Friday 18 February 2022

MBINU ZA KUISHI NA WATU WENYE TABIA NGUMU

MBINU ZA KUISHI NA WATU WENYE TABIA NGUMU MAKAZINI. 

Kama sio wewe basi utakuwa umewahi kutana na mtu akilalamika dhidi ya watu ambao wana tabia zisizo rafiki na pengine mpaka mtu huyo anatamani kuachana na kazi hiyo ili aepuke kukutana na watu hao , ni kweli wapo watu wana tabia ambazo ni ngumu kuvumilikika kiasi kiasi cha kufanya wengine wakose amani pindi wakiwa na watu watu hao wenye tabia zisizo rafiki. 

Pengine hata wewe kuna mtu ana tabia ambazo zimekufanya ujiulize swali hili " hivi huyu mtu anaishije na familia yake kwa tabia hizi?" Maana kama yuko hivyo kazini inakuwaje nyumbani kwa ndugu zake ambao wengine analala nao kitanda kimoja  na kula nao meza moja si pengine ikawa kila siku makwazo kwenye nyumba hiyo ? Lakini ukweli ni kuwa hakuna makwazo kabisa anaishi na familia yake vizuri tu kwa sababu  walipomfahamu walijifunza kuishi naye kwa kumzoea alivyo  changamoto ipo kwako ambaye hujazaliwa naye bado hujajifunza kuishi naye na pengine hutaki kujifunza kuishi naye. 

Hakuna namna utaishi bila kukutana na watu wenye tabia zote nzuri na mbaya ili uepuke hilo basi kajifungie kisiwani peke yako lakini tofauti na hivyo lazima utakutana na watu wenye tabia zote nzuri na mbaya sasa itategemea na watu hao umekutana nao wapi na wana nafasi gani kwako  kama ni kazini na ofisi moja je utaacha kazi kwa sababu ya watu hao?  Au utakuwa unakaa nje ya ofisi kuwakwepa watu hao ? Haiwezekani hilo na sio suluhisho lake lazima ujifunze kuishi nao watu hao. 

Jitahidi ujue mnapishana sana kwenye kipi kwa sababu sio kweli kwamba mtapishana kwenye kila kitu lazima tu kuna sehemu moja  ndio huwa chanzo cha kupishana naye na ukilitambua  eneo hilo basi tenga siku moja tafuta eneo tulivu jitafakari ni kwa nini mtapishana? na kwa nini eneo hilo? Anza kutengeneza mbinu za kuishi naye mtu huyo kwenye eneo hilo na moja wapo ya mbinu nzuri ni kutojibana naye sana kwenye eneo hilo jifunze kupuuzia baadhi ya kauli zake , pengine uone ugumu kukaa kimya pindi anapoongea kama tabia yake ilivyo lakini baadaye utazoea tu na itakuwa akiongea mambo yake unajibu machache mengine unamsikiliza. 

Mbinu nyingine ni kumpuuza kwenye baadhi ya mambo yake lakini usimuonyeshe kuwa unampuuza bali usifanyie kazi kila tukio lake kwako kwa mfano mmekutana kazini umemsalimia hajaitika au yeye hakusalimii  hilo lisikupe msongo wa mawazo kwa kujiuliza kwa nini haitikii salamu zako bali mpuuzie tu kwa sababu ndivyo alivyo na usiache kutabasamu pindi ukikutana naye na wala usilipe kisasi kwa anayokufanyia  na hapo itakuwa mwanzo wa wewe kuishi naye mtu huyo. 

Mbinu nyingine ya tatu ni kujitahidi unaepuka mazingira ya kukaa na mtu huyo muda mrefu ila isipokuwa pale tu inapobidi kwa sababu za kikazi tofauti na hivyo muepuke mtu huyo kwa kujishugulisha na mambo yako mengine. 

Mbinu nyingine ni usiitizame tabia yake kama kikwazo kwako bali muone kama ndivyo aliumbwa hivyo na ukiliweza hili basi usiwe unamuongelea jinsi alivyo mbele ya wengine bali muombee kubadilika kwa sababu tabia yake sio kwamba unaiyona wewe tu bali kuna wengine pia wanaiyona hivyo tabia yake inakuwa kikwazo kwake sio kikwazo kwako wewe kazi yako ni moja tu kujifunza kuishi naye 

Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul Kalivubha


+255652134707

Tuesday 1 February 2022

ELIMU YA PESA

 USISUBIRI PESA IPUNGUE NDIO UWEKE NIDHAMU YA MATUMIZI

Matumizi ya pesa bado ni changamoto kwa watu wengi na matokeo yake ni hujikuta katika ukosefu wa pesa mara kwa mara na hii sio kwa waajiwa tu hata waliojiajiri kwenye mambo binafsi  bado hujikuta kwenye kipindi kigumu cha ukosefu wa pesa sio kwa sababu haikuwepo la hasha ni kwa sababu ilikuwepo lakini ikatumiwa bila kuzingatia matumizi sahihi kutokana na kipato. Ukipata muda tulivu ukajitafakari utagundua kuwa pindi upatapo pesa matumizi yako yanakuwa juu na hupungua kadri pesa inavyopungua yaani kwa lugha rahisi  ni kuwa nidhamu yako ya matumizi ya pesa inaongezeka kadri unavyoishiwa pesa. 

Pesa ni nguvu ya kihisia ambapo usipoitawala itakutawala yenyewe kwa kukupa maamuzi mengi na hapo utakosa utulivu hali ambayo itafanya upoteze nidhamu ya matumizi ndio maana mshahara ukiingia unaweza jikuta unafanya manunuzi bila kuangalia ukubwa wa gharama kwa sababu unajua pesa ipo lakini ukianza kusikia mfuko umepwaya ndio utarudisha makini wa matumizi kwa mfano mwanzo ulilipwa laki tano na ilipofikia mfukoni umebaki na laki moja ndio utaanza kuipogia mahesabu hiyo laki moja kuangalia kama itakufikisha mwezi mwingine, je kwa nini hukufikiria hivyo tangu ukiwa na laki tano? 

Nidhamu ya pesa ni kuheshimu pato lako kwanza na pili ni kuheshimu matumizi sahihi yaliyo ndani ya kipato chako kama ulipanga kununua kitu cha shilingi mia ndio itakuwa sawa kulingana na kipato chako basi fanya hivyo lakini ulinunua kwa shilingi Mia mbili ujue umekula na pesa ya siku fulani hivyo jiandaye siku hiyo kukosa pesa la sivyo iwe ni dharura ndio tumia lakini kama si dharura yatakiwa ujidhibiti dhidi ya matumizi ya pesa pale tu unapoipata, changamoto ya pesa ni kuwa ukitumia pesa ndogo unaona kawaida tu lakini mwisho wa siku ukijumlisha unakuta kama ungehifadhi ungekuwa mbali sana kifedha hivyo nidhamu ukianza na kuheshimu matumizi yako yaliyo ndani ya kipato chako utakuwa kwenye kiwango kizuri cha kuweka akiba. 

Nidhamu binafsi katika matumizi ya pesa inajengwa na lengo kuu ulilonalo la kesho hapo ndio utakuwa unatumia pesa ukikumbuka kesho hivyo utakuwa ukijikumbusha kila kabla ya matumizi ambayo si salama kulingana na kipato chako na utakuwa na nidhamu muda wote, lazima uwe na nidhamu au ukose nidhamu lakini ukubali kupoteza lengo kuu la kesho na njia nzuri nyingine ni kuigawa pesa yako kwa siku utagundua unaingiza shilingi ngapi kila siku na kisha angalia matumizi yako kila siku yanaendana na pato lako la siku? Kwa kuanzia na hapo utajirekebisha kimatumizi na utaheshimu matumizi sahihi ya pesa. 

Pesa ikiwa nyingi itakupa upofu uuamini kuwa huwezi kuishiwa hivyo kila matumizi yakujiayo kichwani utayafanya na hapo ndio mwanzo wa kutumia hovyo pesa  mpaka baadaye ikipungua ndio itakutoa upofu uone kuwa kuna hatari itokanayo na ukosefu wa pesa kwa sababu pesa uliyonayo haitoshi kukufikisha msimu mwingine wa pesa kumbe kuna kuna nguvu kubwa inatakiwa uwe nayo awali ili kudhibiti hisia za pesa zisikutawale. 

Kujua unataka nini pia ni moja wapo wa ujenzi mzuri wa nidhamu ya pesa kwa sababu utajizuia dhidi ya matumizi ambayo sio ya msingi kwako na hayapo ndani ya bajeti yako kwa kipato chako na aina yako ya safari uliyonayo, kutojua nini unataka itakuingiza kwenye matumizi yasiyo sahihi kwa sababu kila utakachokiona kinavutia utahitaji kukinunua. 


Mwanasayansi Saul Kalivubha 

0652 134707