Sunday 12 November 2023

EPUKA MARAFIKI HAWA ILI UFANIKIWE

 KAMA UNA MARAFIKI HAWA HUWEZI KUFANIKIWA  


Marafiki ni sehemu ya maisha ya kila siku maana sio rahisi kuishi bila marafiki hata mtu awe na tabia ngumu vipi kiasi cha kuonekana havumiliki ila tambua ana marafiki ambao wanamvumilia na tena wanapendana. Kitu ambacho wengi hatukijui ni mahusiano kati ya marafiki na mafanikio, kuna mahusiano makubwa kati ya mafanikio yako na aina ya marafiki ulionao ndio maana kuna mwandishi na mwanafalsafa maarufu aliwahi kusema mafanikio yako ni wastani ya marafiki zako watano ambao mnatumia muda mrefu kuwa pamoja, kwa ufafanuzi wa haraka ni kuwa ukimuona maskini mmoja jua kuna maskini wengine watano anaoshirikiana nao na ukimuona  tajiri mmoja jua kuna matajiri watano anaoshirikiana nao .

Marafiki ni chachu ya mafanikio yako kwa sababu  ni ngumu kuwa na rafiki mfanya biashara ilihali wewe huna biashara kwani maingezi yenu yatapishana tu na kama ikitokea hivyo basi jua kuna unafiki kati yenu yaani maongezi yenu hayana maana na hakuna urafiki hapo kwa sababu.

Kabla hatujaenda kwenye marafiki wa kuwaepuka hebu angalia mifano hii na kisha jichunguze uone ukweli ulivyo.

Mtu ambaye anafeli sana jambo fulani Jaribu kuchunguza marafiki zake utakuta wanafarijiana kuhusu kufeli kwao.

Mtu ambaye ana starehe nyingi ambazo zimeguka kuwa kikwazo chake cha mafanikio Jaribu kumfuatilia utakuta ana marafiki ambao anashirikiana nao na wanajiona wapo sahihi kabisa kufanya hivyo ndio maana wanaendelea.

Ukiona mtoto kuna tabia haachi jua kuna mtu anamuhamisisha kuendelea nayo hiyo tabia. 

Umeona mifano hiyo ? Bila shaka umepata mahusiano kidogo na pengine hata wewe kuna jambo unaendelea nalo kwa sababu kuna mtu nyuma ya jambo hilo , na mfano wa mwisho ni huu hebu angalia michango ya mtu maskini akiwa ana jambo lake kama harusi na kisha angalia michango ya jamaa zake kisha fanya hivyo hivyo kwa tajiri hapo utagundua kila mtu kachangiwa na marafiki wanaofanana uwezo  na hapo ndipo tunarudi kwenye ule ukweli kuwa upo sawa na marafiki zako.

Kuna marafiki ambao unatakiwa kuwakwepa  na kama unao basi tambua kuna hatua hutaziona za kimafanikio, marafiki hao ni hawa wafuatao :

Wanaolalamika sana;hawa watakuambukiza tabia ya kukwepa kuwajibika kwa makosa yako mwenyewe kwa sababu kwa tafasiri ya haraka ya mtu mlalamikaji ni kuwa haoni kuwa anakosea bali muda wote anaona wengine ndio wenye makosa na mwisho wa siku mtu anayelalamika sana huwa anaishia kuwa mtumwa wa wengine, ukiwa na marafiki hawa sio muda mrefu nawe utaanza kuwa mlalamikaji na kunyonyeshea vidole wengine kila muda. 

Marafiki wenye mitizamo ya kimaskini, hawa ni wale ambao wameridhika na hali zao za kuteseka na ukosefu wa fedha yaani tayari wameukubali umaskini, watu hawa wanakuwa na kauli nyingi za kutetea umaskini wao na pia huwa ni wavivu wa uthubutu  kwa sababu tayari wameshahalalisha umaskini wao na utawasikia mara nyingi wakijificha pia kwenye imani za Mungu kama vile kusema ni mpango wa Mungu wao kuwa hivyo na wengine huanini utajiri ni dhambi hivyo kila tajiri wanamuita mshirikina( freemason) ,Kaa mbali na watu hao watakuambukiza umaskini na ikitokea ni ndugu zako ambao huwezi kuwakwepa basi jua una kazi kubwa ya kufanya kutengeneza ukoo tajiri kutokea kwako.

Marafiki wanakutafuta tu kwenye uhitaji, hawa ni wale watu ambao kila mkikutana lazima kuna jambo upoteze , yaani ukiona simu yake tu basi jua lazima mazungumzo yenu yaishie na wewe kumpa kitu au kutoa ahadi utampa lini na ni  siku chache sana wao kukutafuta kwa mijadala mingine ya kimaisha, hawa watu hawakupa mawazo mapya bali wanakufanya uwafikirie wao tu tena kwa kuwapa vitu.Kusaidiana ni sehemu ya maisha ila epuka watu ambao muda wote wamekugeuza kituo cha msaada kwa sababu usipokuwa makini watakugruza mtumwa wao yaani watajiona muda wote wana haki ya kusaidiwa na wewe na siku ukikosa watajua umefanya makusudi watasahau siku ulizowasaidia na kuanza kukulaumu na kumuona yule ambaye hajawsaidia hata siku moja ndio mtu mzuri anayefaa.

Marafiki wanaotaka wewe tu ndio uwatafute, Kaa nao mbali kabisa tena ukiweza futa hata mawasiliano yao na kama ni ndugu  basi ishi nao kama wanavyoishi na wewe acha kuwatafuta mpaka pale kwenye ulazima wa kufanya hivyo kwa sababu ukikubali tu kuwa mtu wa kuwatafuta wewe muda wote jua utakuwa mtumwa wao na utaanza kuwafikiria wao muda wote hali ambayo itafanya ushindwe kufikiria ya kwako vizuri na ushindwe kwenda mbele kwa sababu wao wapo nyuma maana huo ujasiri utaukosa na usipokuwa makini utajikuta kwenye madeni ya kukopa mpaka muda wa maongezi ili tu uwasiliane nao na huku kwenye simu zao wana salio la kutosha , mtu ambaye anataka wewe tu ndio umtafute sio kwamba hiyo ni tabia yake bali kisha ona udhaifu wako na hili uthibitishe hilo fuatllia watu wake wa karibu je anawafanyia kama wewe?

Marafiki wajuaji , hawa ni wale ambao wanakukosoa hata kabla hawajakusikiliza na tena wanamalizia ulichokianzisha bila kujua ungemaliziaje, hawa ni marafiki hatari sana usiruhusu muda mwingi kuwa nao kwa sababu watakufunza ubishi usio na faida.

Marafiki waongo na wambea, Muongo ni mtu ambaye anakusambizia au kukuzuishia habari za uongo ila mmbea yeye ni yule ambaye anakusambazia habari za kweli ila bila idhini yako na kwa watu ambao hawakutakiwa kuzijua hizo habari, hao ni watu hatari sana kwa sababu watakufanya mweupe kwa kutoa siri zako na kufanya rahisi kwa adui zako kukushambulia na ukiwa na marafiki hao yawezekana mipango yako ikawa inasindwa kila mara kwa sababu kuna muda inanidi watu waone tu matokeo na sio maandalizi kwa sababu watakuzuia .


Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul kalivubha, mtafiti 


+255652 134707