Monday 26 October 2020

VITABU MLO KAMILI

 VITABU NI MLO KAMILI .


Habari ndugu msomaji wa blogu yetu pendwa na karibu katika safu hii ya kila wiki ya   vitabu na uchambuzi na leo tukiangazia  namna ambavyo vitabu ni chakula ambacho kina virutubisho vyote muhimu kwa afya ya mafanikio yetu , karibu. 


Usomaji wa vitabu ni utamaduni wa kawaida katika nchi za ulaya  lakini ni utamaduni mpya na usiopendwa na wengi katika nchi za Africa  licha ya kuwa uhamasishaji dhidi ya usomaji vitabu unazidi kukua Africa lakini wasomaji bado sio wengi  wa kuridhisha, leo naungana na wahamasishaji dhidi ya usomaji vitabu kukueleza kuwa maarifa ya vitabuni ni chakula cha ajabu sana, watalaam wa afya lishe wanahimiza kila siku kula chakula chenye karibu virutubisho vyote muhimu ili kuujenga mwili   na ili kupata mlo huo itakukagharimu  kuandaa menu yenye vyakula hivyo    kisha uende sokoni kununua na baadaye kuvipika na mwishoni kufurahia mlo huo  mezani .


Kwenye vitabu ni tofauti kidogo ndani ya kitabu kimoja mwandishi anakuwa kafanya maandalizi yeye kwa kufanya utafiti wa kutosha na kisha kukuwekea kwenye kitabu kimoja hivyo unapo kaa mezani na kitabu tayari upo kwenye mlo kamili wa maarifa  yaliyoandaliwa kwa weredi wa kutosha. Napoleon Hill mwandishi wa kitabu cha THINK AND GROW RICH  aliandika kitabu hicho miaka imepita  ( kabla ya vita ya pili ya Dunia)  lakini  bado ni mlo kamili mpaka sasa unajua kwa nini ni mlo kamili?  Maandalizi ya kuandika kitabu hicho yalifanyika kwa miaka isiyopungua ishirini kwa mwandishi kufanya mahojiano na watu mbali mbali waliofanikiwa ikiwemo mgunduzi maarufu wa bulbu Thomas Edson, unajisikaje kusoma kitabu kiliichoandaliwa kwa takribani miaka 25? tena kikiwa na mbinu za Thomas Edson ambaye hakukuta tamaa kwa kufanya majaribio zaidi ya 999 na kufanikiwa kwenye jaribio la 1000 .


Napoleon hill katupa mlo kamili kwenye kitabu chake aliyoandika miaka hiyo mpaka sasa ukiyasoma  bado ni chakula chenye virutubisho muhimu kwako, machache kati ya mengi ambayo mwandishi alijihakikishia kutoka kwa watu waliyofanya ni kutojipa ukomo wa uvumilivu  hili ni jambo muhimu sana miaka yote  kwa sababu tunashindwa kufikia malengo sio kwa sababu hatujui njia za kupita la hasha muda mwingine ni kwa sababu tunaishia njiani lakini njia ndiyo yenyewe, tunapata mbinu moja muhimu ya kutoichoka safari isemayo kabla hujakata tamaa jiambie nitafanya mara tano tena zaidi mfano umefanya biashara imekufa kabla ya kusema sitofanya tena biashara jiambie nitafanya tena mara tano zaidi nione matokeo. 


Kusoma vitabu ni tabia ya hekima  ya kujilisha kimaarifa  ambapo pishi linakuwa tayari limepikwa na mwandishi inabaki ni wewe kukaa mezani na kula chakula hicho chenye virutubisho vyote muhimu, mwandishi Napoleon hill katika kufanya utafiti wake wa kutuandalia mlo kamili  anatoa mbinu nyingine nzuri sana inayofanya kazi mpaka sasa nayo ni kuacha tabia ya kuaga kila mtu kabla ya kusafiri, mwandishi anasema unapotaka kuthubutu jambo jipya na ukataka ruhusa kutoka kwa watu wako wa karibu inawezekana idadi kubwa itakuonea huruma na hatimaye kukukataza usifanye kwa sababu ni hatari hivyo ukiwa na tabia ya kuaga kila mtu unaweza usiende uendapo kwani utakatazwa ni bora wengine waone matokeo ndio uwaambie uliwezaje , nenda kisha utarudi baadaye kuwaambia kuwa uliondoka . Thomas Edson aliweza kuthubutu mara elfu moja sio kwa sababu alikuwa na moyo mgumu wa kutokota tamaa kuliko watu wote Duniani la hasha pia hata tabia ya kutoaga kila mtu ilimsaidia wengi walikuja kuona tu matokeo.


Mwandishi bado akaendelea kutuonyesha kuwa vitabu ni mlo kamili kwa kutuletea mbinu zilizotumiwa na Henry Ford ( mwana mapinduzi katika ulimwengu wa magari) , mwandishi katika mahojiano na kampuni ya Ford hakuwa mchoyo kuziweka mbinu  wazi kwenye kitabu chake cha think and grow rich , moja ya mbinu aliyotuwekea ni  kufikiria kwa kuendana na nyakati kwa sababu sio mtu wa kwanza kugundua gari lakini alichokifanya ni ugunduzi wa gari kutokana na mahitaji ya jamii  na vipato vyao.Henry Ford alifariki mwaka 1947 lakini mpaka leo bado ujuzi wake na mfumo wake unatumiwa na watu mbalimbali wanaofanikiwa huoni kama vitabu ni mlo kamili? Mpaka sasa bado ukisoma kitabu cha think and grow rich unapata chakula ambacho hakijachachcha kutoka kwa mwandishi aliyetumia muda mrefu kukuandalia. 



Nyuma ya vitabu kuna maandalizi ya kutosha hadi kuja kukisoma wewe hivyo waandishi wanaingia gharama za kukutafutia viini lishe vyote muhimu na kukuwekea kwenye kitabu kimoja kazi ibaki kwako kula na kufanyia kazi, vitabu ni hazina na utajiri .


Makala hii imeandikwa Saul Kalivubha, Mwanasayansi tiba katika maabara za binadamu na mwalimu. 

0652 134707

JIAMBIE UKWELI UPIGE HATUA

 JIAMBIE UKWELI UPIGE HATUA 


Habari ndugu msomaji wa blogu  yetu pendwa na karibu tena katika safu hii ya kila wiki ya NASAHA ZA WIKI , leo tuna somo ambalo litafumbua macho yetu kuona hatua mpya mbele  hivyo tuambatane sote. 


Mara ya mwisho kujiambia ukweli ni lini?  Kwa uaminifu jipe majibu stahiki katika swali hilo  kwa sababu wengi tunajidanganya ndio maana leo nimekuja na somo hili ili tuone madhara ya kujidanganya na jinsi ya kuachana na tabia hiyo ya kujiadanganya .

Unapenda kudanganywa?  Jibu litakuwa hapana! sidhani kama kuna mtu hupenda kudanganywa  .Kudanganya  ni hali ya kuaminisha uongo utumike kama ukweli  mfano umelala kitandani unapigiwa simu ukiulizwa uko wapi?  Unajibu upo kazini  tayari hapo umemuaminisha uongo ya kuwa upo kazini lakini ukweli upo kitandani hivyo umemfanya mwenzako aamini ulichomuaminisha. Sifa ya uongo ni kuendelezwa hivyo ukidanganya mtu utajitahidi utafute tena mazingira ya uongo ili kuujazia nyama uongo wako uonekane ukweli  ndio maana mtu akidanganya kwa jambo moja kuna uwezekano mkubwa hata jambo la pili litalokofuata likawa sio la kweli .Bila shaka umepata picha ya uongo sasa tumeona mtu akiwa anadanganya mwingine ni vipi ukiwa unajidanganya? 

KUJIDANGANYA. 

Kujidanganya ni kutafuta usahihi kwa kuwalaumu wengine kwa makosa yako  mfano umechelewa kufika kazini hivyo ukachelewa pia kumaliza majukumu ya siku lakini  badala ujiambie ukweli kuwa tatizo ni kuchelewa ndio chanzo cha yote  wewe unajitetea kwa  kujiambia kuwa kazi zilikuwa nyingi sana hivyo kosa ni la mwajiri kukupanga peke yako kitengo hicho, tayari hapo umejidanganya kuhalalisha kuchelewa kwako kuwa sio tatizo bali tatizo ni la mwajiri. Tunajidanganya kila siku katika mambo mengi sana na hali inayofanya tujione kila siku tupo sahihi kwa 100% .

Wayajua madhara ya kujidanganya?  Moja ya dalili za kuwa mtu fulani anajidanganya ni hizi kuu mbili 

1.Kuwa na idadi kubwa ya watu ambao anawalaumu kila siku ikiwa sio watu basi atakuwa na idadi kubwa ya mazingira tofauti tofauti ya kuyalaumu mfano utasikia ni kwa sababu ya mvua, jua kali, foleni, nk na hata siku moja hutamsikia akisema ni sababu ya uvivu wake wa kuchelewa kuamka. 

2.Kuwa na changamoto zinazojirudia hii ni kutokana na sababu kuwa tatizo linakuwa ni yeye ila anajidanganya kuwa sio yeye na kwa sababu tatizo ndio mwanzo wa changamoto ndio maana changamoto za aina moja hujitokeza sana kwake mfano   mwanzo atakwambia tatizo ni pesa ndio maana hafanyi biashara lakini ukimpa pesa  tatizo atakwambia ni muda sio rafiki  na ukimpa muda wa kutosha utasikia akisema tena biashara anayotaka kuifanya sio msimu wake lakini pengine tatizo ni hofu yake au matumizi mabaya tu ya pesa  ndio maana changamoto ya kushindwa kuanzisha biashara imejirudia kila wakati. 

Dalili hizo mbili zinaonyesha wazi madhara apatayo mtu ambaye anakwepa ukweli kwa kuwajibisha wengine katika makosa yake  . Tatizo ukiwa ni wewe utalikwepa kwa kujitetea lakini matokeo ya tatizo hilo yatakurudia kila mara  hivyo utakuwa mtu wa kujitetea kila siku lakini makosa yale yale kila siku unarudia. Kujidanganya ni tabia inayofunga miguu yetu kutembea  kwa sababu huwezi kuendelea mbele ilihali bado hujatatua tatizo linalofanya miguu iwe mizito.  Mfano ukiwa unaendesha gari  betri ikapata shida taa zikazima  badala ya kushughurikia betri ipone wewe ukaamua utafute barabara mbazo zinataa za bararani ndio upite  hapo utakuwa unakwepa ukweli na tatizo litabaki palepale kwa sababu taa za barabarani zikizima na zenyewe? 

JIAMBIE UKWELI. Kila kwenye changamoto wewe tafuta uhusika wako uliofanya changamoto hiyo itokee kisha anza kupambana na tabia hiyo yako. Moja ya mbinu nzuri za kutumia ili uwe unajiambia ukweli ni kutafuta  muda wa tathmini binafsi  ikiwezekana kila wiki au kila mwezi au kila siku ni wewe tu jiwekee ratiba zako , katika kujitathmini huko binafsi   angalia changamoto unazokumbana nazo kwa siku/wiki/mwezi nk na jiulize kwa nini zinatokea na kuendelea kisha orodhesha sababu za kimazingira zinazopelekea changamoto hizo zitokee na orodhesha sababu kutoka kwako namna gani unachangia changamoto hizo zitokee kisha anza kujidhibiti na kujitibu na kama ikiwa ngumu kujitibu peke yako basi tafuta watalaamu wakusaisie.

Makala hii imeandikwa na Saul Kalivubha Mwanasayansi tiba katika maabara za binadamu na mwalimu. 


+255652 134707



Saturday 17 October 2020

TIBA YA HISIA ZILIZOJERUHIWA

 TIBA YA HISIA ZILIZOJERUHIWA. 


Habari ndugu msomaji wa blugu yetu pendwa ya fikiandotozako , leo tuna somo ambalo nina hakika litakuwa tiba kwa wahanga wengi  hivyo twende sambamba. 


HISIA ni msukumo ambao unahitaji kutimilizwa , mfano  mtu ukiwa na hisia za kupenda utafurahi ukipendwa, ukiwa na hisia za hasira utataka ufanye jambo fulani kuimaliza hasira n.k, sasa tunapata picha kuwa kila kwenye hisia kuna jambo litatakiwa kufanywa ili kutimiliza lengo la hisia.Tuangalie kisa  hiki ambapo najua kwa namna moja au nyingine utakuwa umewahi kuwa muhanga, mmepanga kukutana na rafiki yako mnayependana kweli   mara ghafla siku moja kabla anakutumia ujumbe kuwa hatoweza kuja tena siku hiyo kapatwa na dharura  hivyo mpaka siku nyingine kama wewe utajisikiaje? Kwa jibu la haraka utajisikia vibaya na sababu kubwa sio kuwa kakupotezea muda kama wengi wanavyodai la hasha ni kwa sababu ujio wake kwako ulikuwa ni tiba ya hisia fulani ambazo tayari zilikupanda pale tu mlipokubaliana  kukutana  tena kibaya zaidi mkiwa mna mahusiano ya kimapenzi ndio utatumia zaidi  kwa sababu kajeruhi hisia zako. 


KUJERUHIWA KWA HISIA. 

Tumeona kuwa kila kwenye hisia kuna jambo linatakiwa hivyo lisipofanyika basi hisia zako zitakuwa zimejeruhiwa. Jeraha la kuhisia ( psychological trauma)   linatofautiana ukubwa kutokana na aina ya hisia iliyojeruhiwa  mfano hasira uliyonayo dhidi ya mtu unayemdai na unataka uonane naye umwambie bayana endapo hutaonana naye utaumia lakini muda sio mrefu jeraha lake litapona utaendelea na maisha lakini hisia za kupenda ikitokea umempenda mtu  lakini mwenzako akawa msaliti na mwisho mkavunja uhusiano hilo jeraha lake  kupona sio rahisi na litakuathiri sana kama utakosa mbinu za kujitibu.


TIBA YA HISIA ZILIZOJERUHIWA. 


Bila shaka umewahi kuona watu wakiwa na tabia mpya punde tu baada ya kukutwa na maswaibu fulani, ulevi, wizi, uhuni , kuchelewa kuoa/kuolewa kwa kutoamini tena mahusiano  n.k, hayo ni moja ya matokeo ya kushindwa kujitibu majeraha ya hisia zilizojeruhiwa au  kujitibu kwa mbinu zisizo sahihi  kwa sababu baada ya hisia kujeruhiwa  kinachofuata  ni muhusika kutafuta tabia mpya itakayomsaidia kusahau maumivu  sasa hapo ndipo kuna tatizo  wengi huchagua tabia ambayo ndio badala ya kuwatibu ndio inawakandamiza zaidi mfano baada ya mtu kuachwa kwenye mahusiano anaamua kutokuwa tena muaminifu au kutowaamini tena watu tabia ambayo inamfanya aendelee kuteseka kwa sababu ataachwa tena kwa kukosa uaminifu. 


Hisia zinapojeruhiwa jitahidi ukubali kwanza hali  na pia katika machaguzi ya tabia mpya itayokufanya ujione sawa usichague vilevi  na wala usichague kulipiza kisasi bali chagua kujiboresha zaidi ili hata ikitokea tena basi sababu nyingi zisilalie kwako , fuata hatua hizi :


1.ikubali hali. 

2.Usianzishe tabia za kujisaulisha kwa muda  mfano kuanza ulevi n.k,bali tafuta tabia itayokuboresha zaidi 

3. Jipe muda mrefu wa kujiboresha ukiwa bora itakujengea kujiamini. 

4.Ukiridhika kuwa umejiboresha sasa unaweza kuendelea na maisha mengine na ukiweza epuka vichocheo vitavyokufanya ukumbuke namna ulivyojeruhiwa kihisia.


Makala hii imeandikwa na Saul Kalivubha ambaye ni Mwanasayansi tiba katika maabara za binadamu na mwalimu. 

0652 134707