangazwa na taarifa kadhaa kuhusu matukio ya washabiki wa mpira  mfano kujiua, kupigana mpaka kuvunja urafiki sababu tu ya upenzi wa mpira.Zamani hayo tuliyasikia katika nchi za ulaya lakini sasa mpaka nchini kwetu tayari kuna visa kadhaa vya kushangaza kutoka kwa mashabiki wanaojiita kindakindaki. 


Nimeona vyema kuchagua eneo la mpira wa miguu kwa sababu ndiko visa vingi hutokea huko lakini upo ushabiki wa aina nyingi mfano ushabiki wa ndondi, muziki nk, ikiwa sio mshabiki wa mpira lazima kuna eneo jingine unashabikia kwani ushabiki ni moja ya hitaji la kihisia la kila mtu hivyo lazima kuna eneo tu wewe ni mpenzi. 


Ushabiki ni eneo la kihisia ambalo humpa utulivu wa kihisia mshabiki wa eneo hilo  mfano mshabiki wa timu fulani hujisikia vizuri pindi anaposikia taarifa za kupendeza kuhusu timu yake na hujisikia vibaya pindi akisikia taarifa zisizo pendeza kuhusu timu yake anayoshabikia ndio maana tunasema ushabiki ni eneo la kihisia na lenye uraibu ( addiction ) hivyo kadri unavyozidi kuwa karibu na eneo unaloshabikia ndivyo unazidi kuwa kupoteza uwezo wa kujizuia na hatimaye kufikia kiwango cha kufanya jambo lolote la kushangaza kisa ushabiki,bila shaka umewahi kusikia watu wakitembea utupu kwa sababu tu wamefunga au kufungwa.


Eneo lolote linalotawaliwa na hisia huwa linahitaji uwezo mkubwa sana wa kujizuia pia kwani maamuzi ya kihisia huwa ni ya kushangaza siku zote na ndio maana somo letu leo linasema tuwe na Kiasi kwenye ushabiki,ushabiki uwepo lakini usiathiri maisha mengine kuendelea mpaka kuvunja urafiki na undugu. 


Kuwa mshabiki kwa wakati na baada ya hapo endelea na maisha mengine ya kawaida kwa mfano ikiwa kesho timu yako inacheza  basi leo endelea na mambo yako mengine kawaida kabisa na ikifika kesho muda stahiki nenda kashabikie uwanjani,kibanda umiza au redioni na rafiki zako pengine na baada ya mchezo kuisha kaendelee na miasha yako mengine kabisa bila kuathiriwa na matokeo ya mchezo na hapo utakuwa tayari umejipa kiasi katika ushabiki. 


Kwa nini uwe na kiasi katika ushabiki ? Kama sio wewe basi utakuwa umewahi kusikia au kushuhudia mtu siku moja kabla ya timu yake kuwa uwanjani anakuwa bize na timu hiyo na kuacha shughuli zake nyingine za ki uzalishaji kwa siku nzima na kesho pia hivyo hivyo na ikitokea timu yake pengine inafungwa basi mpaka kesho kutwa yake bado atakosa msukumo wa kuendelea na shughuli zingine za ki uzalishaji,kwa hali hiyo tayari huna kiasi bali mtumwa wa ushabiki .


Malipo ya ushabiki sio pesa bali ni msawazo tu wa kihisia,ukilijua hilo nafikiri utakuwa na kiasi cha ushabiki kwani kuna maisha mengine yataendelea yanoyohitaji pesa sasa ukiacha shughuli kwa siku tatu utakuwa umepotea kiasi gani? Matajiri wengi Duniani ni washabiki wa mpira lakini utakubalina na mimi kuwa wana kiasi katika ushabiki ndio maana ukifuatilia huwa wanajitokeza au kuongea sana siku ya tukio na baada ya hapo watakuwa kimya kuendelea na maisha mengine ya ki uzalishaji pengine ikiwa ni wameajiriwa kushabikia na wanalipwa pesa ndio muda wote wote watakuwa ki ushabiki kwa sababu ndio eneo lao la ajira. 



Pengine ulianza taratibu kuwa mshabiki na sasa umefikia hatua ya uraibu kiasi cha kukosa kiasi katika ushabiki basi tambua kurudi kuwa na kiasi inawezekana pia japo sio kazi ya siku moja lakini unaweza kuanza na kanuni hii kubwa isemayo kwamba sio lazima kila mchezo uhudhuria au kuangalia ,yaani uwe na uwezo wa kuacha kufuatilia ushabiki na sio uwe na uwezo wa kuacha shughuli uende kushabikia hivyo siku michezo ukichezwa na wewe upo kibandani kwako kibiashara basi endelea na biashara bila kuathiriwa  na matokeo ya kutokwenda kwako uwanjani kwa maneno mengine ushabiki uwe ni sehemu tu na sio sehemu kamili katika maisha yako.


Makala hiii imendikwa na Saul Kalivubha,Mwanasayansi tiba katika maabara za binadamu kitaaluma na mwalimu. 


0652 134707

Wednesday 18 November 2020

IJUE MILANGO YA CHANGAMOTO NA JINSI YA KUIFUNGA



Habari ndugu msomaji wa blogu  yetu pendwa  , karibu tena katika mwendelezo wa masomo yetu


Kama sio kila siku basi pengine haishi wiki bila kukutana na changamoto au kumsikia mtu akilalimika dhidi ya changamoto anazopambana nazo,hivi umewahi kaa chini ukajiuliza kwa nini changamoto zikuandame? .


Ni kawaida kukutwa na changamoto  haijalishi ni changamoto za aina gani lakini huwezi kuishi bila kukutana na aina yoyote ya vikwazo ( changamoto) na hii ni kwa sababu ili  tuwe watu wapya ni lazima tusafishe vikwazo vilivyo katika njia zetu la sivyo itakuwa ngumu kusonga mbele, je changamoto hupitia wapi mpaka kutufikia sisi? 


Ipo milango ya changamoto ambapo asilimia kubwa ya changamoto kupitia huko hivyo ni muhimu kujua milango hiyo ili ikiwa kuna uwezekano basi marekebisho yafanyike kuzipunguza aina hizo za changamoto, bila shaka umewahi kuandamwa na aina fulani tu ya changamoto au umewahi kusikia mtu fulani akilalimika kusumbuliwa na aina fulani tu ya changamoto hayo ni matokeo ya kuacha mlango fulani wazi wa changamoto ndio maana changamoto hujirudia za aina fulani. 



Sifa uliyonayo, una sifa gani?  yaweza kuwa cheo, uzuri, upole  , utajiri  n.k , hapo nazungumza sifa yoyote ile ya mtu uliyonayo usipojitambua na kujidhibiti lazima kuna aina fulani za changamoto zitakufuata kwa sababu ya kuwa na sifa hiyo .Upole ni sifa  na kuna watu fulani watakufanyia mambo mabaya wakijua ikiwemo kukudhulumu pesa wakijua kwa upole wako utakaa kimya hivyo na wewe ukiendekeza upole wako basi utaandamwa na changamoto za kudhulumiwa kila siku , kuna watu wakijitambua wazuri huanzisha tabia fulani ya dharau  ambapo matokeo yake ni kuandamwa na changamoto za kukimbiwa na marafiki . Sifa yoyote uliyonayo yafaa kuiidhibiti isikupe maamuzi kwani itakuwa ndio mlango wako wa changamoto. 



Ufahamu wako, Karibu kila mtu endapo angeongezewa ufahamu zaidi pengine asingefanya maamuzi anayojutia leo kumbe tunafanya maamuzi kutoksna na ufahamu wetu wa sasa  hivyo ufahamu wako ni mlango wa changamoto fulani kwako  mfano  ukiona mtu anaandamwa na changamoto kujutia maamuzi yake kuna uwezekano mkubwa akawa na shida kwenye ufahamu anaotumia kufanyia maamuzi. Jitahidi kujiongezea ufahamu wa kutosha kwenye eneo ambalo unataka kulifanyia maamuzi la sivyo utakuwa unatumia taarifa chache kutoa hitimisho na kesho ukipata taarifa nyingine ndipo unaanza kujutia kuwa hitimisho uliyofanya sio sahihi. 


Mtindo wa maisha ( life style) , karibu kila mtu ana mtindo wake wa maisha yaweza kuwa ndivyo umezaliwa hivyo au ni uchaguzi wako umefanya kuishi hivyo lakini huo ndio mtindo wako wa maisha, mtindo wako ni upi? .Nakumbuka kipindi nipo shule nilikuwa na mtindo wangu wa maisha unaotakana na asili yangu ya kuumbwa na mtindo huo ilikuwa ni kupenda kutojichanganya  na watu nilikuwa mtu wa kukaa sana peke yangu mtindo huo ulifanya nikutane na changamoto za kukosa habari nyingi ikiwemo kukosa makundi ya kufanya nao mijadala  ya kimasomo ( discussion), nilikaa chini nikaona huo mtindo wangu utafanya nifeli hivyo nikajilizamisha kuwa mtu wa jamii ( social) ili tu nipunguze changamoto za kufeli masomo kwa kukosa watu wa kujadili nao.Nimekushirikisha mtindo wangu wa maisha bila shaka utakuwa umejitafakari ukaona kuna changamoto nyingi hazikuachi kwa sababu ya mtindo wako maisha , mtindo wako maisha  ni upi ? Kuna changamoto zinakufata kwa kuvutiwa na namna unavyoishi?  Jitafakari uchukue maamuzi ya kurekebisha mtindo wako inawezekana. 


Utakubaliana na mimi kuwa kama sio sifa yako basi itakuwa mtindo wako wa maisha au ufahamu wako ndio chanzo cha aina fulani ya changamoto zilikukuta au zinazoendelea kukufuata hivyo ni kazi kwako kujifanyia mabadiliko katika maeneo hayo ili kuzipunguza changamoto za aina fulani kukufuata muda wote .


Makala hii imeandikwa na Saul Kalivubha , Mwanasayansi tiba katika maabara za binadamu na mwalimu. 


0652 134707

Monday 26 October 2020

VITABU MLO KAMILI

 VITABU NI MLO KAMILI .


Habari ndugu msomaji wa blogu yetu pendwa na karibu katika safu hii ya kila wiki ya   vitabu na uchambuzi na leo tukiangazia  namna ambavyo vitabu ni chakula ambacho kina virutubisho vyote muhimu kwa afya ya mafanikio yetu , karibu. 


Usomaji wa vitabu ni utamaduni wa kawaida katika nchi za ulaya  lakini ni utamaduni mpya na usiopendwa na wengi katika nchi za Africa  licha ya kuwa uhamasishaji dhidi ya usomaji vitabu unazidi kukua Africa lakini wasomaji bado sio wengi  wa kuridhisha, leo naungana na wahamasishaji dhidi ya usomaji vitabu kukueleza kuwa maarifa ya vitabuni ni chakula cha ajabu sana, watalaam wa afya lishe wanahimiza kila siku kula chakula chenye karibu virutubisho vyote muhimu ili kuujenga mwili   na ili kupata mlo huo itakukagharimu  kuandaa menu yenye vyakula hivyo    kisha uende sokoni kununua na baadaye kuvipika na mwishoni kufurahia mlo huo  mezani .


Kwenye vitabu ni tofauti kidogo ndani ya kitabu kimoja mwandishi anakuwa kafanya maandalizi yeye kwa kufanya utafiti wa kutosha na kisha kukuwekea kwenye kitabu kimoja hivyo unapo kaa mezani na kitabu tayari upo kwenye mlo kamili wa maarifa  yaliyoandaliwa kwa weredi wa kutosha. Napoleon Hill mwandishi wa kitabu cha THINK AND GROW RICH  aliandika kitabu hicho miaka imepita  ( kabla ya vita ya pili ya Dunia)  lakini  bado ni mlo kamili mpaka sasa unajua kwa nini ni mlo kamili?  Maandalizi ya kuandika kitabu hicho yalifanyika kwa miaka isiyopungua ishirini kwa mwandishi kufanya mahojiano na watu mbali mbali waliofanikiwa ikiwemo mgunduzi maarufu wa bulbu Thomas Edson, unajisikaje kusoma kitabu kiliichoandaliwa kwa takribani miaka 25? tena kikiwa na mbinu za Thomas Edson ambaye hakukuta tamaa kwa kufanya majaribio zaidi ya 999 na kufanikiwa kwenye jaribio la 1000 .


Napoleon hill katupa mlo kamili kwenye kitabu chake aliyoandika miaka hiyo mpaka sasa ukiyasoma  bado ni chakula chenye virutubisho muhimu kwako, machache kati ya mengi ambayo mwandishi alijihakikishia kutoka kwa watu waliyofanya ni kutojipa ukomo wa uvumilivu  hili ni jambo muhimu sana miaka yote  kwa sababu tunashindwa kufikia malengo sio kwa sababu hatujui njia za kupita la hasha muda mwingine ni kwa sababu tunaishia njiani lakini njia ndiyo yenyewe, tunapata mbinu moja muhimu ya kutoichoka safari isemayo kabla hujakata tamaa jiambie nitafanya mara tano tena zaidi mfano umefanya biashara imekufa kabla ya kusema sitofanya tena biashara jiambie nitafanya tena mara tano zaidi nione matokeo. 


Kusoma vitabu ni tabia ya hekima  ya kujilisha kimaarifa  ambapo pishi linakuwa tayari limepikwa na mwandishi inabaki ni wewe kukaa mezani na kula chakula hicho chenye virutubisho vyote muhimu, mwandishi Napoleon hill katika kufanya utafiti wake wa kutuandalia mlo kamili  anatoa mbinu nyingine nzuri sana inayofanya kazi mpaka sasa nayo ni kuacha tabia ya kuaga kila mtu kabla ya kusafiri, mwandishi anasema unapotaka kuthubutu jambo jipya na ukataka ruhusa kutoka kwa watu wako wa karibu inawezekana idadi kubwa itakuonea huruma na hatimaye kukukataza usifanye kwa sababu ni hatari hivyo ukiwa na tabia ya kuaga kila mtu unaweza usiende uendapo kwani utakatazwa ni bora wengine waone matokeo ndio uwaambie uliwezaje , nenda kisha utarudi baadaye kuwaambia kuwa uliondoka . Thomas Edson aliweza kuthubutu mara elfu moja sio kwa sababu alikuwa na moyo mgumu wa kutokota tamaa kuliko watu wote Duniani la hasha pia hata tabia ya kutoaga kila mtu ilimsaidia wengi walikuja kuona tu matokeo.


Mwandishi bado akaendelea kutuonyesha kuwa vitabu ni mlo kamili kwa kutuletea mbinu zilizotumiwa na Henry Ford ( mwana mapinduzi katika ulimwengu wa magari) , mwandishi katika mahojiano na kampuni ya Ford hakuwa mchoyo kuziweka mbinu  wazi kwenye kitabu chake cha think and grow rich , moja ya mbinu aliyotuwekea ni  kufikiria kwa kuendana na nyakati kwa sababu sio mtu wa kwanza kugundua gari lakini alichokifanya ni ugunduzi wa gari kutokana na mahitaji ya jamii  na vipato vyao.Henry Ford alifariki mwaka 1947 lakini mpaka leo bado ujuzi wake na mfumo wake unatumiwa na watu mbalimbali wanaofanikiwa huoni kama vitabu ni mlo kamili? Mpaka sasa bado ukisoma kitabu cha think and grow rich unapata chakula ambacho hakijachachcha kutoka kwa mwandishi aliyetumia muda mrefu kukuandalia. 



Nyuma ya vitabu kuna maandalizi ya kutosha hadi kuja kukisoma wewe hivyo waandishi wanaingia gharama za kukutafutia viini lishe vyote muhimu na kukuwekea kwenye kitabu kimoja kazi ibaki kwako kula na kufanyia kazi, vitabu ni hazina na utajiri .


Makala hii imeandikwa Saul Kalivubha, Mwanasayansi tiba katika maabara za binadamu na mwalimu. 

0652 134707

JIAMBIE UKWELI UPIGE HATUA

 JIAMBIE UKWELI UPIGE HATUA 


Habari ndugu msomaji wa blogu  yetu pendwa na karibu tena katika safu hii ya kila wiki ya NASAHA ZA WIKI , leo tuna somo ambalo litafumbua macho yetu kuona hatua mpya mbele  hivyo tuambatane sote. 


Mara ya mwisho kujiambia ukweli ni lini?  Kwa uaminifu jipe majibu stahiki katika swali hilo  kwa sababu wengi tunajidanganya ndio maana leo nimekuja na somo hili ili tuone madhara ya kujidanganya na jinsi ya kuachana na tabia hiyo ya kujiadanganya .

Unapenda kudanganywa?  Jibu litakuwa hapana! sidhani kama kuna mtu hupenda kudanganywa  .Kudanganya  ni hali ya kuaminisha uongo utumike kama ukweli  mfano umelala kitandani unapigiwa simu ukiulizwa uko wapi?  Unajibu upo kazini  tayari hapo umemuaminisha uongo ya kuwa upo kazini lakini ukweli upo kitandani hivyo umemfanya mwenzako aamini ulichomuaminisha. Sifa ya uongo ni kuendelezwa hivyo ukidanganya mtu utajitahidi utafute tena mazingira ya uongo ili kuujazia nyama uongo wako uonekane ukweli  ndio maana mtu akidanganya kwa jambo moja kuna uwezekano mkubwa hata jambo la pili litalokofuata likawa sio la kweli .Bila shaka umepata picha ya uongo sasa tumeona mtu akiwa anadanganya mwingine ni vipi ukiwa unajidanganya? 

KUJIDANGANYA. 

Kujidanganya ni kutafuta usahihi kwa kuwalaumu wengine kwa makosa yako  mfano umechelewa kufika kazini hivyo ukachelewa pia kumaliza majukumu ya siku lakini  badala ujiambie ukweli kuwa tatizo ni kuchelewa ndio chanzo cha yote  wewe unajitetea kwa  kujiambia kuwa kazi zilikuwa nyingi sana hivyo kosa ni la mwajiri kukupanga peke yako kitengo hicho, tayari hapo umejidanganya kuhalalisha kuchelewa kwako kuwa sio tatizo bali tatizo ni la mwajiri. Tunajidanganya kila siku katika mambo mengi sana na hali inayofanya tujione kila siku tupo sahihi kwa 100% .

Wayajua madhara ya kujidanganya?  Moja ya dalili za kuwa mtu fulani anajidanganya ni hizi kuu mbili 

1.Kuwa na idadi kubwa ya watu ambao anawalaumu kila siku ikiwa sio watu basi atakuwa na idadi kubwa ya mazingira tofauti tofauti ya kuyalaumu mfano utasikia ni kwa sababu ya mvua, jua kali, foleni, nk na hata siku moja hutamsikia akisema ni sababu ya uvivu wake wa kuchelewa kuamka. 

2.Kuwa na changamoto zinazojirudia hii ni kutokana na sababu kuwa tatizo linakuwa ni yeye ila anajidanganya kuwa sio yeye na kwa sababu tatizo ndio mwanzo wa changamoto ndio maana changamoto za aina moja hujitokeza sana kwake mfano   mwanzo atakwambia tatizo ni pesa ndio maana hafanyi biashara lakini ukimpa pesa  tatizo atakwambia ni muda sio rafiki  na ukimpa muda wa kutosha utasikia akisema tena biashara anayotaka kuifanya sio msimu wake lakini pengine tatizo ni hofu yake au matumizi mabaya tu ya pesa  ndio maana changamoto ya kushindwa kuanzisha biashara imejirudia kila wakati. 

Dalili hizo mbili zinaonyesha wazi madhara apatayo mtu ambaye anakwepa ukweli kwa kuwajibisha wengine katika makosa yake  . Tatizo ukiwa ni wewe utalikwepa kwa kujitetea lakini matokeo ya tatizo hilo yatakurudia kila mara  hivyo utakuwa mtu wa kujitetea kila siku lakini makosa yale yale kila siku unarudia. Kujidanganya ni tabia inayofunga miguu yetu kutembea  kwa sababu huwezi kuendelea mbele ilihali bado hujatatua tatizo linalofanya miguu iwe mizito.  Mfano ukiwa unaendesha gari  betri ikapata shida taa zikazima  badala ya kushughurikia betri ipone wewe ukaamua utafute barabara mbazo zinataa za bararani ndio upite  hapo utakuwa unakwepa ukweli na tatizo litabaki palepale kwa sababu taa za barabarani zikizima na zenyewe? 

JIAMBIE UKWELI. Kila kwenye changamoto wewe tafuta uhusika wako uliofanya changamoto hiyo itokee kisha anza kupambana na tabia hiyo yako. Moja ya mbinu nzuri za kutumia ili uwe unajiambia ukweli ni kutafuta  muda wa tathmini binafsi  ikiwezekana kila wiki au kila mwezi au kila siku ni wewe tu jiwekee ratiba zako , katika kujitathmini huko binafsi   angalia changamoto unazokumbana nazo kwa siku/wiki/mwezi nk na jiulize kwa nini zinatokea na kuendelea kisha orodhesha sababu za kimazingira zinazopelekea changamoto hizo zitokee na orodhesha sababu kutoka kwako namna gani unachangia changamoto hizo zitokee kisha anza kujidhibiti na kujitibu na kama ikiwa ngumu kujitibu peke yako basi tafuta watalaamu wakusaisie.

Makala hii imeandikwa na Saul Kalivubha Mwanasayansi tiba katika maabara za binadamu na mwalimu. 


+255652 134707



Saturday 17 October 2020

TIBA YA HISIA ZILIZOJERUHIWA

 TIBA YA HISIA ZILIZOJERUHIWA. 


Habari ndugu msomaji wa blugu yetu pendwa ya fikiandotozako , leo tuna somo ambalo nina hakika litakuwa tiba kwa wahanga wengi  hivyo twende sambamba. 


HISIA ni msukumo ambao unahitaji kutimilizwa , mfano  mtu ukiwa na hisia za kupenda utafurahi ukipendwa, ukiwa na hisia za hasira utataka ufanye jambo fulani kuimaliza hasira n.k, sasa tunapata picha kuwa kila kwenye hisia kuna jambo litatakiwa kufanywa ili kutimiliza lengo la hisia.Tuangalie kisa  hiki ambapo najua kwa namna moja au nyingine utakuwa umewahi kuwa muhanga, mmepanga kukutana na rafiki yako mnayependana kweli   mara ghafla siku moja kabla anakutumia ujumbe kuwa hatoweza kuja tena siku hiyo kapatwa na dharura  hivyo mpaka siku nyingine kama wewe utajisikiaje? Kwa jibu la haraka utajisikia vibaya na sababu kubwa sio kuwa kakupotezea muda kama wengi wanavyodai la hasha ni kwa sababu ujio wake kwako ulikuwa ni tiba ya hisia fulani ambazo tayari zilikupanda pale tu mlipokubaliana  kukutana  tena kibaya zaidi mkiwa mna mahusiano ya kimapenzi ndio utatumia zaidi  kwa sababu kajeruhi hisia zako. 


KUJERUHIWA KWA HISIA. 

Tumeona kuwa kila kwenye hisia kuna jambo linatakiwa hivyo lisipofanyika basi hisia zako zitakuwa zimejeruhiwa. Jeraha la kuhisia ( psychological trauma)   linatofautiana ukubwa kutokana na aina ya hisia iliyojeruhiwa  mfano hasira uliyonayo dhidi ya mtu unayemdai na unataka uonane naye umwambie bayana endapo hutaonana naye utaumia lakini muda sio mrefu jeraha lake litapona utaendelea na maisha lakini hisia za kupenda ikitokea umempenda mtu  lakini mwenzako akawa msaliti na mwisho mkavunja uhusiano hilo jeraha lake  kupona sio rahisi na litakuathiri sana kama utakosa mbinu za kujitibu.


TIBA YA HISIA ZILIZOJERUHIWA. 


Bila shaka umewahi kuona watu wakiwa na tabia mpya punde tu baada ya kukutwa na maswaibu fulani, ulevi, wizi, uhuni , kuchelewa kuoa/kuolewa kwa kutoamini tena mahusiano  n.k, hayo ni moja ya matokeo ya kushindwa kujitibu majeraha ya hisia zilizojeruhiwa au  kujitibu kwa mbinu zisizo sahihi  kwa sababu baada ya hisia kujeruhiwa  kinachofuata  ni muhusika kutafuta tabia mpya itakayomsaidia kusahau maumivu  sasa hapo ndipo kuna tatizo  wengi huchagua tabia ambayo ndio badala ya kuwatibu ndio inawakandamiza zaidi mfano baada ya mtu kuachwa kwenye mahusiano anaamua kutokuwa tena muaminifu au kutowaamini tena watu tabia ambayo inamfanya aendelee kuteseka kwa sababu ataachwa tena kwa kukosa uaminifu. 


Hisia zinapojeruhiwa jitahidi ukubali kwanza hali  na pia katika machaguzi ya tabia mpya itayokufanya ujione sawa usichague vilevi  na wala usichague kulipiza kisasi bali chagua kujiboresha zaidi ili hata ikitokea tena basi sababu nyingi zisilalie kwako , fuata hatua hizi :


1.ikubali hali. 

2.Usianzishe tabia za kujisaulisha kwa muda  mfano kuanza ulevi n.k,bali tafuta tabia itayokuboresha zaidi 

3. Jipe muda mrefu wa kujiboresha ukiwa bora itakujengea kujiamini. 

4.Ukiridhika kuwa umejiboresha sasa unaweza kuendelea na maisha mengine na ukiweza epuka vichocheo vitavyokufanya ukumbuke namna ulivyojeruhiwa kihisia.


Makala hii imeandikwa na Saul Kalivubha ambaye ni Mwanasayansi tiba katika maabara za binadamu na mwalimu. 

0652 134707

Thursday 30 April 2020

UNATAFUTA MAISHA? HAYA HAPA.

UNATAFUTA MAISHA ? HAYA HAPA.

Karibu ndugu msomaji kwenye blogu yako hii pendwa ya FIKIA NDOTO ZAKO  ambapo tunajifunza mengi sana kuhusu maisha ya kila siku.Tupo kwenye hali ya taharuki nakusihi sana ufaute ushauri wa watalaamu na kwa ushauri wangu wa nyongeza katika uchumi kwa sasa kutunza pesa iwe lengo la kwanza  kwa sababu mfumo umeyumba kwa janga hili la Corona hivyo inahitaji utulivu sana kabla ya kuwekeza pesa yako vinginevyo utaisaidia Corona badala ya kujisaidia wewe, tuwe watulivu na hali hii itapita.


Tuachane na stori twende moja kwa moja kwenye somo letu maalumu kwa leo kabla ya vyote nikuulize na wewe upo kundi la watu wasemao " NINATAFUTA MAISHA" umewahi kuyapata? .

Kwa mujibu wa kamusi mbali mbali  MAISHA ni hali ya wewe kuwa mzima tayari hayo ni maisha  hivyo mtu ambaye ni mfu huyo hana maisha Duniani pengine huko aendako ( kuna imani nyingi kuhusu maisha baada ya kifo sitaki twende huko) .Tayari maisha unayo hivyo jivunie kuwa na maisha.
UHAI ni kitu ambacho kinafanya wewe  uwe na maisha mfano chakula ni uhai, maji ni uhai  nk kwa sababu ukivikosa unaweza kupoteza maisha ( kufa).
KUISHI ni namna ya kutetea maisha yako hapa ndipo kiini cha somo, maisha unayo lakini unafanya nini ili UISHI?

Ili uishi kuna mahitaji muhimu ya kwanza ambayo ni CHAKULA na MALAZI ( ule upate na pakulala) kwa sababu ukikosa chakula utakufa, ukilala nje uanaweza shambuliwa na wanyama wakali ukafa .

Mtu akiwa na Nyumba nzuri, gari zuri na kula vyakula vizuri ki kawaida hiyo ni hali ya kawaida na sio mafanikio ya kujitamba kwa sababu ni kawaida ule na upate pakulala ili kutetea uhai wako mambo ya gari ni ziada tu lakini gari halitetei uhai wako. Hatua hii ya kula na kuishi ni hatua ambayo kama umeifikia kujipatia mahitaji hayo tayari unatetea uhai wako  ( magonjwa , ajari nk ni changamoto tu katika kuwinda uhai wako).

HATUA YA PILI NA KUBWA. Kujitofautisha kutoka kwenye kutetea uhai wako tu mpaka kutetea maisha ya wengine hii ni hatua kubwa zaidi ambayo tunaiweka kwenye SAIKOLOJIA na FALSAFA  yaani kujitambua kuwa kuna zaidi ya kula na kulala na starehe. Hapa ni kutafuta wewe halisi ni nani, je ni mwimbaji? Mchezaji mpira  nk.

WEWE HALISI NI NANI? Watu wanaofanikiwa kujitambua hivyo huwa wanaonekana wa tofauti sana kwenye jamii  na kile wanachokifanya hakitetei uhai wao tu bali kuna wengine wanafaidika pia  mfano tuseme msanii Diamond kuimba kwake kuna mfanya atetee uhai wake lakini pia kuna ambao wameajiriwa naye lakini pia kuna watu ambao hisia zao zinapona kwa kusikia tu nyimbo zake.

UNATAFUTA MAISHA? Maisha unayo ila unatafuta namna ya kutetea uhai wako lakini namna nzuri usiishie kwenye kula, kulala na starehe ila tafuta wewe halisi ni nani? Tafuta kipaji chako na ukiishi. Kuishi kipaji chako ni nyongeza kubwa sana ya KUTETEA UHAI WAKO NA WENGINE. Kipaji sio kuimba tu na kucheza mpira au kuandika hapana hata ubunifu nao ni kipaji,kuchora, kushona  nk yaani ni vile tu unaishi kile ulichoombwa kufanya na njia rahisi ya kukijua ni msukumo wako wa ndani unajihisi furaha yako ipo ukiwa unafanya nini?

Makala hii imeandikwa na
Mwanasayansi Saul Kalivubha.
fikiandotozako.
Bila kusahau vitabu vya siri za urafiki na thamani ya changamoto vinapatikana kwa bei ya ofa kwa Tsh 6000 tu vyote, ni soft copy ( nakala tete).
 0652134707/ 0756388688.

Friday 21 February 2020

USIYOJUA KUMUHUSU SAUL KALIVUBHA

USIYOJUA KUMUHUSU SAUL KALIVUBHA.

Karibu sana ndugu mpenzi msomaji wa blogu yako pendwa hii ya fikiandotozako ambayo inakupa  mafunzo mbali mbali ya maisha na bila kusahau kutufuatilia katika majukwaa yetu ya Facebook, you tube na Instagram kwa jina moja tu la FIKIANDOTOZAKO,  Karibu sana.

Leo ni somo la tofauti sana kama zawadi kwako  ikiwa ni sherehe ya kumbukizi ya  siku ya kuzaliwa kwangu nikiwa natimiza umri wa miaka 28 , ulifikiri nina umri gani kabla?.Nawashukuru sana wazazi wangu na nyinyi wapenzi wasomaji kwa kuwa nami karibu katika kujifunza mambo mbali mbali ya maisha.

SAUL KALIVUBHA  ni nani? na itakusaidia nini kumfahamu? twende sambamba mpaka mwisho wa darasa kuna kitu utajifunza.

1.Ni mzawa wa Kigoma katika familia yenye uchumi wa kawaida sana (uchumi wa daraja la tatu) yaani uchumi wa mwisho kutokea  uchumi wa juu, uchumi wa kati na uchumi wa mwisho, hivyo Saul Kalivubha katokea familia yenye uchumi wa mwisho.

2.Ni mtu wa kundi la watu wasiowaongeaji sana na wenye usiri mkubwa sana (melancholic) , hili ni kundi la watu ambao muda mwingi hupenda kukaa peke yao kuliko kuwa na makundi, faida ya kundi hilo mojawapo ni kuwa wabunifu na wenye kufikiria sana lakini pia hasara moja wapo ya watu wa kundi hilo ni kuumia sana kwa sababu hukaa na mambo mengi moyoni bila kushirikisha wengine (marafiki).

3.Kasoma katika mazingira magumu kuanzia shule ya msingi mpaka shule ya upili, mazingira magumu yalimfanya atoke shule ya vipaji maalumu ya Musoma wavulana sekondari ya ufundi na kurudi shule ya kata ambapo alisoma kidato cha kwanza mpaka cha nne, hilo halikumkatisha tamaa zaidi ya kujitoa zaidi akiwa shule hiyo ya kata na kupata matokea mazuri ya kuendelea kidato cha tano na sita .

4.Maisha ya kidato cha tano na sita katika shule ya bwiru wavulana pia hayakuwa rahisi ki uchumi kwani ilimlazimu awe anasoma huku akitafuta pesa za kulipia michango midogo midogo ya shuleni.

5.Ugumu wa maisha ya shule hamkufanya akate tamaa hivyo alipambana na vikwazo na hatimaye akapata ufaulu wa kumfanya aendelee na masomo  ya chuo kikuu japo hakuweza kwenda mwaka huo aliomaliza shule (2014) na akaenda chuo mwaka uliofata (2015).

5.Mwaka 2015 aliweza kujiunga na chuo kikuu cha afya na sayansi shirikishi (Muhimbili) kwa kozi ya Mwanasayansi tiba wa maabara za binadamu (Medical laboratory science) .Maisha ya chuo hayakuwa magumu sana ki uchumi kulinganisha na hatua za nyuma hivyo kidogo unafuu ulionekaa wa maisha.

6.Maisha ya chuo yana changamoto nyingi sana lakini pia ni jukwaa zuri sana la kujifunza maisha kwa upana zaidi kwani unakutana na watu wengi mnaopishana mitizamo hivyo kupitia kupishana huko mtu unajifunza mambo mengi sana.

7.Safari ya uandishi ulianza rasmi akiwa chuoni mwaka wa pili ni safari isiyo rahisi lakini ilikuwa ndio mahala pake kwani kukutana na watu wengi wenye upeo tofauti ilimfanya ajifunze zaidi na kuanzisha jukwaa la FIKIANDOTOZAKO ambalo hadi sasa linafikia watu wengi nchini na nje ya nje katika kuwafungua vijana namna na kuwapa moyo wa kuendelea mbele.

8.Saul Kalivubha sasa sio mwanafunzi tena tayari ni muhimu  haijalishi changamoto zipi zilijitokeza lakini safari iliisha salama.Vikwazo vya maisha ni vingi sana  lakini hupaswi kusema nimeshindwa kwa sababu hakuna safari rahisi japo ugumu unatofautiana kulingana na aina ya safari uliyonayo.

9.kuna muda unahisi wewe utabaki hapo hapo ulipo kulingana na vikwazo vinavyofanya usione njia mbele, safari inakuwa na giza   na Dunia hata siku moja haitambui shida zako hivyo haiwezi kukuonea huruma. Muhimu ni kutoa imani  ya kubaki ulipo kwa sababu maisha ya leo yatakufunza funzo la kuishi kesho hivyo kesho utakuwa mtu mpya kabisa ni uvumilivu tu.

10.Uvumilivu sio kazi rahisi hata kidogo ni kazi ngumu sana kwa sababu silaha pekee ya uvumilivu ni IMANI  , unavumilia ukiwa na tumaini kuwa hali hiyo itapita na kweli itapita  kwa sababu  njia unazohisi zitakupa mafanikio ya haraka zina gharama iliyo nje ya uwezo wako zitakufanya ufilisike na bado hayo mafanikio usiyaone , tembea mwendo wako kwa kufuata nchi yako (Mungu aliyokuandalia).

Makala hii imeandikwa na.

 #Mwanasayansi Saul Kalivubha
  #0652 134707