Tuesday 27 February 2024

IFIKE MUDA UJANJARUKE NA WEWE KATAA KUFANYWA FURSA ISIYO NA FAIDA KWAKO

 IFIKE MUDA UJANJARUKE NA WEWE KATAA KUFANYWA FURSA ISIYO NA FAIDA KWAKO. 


1.Unakubalije kuwa na mtu ambaye kila akikutafuta basi ana shida. 

2.Unakubalije kuhusiana na mtu ambaye bila wewe kumtafuta basi mahusiano ndio yanakufa .

3.Unakubalije kuwa na rafiki ambaye anataka umtimizie mambo yake kila anapotaka la sivyo anakuchukia 

4.Unakubalije kuwa mtu wa kuonewa hovyo hovyo?


WATU WA HOVYO WANAWEZA KUWA KIKWAZO KWAKO KUFANIKIWA. 


Kuna watu lazima ufanye tu maamuzi magumu ya kuwaepuka na hapo ndipo utagundua kuwa walikuchelewesha kwa sababu utaanza kuona matokeo chanya kwako.


Taarifa isiyopendeza ni kuwa kuna watu wamekusoma vya kutosha na wamekuona hujielewi hivyo wanakutumia kama mtatuzi wa shida zao huku wewe ukiendelea kuangamia taratibu. 


Kila siku jifunze kuhusu watu bila kusahau kuwatathimini marafiki zako ili ujue nani yupo kwako kweli na nani yupo kwako kukutumia hovyo. 


Mwanasayansi Saul kalivubha

Fikia Ndoto zako 

+255652 134707

Sunday 18 February 2024

KAMA LENGO LAKO KUU NI KUZAA ILI WATOTO WAJE KUKULIPA FADHILA KWA MALEZI BASI NAKUSHAURI HAIRISHA KUWA MZAZI KWA SABABU WEWE NI MJASIRIAMALI NA SIO MZAZI.

 KAMA LENGO LAKO KUU NI KUZAA ILI WATOTO WAJE KUKULIPA FADHILA KWA MALEZI BASI  NAKUSHAURI HAIRISHA KUWA MZAZI KWA SABABU WEWE NI MJASIRIAMALI NA SIO MZAZI.

Ni ushauri tu sio lazima ufuatwe na wote ila unaweza kuutafakari kabla ya kuupinga kwa mihemko ya hoja zisizo na mashiko.Kama hujui kwanini tunazaliana sio vibaya ukapitia upya tena hata maandiko ya Mungu ili uone hata huko lengo kuu halisemi  kuzaa ili watoto waje kukulipa fadhila kwa malezi yako na kama hapo bado haitoshi basi Jaribu kukaa na wazee hasa wenye umri wa miaka sitini utasikia wengi wao wakilalamika kuwa watoto wao hawawasaidii ila usikomee hapo nenda kafuatilie maisha ya hao wanaopewa lawama utakuta maisha yao bado pia yanahitaji utegemezi yaani bado hata wao hawajajimudu sasa swali ni je ni sawa kulaumiwa?

Kama sio changamoto mfano kubakwa na kusababishiwa ujauzito basi usikurupuke kuwa mzazi ilihali hujajua kwanini unatakiwa kufanya hivyo.


Usiwe  mzazi kwa ulimbukeni tu  bali jiulize upo tayari kulipa gharama za kuwa mzazi? Au ndio unataka uwe yule mzazi ambaye anatoa malezi kwa mkopo ili baadaye alipwe?

Kuna watoto hawasemi tu ila ukweli wanashindwa kuwaelewa wazazi wao kwa sababu mpaka wanatamkiwa maneno ya laana kwa sababu tu hawataki kuwalipa fadhila wazazi wao , wazazi wamekuwa wakiwatamkia maneno makali na kusema bila aibu kuwa waliuza sijui nyumba ili watoto wasome sasa huo ni wajibu wa mzazi kumuandaa mtoto ikiwemo kumpa elimu sio uje kumdai baadaye naye akulipe.

Mzazi jiandaye vizuri kabla ya kuwa Baba au mama na elewa kuwa utatakiwa kuwajibika kimalezi bila kufikiria kulipwa fadhila.

Watoto wengi wamekuwa wanaishi kwa kukosa utulivu kwa sababu wanalazimishwa kuwajengea wazazi nyumba bila hivyo wanatishiwa kupewa laana sasa Kama umri wako wote wa ujana umeshindwa kujenga na tena usikute ni kwa uzembe wako tu iweje uwabane watoto wakufanyie hivyo na kibaya zaidi unakuta ndio kwanza mtoto kapata ajira au ndio kwanza anajitafuta ila tayari mezani umemlundikia matatizo yote ambayo wewe ukiwa na nguvu yalikushinda.

Kushindwa kujiandaa kwako mzazi ni chanzo cha matatizo kwenye familia za watoto wako kwa sababu mtoto ataogopa mpaka kuoa kwa sababu tu akijiongezea majukumu atashindwa kukuhudumia wewe na kwa wale ambao watalazimisha kufanya hivyo basi itazuka vita kati ya mzazi na mkwe wake kwa sababu mzazi ataamini hajaliwi kwa sababu mkwe ameingilia kati.Kwa mtoto wa kike naye ndio pale analazimishwa kuolewa na mtu mwenye pesa tu ili awe Kama kitega uchumi na kama sio hivyo basi ndio akiolewa anabanwa awe anatuma pesa mara nyingi mwisho wa siku mumewe anagundua hivyo tayari ndoa inaanza migogoro na yote hayo ni kosa tu la mzazi Kushindwa kujiandaa kujitegemea na kutaka watoto wamlipe fadhila.


Mzazi tambua kuwa kumtunza mtoto ni wajibu wako sio kumkopesha na jukumu la kujitunza wewe ni lako japo watoto wanaweza kukusaidia ila sio kitu cha kutegemea kwa sababu na wao wana majukumu ya kuanzisha familia na kujitafuta pia kiuchumi ili uzao uendelee, ukizeeka au ukawa unaumwa na huwezi kujimudu basi hapo watoto watachukua jukumu la kukutunza ila bado una nguvu na sio mzee unaanza kuwabana watoto wakulipe fadhila je wakaibe ? 

Kushindwa kujiandaa kwa mzazi ndio mwanzo wa kulaumiana kwenye familia mpaka ukoo na hii ni pale ambapo watoto wako mwenyewe unataka ndugu wakusomeshee na wakisema hawawezi tayari unawatupia lawama nyingi  tena bila aibu unaongea hata mbele za watu kuwa kina fulani hawataki kusomesha watoto zako ilihali wana pesa bila kufikiria kuwa na wao wana mizigo yao pia hata kama wana pesa ila unajua bajeti zao? Kilichofanya yote hayo ni wewe hapo kwanini lawama wapewe wengine?

Mzazi kamili hujiandaa yeye na kuwaandalia watoto pia na kwa kufanya hivi ni rahisi kuvunja mnyororo wa umaskini kwa watoto wakizaliwa wanajipambania  wao na wajukuu zao na sio tena uwape familia nyingine yaani wapambane kwa ajili ya watoto wao na huku pia wakupambanie wewe. 

Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul kalivubha 

+255652 134707

Saturday 10 February 2024

KAMA HIVI NDIVYO UNAVYOISHI MJINI NI BORA URUDI TU KIJIJINI UKAISHI KULINGANA NA KIPATO CHAKO

 KAMA HIVI NDIVYO UNAVYOISHI MJINI NI BORA URUDI TU KIJIJINI UKAISHI KULINGANA NA KIPATO CHAKO.

Yawezekana hii isiwe makala nzuri kwa waishiyo mijini huku wakijisifu kila siku na kuwabeza waishiyo vijijini ila ukimakinika na kuchukulia chanya basi kuna jambo utajifunza. Kuishi mjini ni ndoto ya wengi nafikiri inaweza kuwa zaidi ya asilimia hamsini ya watu wanatamani kuishi mjini na hasa kwenye miji ile mikubwa  lakini uhalisia ukoje huko mjini kwa wengi wao? Kuwa kwenye changamoto  mjini sio sababu pekee ya kusema uhame urudi kijijini/mkoani la hasha ! Hapa namaanisha kwa wale ambo mjini hawapawezi kabisa ila wanapang'ang'ania  tu kwa sababu zisizo na msingi.

Bila shaka utakuwa umewahi sikia ama kuona baadhi ya watu waishio mijini wakiwabeza watu waishio vijijini ama mikoani kama wasemavyo watu  wa Dar es salaam na kibaya zaidi hudiliki kusema watu wa vijijini ni washamba na wasio wabunifu wa maisha, Sio uongo kuwa kuishi mjini kunakomaza akili kulinganisha na kuishi kijijini kutokana na harakati kuwa nyingi mjini na panahitaji wepesi sana katika maamuzi ili uweze kumudu mjini lakini kwenye maamuzi hayo hayo kuna watu wapo mijini kuongeza idadi tu ya watu ila ki uhalisia wanaishi maisha magumu sana kwa lugha isiyo rasmi ni kuwa walikurupuka kuja mjini ilihali hawana mipango ya kuwafanya wanufaike na maisha ya mjini. 

Ikiwa unaishi mjini kwa sababu moja wapo kama  nimevyoelezea hapa chini  basi haraka toka mjini urudi mkoani/kijijini  ama jitafakari zaidi ubadili mtindo wako wa maisha.

Kuishi mjini ki ulimbukeni; Unaishi mjini kutaka tu uonekane nawe unaishi mjini yaani ukisimama na kujitambulisha ama kutambuliswa unaishi mjini hiyo ndiyo furaha yako kuu bila kujali hali ngumu unayokutana nayo huko mjini na kama hii ndio sababu pekee ya wewe kuishi mjini basi haraka ondoka mjini kwa sababu unaongeza tu idadi ya watu na usipokuwa makini maisha yatakuchapa  na kujikuta kwenye hali mbaya kimaisha mpaka kwa uzao wako pia, kwa sababu utatumia gharama kubwa kuwafanya watu wajue kuwa unaishi mjini ilihali hiyo gharama ungeitumia kuboresha maisha yako huko mjini, kila siku utakuwa mtu wa kuchapisha maudhui mitandaoni ya kukuonyesha upo mjini ambapo vocha zitateketea tu bure na hakuna unachokiingiza tofauti na sifa ambazo hazikuingizii pesa. 

Kuishi mjini kwa sababu umepazoea; Kuna mtu maisha ya mjini kwake ni magumu sana na kikawaida tayari yamemshinda ila  ukimpa fursa za kurudi mikoani/kijijini anaweza hata kukutukana na ukitaka kujua sababu anakwambia kapozea mjini hivyo itampa sana tabu kuanza tena upya huko mikoani  kama wewe ndio huyu jua kabisa mjini hapakufai ondoka haraka la sivyo jiandaye kuzeeka maskini.

Kuendelea kuishi mjini kwa maisha magumu ukiogopa kuchekwa endapo utarudi mkoani/kijijini; Huyu pia hafai kuishi mjini kwa sababu hatofautiani sana na mtu limbukeni na asiye na malengo,Huyu yupo tayari kufanya maamuzi ila anaogopa macho ya watu ilihali mjini pememshinda  kuishi sasa nawe jiandaye kuishi maisha magumu sana kwa sababu huna mbinu za kutatua changamoto ili umudu maisha ya mjini bali upo tu kuonekana mtoto wa mjini ilihali maisha yamekushinda .

Kuishi mjini huku unategemea mshahara tu kama chanzo pekee cha pesa na huna chachu yoyote ya kuongeza vyanzo vingine vya pesa; Hili kundi lina watu wengi sana na hapa ndipo utakuta mtu anaishi mjini kimateso sana na hana mpango wowote wa kujinasua na mateso hayo , Kwa mfano unategemea mshahara tu ndio ulipe kodi ya nyumba,ukupe  nauli zako za  kila siku kukupeleka kazini, ukupe ada ya watoto tena shule za mjini hawana huruma kama huna ada mtoto watamfukuza tu sasa hapo kweli utaishi maisha ya furaha? Sio kwamba kila siku utakuwa mtu wa kulalamika tu kwanini mishahara haipandi . Kama wewe ndio huyu ondoka haraka mjini urudi mkoani kwenye nyumba nzima unapanga elfu hamsini na bado zipo jirani na unapofanyia kazi hivyo  huna haja ya kulipa nauli , haya kwako yatakuwa maamuzi sahihi kwa sababu huko mjini pia umekaa tu hutaki biashara hivyo ni bora urudi kuishi kwa kutegemea mshahara sehemu yenye maisha rahisi. 

Kama unaishi mjini huku ukisifia tu maisha mazuri ya mjini na jinsi watu walivyo na majumba makubwa na magari ila wewe huna hiyo nyumba na wala gari pia ; kama wewe pia ni huyu basi  mjini hapakufai tena ondoka haraka kwa sababu upo kwenye kundi lisilo lako na mwisho wa siku shida utapata wewe, upo mjini kushangaa tu wengine wakifanya maendeleo ila wewe unaendelea kuwa mteja wao kwa  kuwaongezea kipato tu sasa unafanya nini mjini? 


Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul kalivubha 

+255652 134707 

Saturday 3 February 2024

MAMBO UNAYOTAKIWA UFANYE UKIWA NA UMRI KATI YA MIAKA 20 MPAKA 30

 KIJANA JITAHIDI USIJIPOTEZE UKIWA NA UMRI KATI YA MIAKA 20-30

Katika makuzi kuna mgawanyo wa hatua takribani nne ambapo karibu kila mtu kwa kudra za mwenyezi Mungu huzipitia, Vipindi hivyo hugawanywa kwa kuzingatia umri na matukio yake na pia kila kipindi ni muhimu zaidi katika kuandaa kipindi kingine hivyo kumbe hutegemeana.Japo hatua hizo za makuzi hutegemeana ila ipo hatua yenye changamoto nyingi na iliyomuhimu sana na mtu usipokuwa makini utajikuta unajipoteza na ukiwa makini zaidi utajipata .

UMRI KATI YA MWAKA 1 MPAKA MIAKA 18 , Huu ni umri wa kujidanganya sana na kutengeneza malengo ya ukubwani  na kwanini kujidanganya? Kwa sababu unakuwa unaona kila kitu kitawezekana bila kusubiriwa kwa mfano: Utaona utamaliza shule mpaka chuo na baada ya kumaliza tu utapata kazi ya kuajiriwa na pengine ukipata kazi tu utalipa fadhila kwa waliokusomesha /kukusaidia na kisha utaoa/kuolewa na ndani ya mwaka huo huo utapata mtoto wako wa kwanza. Hivi ndivyo wengi tulipanga tukiwa na umri huo na walio kwenye umri huo pia wapo wanapanga wakiamini maisha ni mstari mnyoofu hivyo kila kitu kitaenda bila shaka yoyote, Je ni vibaya kupanga? Sio vibaya ndio maana awali nikatangulia kusema kuwa huu ndio umri wa kujiona ukiwa mkubwa utakuaje, Kwanini ni umri wa kujidanganya? Tuone hatua ya pili kisha hili jibu litapatikana.

UMRI KATI YA MIAKA 20- 30 ( UMRI WA UHALISIA) Huu ndio umri wa kuona vitu kwa vitendo kwa namna kijana alivyojichora akiwa na miaka 18 kurudi nyuma,Kwenye umri huu ndio utaona maisha ni mstari mnyoofu ama ni mstari wenye kona nyingi? Katika umri huu kwa wale ambao walienda shule wengi humaliza elimu zao mpaka za vyuoni na kikawaida ndipo wanakaribishwa rasmi mtaani na hapa ndipo uhalisia unaonekana.

Katika umri huu mambo mengi yanakuja kinyume na namna mtu alivyofikiri japo yanatimia ila kuna kitu kinaitwa Subira ndio hasa kinafaa kitumike kwenye umri huo kwa sababu ukiwa mtu wa pupa lazima utakata tamaa na kuona maisha ni magumu sana.

Sio ajabu kumaliza shule ukajikuta unapata kazi baada ya miaka mitano tofauti na ulivyojiona kuwa utamaliza leo na kesho utaitwa kazini.

Sio ajabu ukaoa/ kuolewa nje umri uliojipangia kwa mfano ulijua utamaliza tu chuo utaingia kwenye familia ila unamaliza unakaa tena miaka mitano mbele ndio unaanza familia. 

Sio ajabu ukaingia kwenye familia mapema tu ila ukakutana na  changamoto za uzazi ukajikuta unapata mtoto wa kwanza baada ya miaka 7 ya ndoa tofauti na ulivyoona ukiingia tu leo kwenye ndoa basi kesho tayari mimba na hata usijaliwe kupata maana yote ni mipango ya Mungu.

Sio ajabu ukavuka miaka 20 bila kuwa na kiwanja wala nyumba ukiwa bado umepanga au hata kuishi kwa wazazi  tofauti na ulivyojiona kumiliki nyumba na usafiri ukiwa kati ya  miaka 20 tu.

Hayo ni baadhi ya matukio ambayo yapo na wengi huyapitia na ndio inakuja ile sababu ya huu umri kuitwa umri wa UHALISIA, na huu umri unatufundisha kuwa maisha sio mstari mnyoofu na kutokuwa mstari mnyoofu haimaanishi kuwa malengo hayawezekani la hasha bali subira inatakiwa sana katika umri huo la sivyo utajipoteza kwa kuwa mtu mwenye haraka na mwisho wa siku unaishi maisha yasiyo ya uhalisia wako kwa mfano ulihisi utapata nyumba na gari haraka sasa ili kutaka yawezekana unaingia kwenye wizi au kwa waganga wa kienyeji wanakwambia utoe kafala mwisho wa siku unaishia gerezani .

Umri huu hutakiwi kuwa na haraka bali kuwa na juhudi tu za kupambania ndoto zako na sio lazima zije kwenye mstari mnyoofu ila ikitokea zinakuja kwenye unyoofu basi shukuru Mungu kwa hilo maana upo kwenye kundi la wachache ambao mambo yao yanakuwa kwenye unyoofu pasi na chenga.Usikubali ujipoteze hapa kwa sababu ukijipoteza kuna uwezekano mkubwa nyakati zitazofuata zisikusaidie kujipata tena.

UMRI KATI YA MIAKA 40- 55, Huu ni umri wenye matukio mawili makubwa la kwanza ni kukubali matokeo  huku ukilazimisha uendelee kuonekana kijana wa miaka 30 ,hii ni wale ambao walikata tamaa na kuona maisha ndio haya haya hivyo wanaamua kuridhika lakini changamoto nyingine inayowakabiri ni kupingana na umri yaani hawataki kukubali kuwa wao ni watu wazima na utajigundua hivyo pale ukianza kuona  unalazimisha kufanya vitu visivyo endana na umri wako, kitaalamu hiki kipindi kinaitwa mid age crisis(kuupinga utu uzima)

Tukio la pili ni wale ambao hawakukata tamaa hivyo wanaendelea kujitafuta na uwezekano wa kujipata upo  .

Changamoto kubwa kwenye umri huu ni kuwa majukumu yanakuwa mengi sana hivyo utegemezi unakuwa mkubwa hivyo kama hukujipanga vizuri utakuwa unapata pesa ila zinaishia kwa wategemezi wako.

UMRI KUANZIA MIAKA 60 KUENDELEA, Hapa ni uzee tu na kupumzika ijapo bado kuna wengine wataendelea na kutafuta tu kama matokeo ya kushindwa kutumia ujana wao vyema au kushindwa kuweka mikakati mizuri ujanani. 

Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul kalivubha 

+255652 134707

Friday 2 February 2024

JIFUNZE KUTOFAUTISHA WATU HAWA WAWILI WANAOKUJA KWAKO KIMAHUSIANO

 JIFUNZE KUTOFAUTISHA   WATU HAWA WAWILI WANAOKUJA KWAKO KIMAHUSIANO.

Karibu tena ndugu msomaji kwenye blogu hii ya fikia ndoto zako kwa minajiri ya kuongeza maarifa, leo tutazame kidogo kuhusu aina hizi mbili za watu wanaokuja kwako kwenye mahusiano. 

Mahusiano sio kitu kigeni na hasa mahusiano ya kimapenzi yamekuwa yakiimbwa kwa ubaya na uzuri kila uitwao leo, kwenye hii Dunia kila mtu ni lazima ahusiane kama hutofanya hivyo kwenye mahusiano ya kimapenzi basi utafanya hivyo kwenye mahusiano ya kijamii hivyo hakuna namna unaweza kukwepa kuhusiana.

Kwenye mahusiano kuna kufaana na kushindwana ndio maana kila siku tunashuhudia matukio makubwa mawili ambayo ni watu kuendelea kuhusiana na huku wengine wakiafiana kuachana, Kwenye kuendelea kuhusiana haimaanishi kuwa wameendana kwa sababu kuna wengine wafanya hivyo kwa sababu tu wanajiona wamekosa pakwenda na kwenye kuachana yawezekana mnaendana ila mmoja tu kushindwa kuwa na subira ama kushindwa kujifunza kuishi na mwenziwe. 

Kuna makundi makubwa mawili ya watu ambao wanakuja/watakuja kwako kimahusiano hivyo ukiyafahamu hutopata shida ya kukabiliana na matokeo ya kila kundi.

Kundi la kwanza ni yule MTU ANAYEKUJA KUKUANGALIA KWELI WEWE NDIYE?

Huyo ni yule ambaye hajui nani anamtafuta hivyo atakuja kwako kama kubahatisha tu ukiwa ndiye atakaa na ukiwa siye ataondoka, hili ni kundi lenye watu wengi sana na kwa ufupi mimi huwa naliita kundi ambalo linajifuta kwenye mahusiano yaani bado wanachama wake hawajui kipi wanataka hivyo wanapoingia kwenye mahusiano wanakuwa mguu mmoja nje na mwingine ndani, utalitambuaje kundi hili? Huwa wana sifa zao zinazo fanana  kwa kiwango kikubwa.

TABIA YA WANAKIKUNDI HIKI NI KAMA ZIFUATAZO:

1.Wanakuwa kama waamuzi wa mpira tu muda mwingi wanatafuta makosa yako.

2.Hawana subira hivyo changamoto inayohitaji utatuzi wa pamoja wao ndio wanaichukulia kama mlango wa kutokea.

3.Hawasamii lengo moja ipasavyo hasa la kwanini wanahusiana yaani ukimuuliza kuhusu kesho yenu kwenye suala la pamoja anakuwa na maelezo mengi yanayokingana yenyewe, wapo hivi kwa sababu wanakuwa hawana uhakika kweli wewe ndiye?

4.Huwa hawatulii na mtu mmoja kwa sababu hawajui nani wanamtafuta hivyo hujikuta kwenye mahusiano na watu wengi 

5.Muda mwingi wanakuwa kama wapelelezi.

6.Kuachana kwao sio jambo dogo na muda mwingi watatishia hivyo hasa changamoto inapojitokeza.

7.Hawapendi kutafuta suluhisho bali wanakuwa kishari zaidi pindi amani inapotakiwa.

8.Wanakuwa na haraka sana na utalijua hilo kwa kuona wanataka mambo yawezekane bila kughairishwa kwa mfano mmepanga kukutana na bahati mbaya ukakutwa na changamoto na ukatoa taarifa ila kwake anaweza kutumia changamoto hiyo kama fimbo ya kukuadhibu na mkaachana.


Kundi la pili katika eneo hili ni MTU AMBAYE ANAKUJA KWAKO KUKAA.

Huyo anajua nani anamtafuta hivyo haji kwako kwa kubahatisha bali kajiridhisha kabla hajaja kwa lugha nyepesi hawa ni wale ambao hawapo kwenye majaribio labda wakukute wewe ndio upo kwenye majaribio uwakimbize ila ukiwa nawe upo tayari basi watajenga kibanda kwako na maisha yataendelea.

Hili ni kundi lenye wanachama wachache kwa sababu ili uwe mwanachama sifa ya kwanza lazima ujitambue vilivyo na ujue nani unamtaka.  Hili kundi ndio linafanya watu wasifie mahusiano na kuyaimba kwa uzuri wake , wanachama wake wana tabia zinazofanana na sio tabia nyingi hata.

SIFA ZA WANACHAMA WA KUNDI HILI.

1.Hawana mambo mengi hivyo wakija kwako hawaji kama waamuzi wa mpira bali wanakuja kujifunza kuishi na wewe na kufundishana pale mnapopishana.

2.Ni kundi ambalo halifichi lengo lao kuu na kupitia matendo utawaona hivyo pia.

3.Ni watafuta suluhu kwenye changamoto sio wepesi wa kutishia muachane.

Hizo ndio sifa za kila kundi na mpaka kufikia hapo natumai umejitambua upo kundi gani ama una uhusiana na mtu wa kundi gani , ikiwa upo kwenye kundi la kwanza ni bora uachane na mahusiano kwanza na uwekeze nguvu kubwa kwenye kujitafuta ili ujue nani hasa unamtafuta.

Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul kalivubha 

#fikia ndoto zako

+255652 134707