Saturday 26 March 2022

MUMBO MUHIMU KABLA YA KUCHUKUA MKOPO

MAMBO MUHIMU YA KUJIULIZA KABLA YA KUCHUKUA MKOPO 

Mikopo ni mkombozi kwa watu wa tabaka zote  wenye kipato kidogo na matajiri pia hivyo sio kitu kibaya bali ni sehemu ya kujikomboa kiuchumi, mikopo hutolewa na taasisi nyingi za kifedha na hata zisizo za kifedha kuna mashirika na makampuni nayo hutoa mikopo vilevile, lakini mikopo yote hiyo huwa na masharti na sharti kubwa ni riba pamoja na ukomo wa muda wa kulipa huo mkopo na kabla ya mteja kukopeshwa lazima ukidhi vigezo ikiwemo pamoja na mteja kukubaliana na masharti kwa kutia saini fomu ya maridhiano hayo .

Makazini kuna kila aina ya watu katika suala la mafanikio na maamuzi pia, kuna ambao tayari wanahatua fulani katika maendeleo na kuna ambao bado kwanza wanaanza nikimaanisha waajiriwa wapya na wengine sio waajiriwa wapya bali kipato chao sio kikubwa kiasi cha kufanya mambo makubwa ya kifedha hivyo na hapo ndipo suala la kujilinganisha na waliowatungulia kunaanza lakini kosa huja pale ambapo hamasa ya kufanya vitu vikubwa ndani ya muda mfupi inamuandama mfanyakazi na bila kufikiria mara ya pili anaamua kuchukua mkopo ulio nje ya uwezo wake. 

Mfanyakazi kabla hujachukua mkopo kwanza hakikisha una ufahamu wako timamu na umejihakikishia kuwa masharti ya mkopo husika na muda husika wa ukomo wa mkopo wako umejiridhisha kuwa hakuna madhara makubwa utapata bali faida kubwa hapo sasa waweza chukua mikopo huo na isiwe una shauku ya kutaka mafanikio makubwa au ukawa umejilinganisha na wafanyakazi wenzako ukajiona uko nyuma kimafanikio sasa unataka uchukue mkopo ili ukimbizane nao kwa sababu hizo ikiwa ndio unazo basi hustahili kuchukua huo mkopo acha kabisa. 

Kabla ya kuchukua mkopo utambue kuwa kuna makato mengine yanafanyika kwenya mshahara wako wa msingi hivyo mkopo utakuja kuongeza asilimia ya makato yako kama ilikuwa unakatwa asilimia kumi sasa itakuwa pengine asilimia ishirini  hivyo utaweza kuishi kwa mshahara wa asilimia themanini mpaka hapo utakapomaliza kukatwa na wadeni wako? 

Jambo lingine muhimu la kuzingatia ni kuwa huo mkopo unachukua kwa ajili ya kutimizia jambo fulani sasa ikiwa ungeweka akiba ungefikisha kiasi sawa na mkopo unaotoka kuuchukua kwa miaka hiyo ambayo utamaliza kuulipa? ikiwa ndio basi tambua huo mkopo uko ndani ya uwezo wako na ikiwa huoni ikiwa hivyo jitafakari upya kabla ya kuingia huo mkataba wa mkopo. 

Kutokana na majukumu kuongezeka kila siku na kipato kuwa kilekile sio vibaya kufikiria mikopo kama suluhisho la kutatua uhuru wako kiuchumi hilo ni wazo zuri lakini isiwe ni kwa mihemko ukifanya kwa mihemko utajikuta kwenye matatizo na majuto ya kuulipa huo mkopo na pengine ukaingiwa na msongo wa mawazo hadi mwishowe ukaamua kujikatisha uhai wako wa thamani na wakati ikiwa ungekaa vizuri na akili yako ungepata maamuzi sahihi kabla ya kuuchukua huo mkopo.

Ikiwa ni mkopo unahitaji kwa ajili ya biashara basi jitahidi uwe na uhakika na wazo lako la biashara  kwa kufanya utafiti wa kutosha kujiridhisha kabla ya uanzishaji huo  na ikiwezekana usitumie pesa yote ya mkopo kwenye biashara bali anza kwa kiasi fulani kisha uende unaongeza mtaji taratibu kwa sababu mara nyingi biashara ikiwa unaanza huwa ni za majaribio chako zitakuwa nyingi sana na inaweza kufa na kuanza tena upya hivyo lazima ujihami katika hilo pia


Mwanasayansi Saul Kalivubha 


+255652 134707

Saturday 19 March 2022

ELIMU YA KUJIAJIRI KWA WANAFUNZI

 ELIMU YA  KUJIAJIRI IFUNDISHWE MASHULENI 

Katika karne hii ya 21 suala la  mtu kumaliza shule na kukosa ajira sasa sio geni tena kwa sababu ongezeko la wakosa ajira limekuwa kubwa sana na  sababu inaweza isiwe moja tu  serikali kushindwa kuajiri wasomi wake wote  bali hata mfumo wa maisha wa sasa umebadilika mbali na kuwa wimbi la wasomi linaongezeka kila siku lakini pia  ajira za watu sasa zinachukuliwa na mapinduzi ya kiteknolojia  mfano zamani ilitakiwa watu waajiriwe kukata tiketi lakini sasa tiketi zinakatwa na mashine hivyo anatakiwa mtu mmoja tu kuisimamia hiyo mashine. 

Baadhi ya viongozi hasa wana siasa wamekuwa wakihimiza suala la wahitimu wa vyuo vikuu kujiajiri  pindi wamalizapo masomo yao na wasitegemee kuajiriwa na serikali na mwisho wa siku kosa inaonekana ni la uvivu wa muhitimu kushindwa kujiajiri  lakini ki uhalisia sio kweli kwa sababu ni rahisi kumwambia mtu ajiajiri lakini kwa muhitimu wa chuo kikuu sio rahisi kwake kwa sababu zaidi ya miaka kumi darasani anaandaliwa kuajiriwa wafikiri siku moja tu itambadili mtizamo aliojengewa kwa miaka kumi? Serikali iweke mfumo wa mwanafunzi tokea shule ya msingi mpaka chuo kikuu hapo mazingira angalau yatakuwa rafiki kujiajiri kwa sababu msingi utakuwa umemjenga, kwa mfano mtu kamaliza taaluma yake ya ualimu kaandaliwa kufundisha sasa akimaliza ajiajiri vipi? afungue kituo cha kufundisha masomo kwa  ziada ( tuition) napo nado ni changamoto kwa sababu sasa serikali inahimiza wanafunzi wamakinike zaidi na darasani na sio kwenye  vituo vya kufundisha masomo kwa ziada hivyo inakuwa ngumu kutumia taaluma kujiajiri na kujiajiri kwenye mambo mengine nje ya taaluma ndio hayo ambayo mwanafunzi hakupewa misingi tokea mapema. 

Serikali kupitia mitaala ya elimu iweke masomo ya kufundisha maisha nje ya taaluma kwa nadharia na vitendo  kwa mfano kuwepo na somo la maisha na kujitegemea ambapo hapo mwanafunzi afundishwe stadi mbali mbali za kuyakabili mazingira tofauti na ile taaluma yake kwa mfano kama ni mwalimu afundishe ni namna gani anaweza kuyakabili mazingira bila kuwa na ajira hivyo apewe stadi hizo kama mbinu za kuanzisha biashara ndogo ndogo na namna ya kuikuza biashara hiyo na mwisho wa siku apewe mtihani wa vitendo kwa kuendesha mradi wa shule au kuleta ubunifu wa mradi hii itasaidia sana kumfanya mwanafunzi azoee mazingira mapema. 

Wanafunzi wengi bado wanaamini kujiajiri ni umaskini ndio maana  wengi wao hilo wazo la kujiajiri hata hawalifikirii na sio makosa yao kuwaza hivyo ni kwa sababu darasani hawakuambiwa ukweli kuwa kuna kukosa ajira na kuishi maisha nje ya ajira ndio maana kila muhitimu kilio chake ni kupata ajira, kuna uwezekano mkubwa wahitimu wakipewa hata mitaji wengi watashindwa kujitegemea kibiashara kwa sababu elimu ya kujitegemea haikufundishwa darasani  ni tofauti na mtu ambaye hakuendelea na masomo tayari akili yake aliiandaa kuwa hakuna namna anaweza kuishi bila kujiajiri mwenyewe hivyo anamakinika zaidi na mwisho wa siku anakuwa na elimu nzuri ya kujitegemea. 


Serikali iweke ukweli kwa wanafunzi mapema kuwa kuajiriwa sasa ni bahati ya wachache na tena kwa baadhi ya kada na iziweke wazi kada hizo na kwa kada zile ambazo ajira zake hazitoki sana basi zipunguziwe udahili vyuoni wachukuliwe wachache ili kuepusha mlindikano wa wahitimu wasio na ajira mtaani. Suala la kujiajiri kwa sasa inatikiwa iwe ni kama kampeni kwa wanafunzi kwa sababu hali ya wahitimu sio rafiki sana mtaani bado kuna umuhimu wa serikali kuingilia kati kwa kubadili mitaala ya elimu 


Mwanasayansi Saul Kalivubha 

+255652 134707

Sunday 13 March 2022

MBINU ZA KUWEKA AKIBA

 JINSI YA KUWEKA AKIBA 

Elimu ya pesa kila siku inakuwa changamoto mpya kwa watu wengi ndio maana  bado kuna watu wanaingiza pesa ya kutosha lakini matumizi yao sio rafiki kiasi cha kuwafanya wabaki na ziada ya pesa . Inawezekana hata wewe ukawa kwenye kundi hilo la watu ambao wanaweka malengo ya kujikomboa kiuchumi kila siku lakini utekekelezaji wake ni mdogo au haupo kabisa, ukijiona wa hali hiyo basi tambua una changamoto katika namna nzima ya kuitawala pesa  na njia rahisi kwa watu  hali zote za vipato ni uwekaji wa akiba na mipango madhubuti ya namna ya kuizalisha hiyo akiba ili nayo ilete faida. 

Akiba kwa tafasiri isiyo rasmi ni namna mtu anavyoijali kesho yake ndio maana leo unajinyima ili kesho ufanikiwe katika jambo fulani , mfano  unaingiza shilingi elfu kumi kila mwezi na unataka baada ya mwaka uwe na mtaji wa laki mbili hapo lengo ni wewe upate mtaji wa laki mbili lakini mfukoni una shilingi elfu kumi ambayo kila mwezi utaipata, kwa kawaida unaweza kuiona ndogo lakini  kuna uwekano mkubwa mtu asiifikishe kwa mwaka .

Kuna elimu nyingi kuhusu uwekaji wa akiba ambazo hutolewa kila leo na pengine ukawa moja kati ya watu ambao tayari wamewahi kuzitumia njia hizo lakini bila mafanikio yoyote, unafikiri tatizo ni nini?  Kuna kitu muhimu kutambua kabla ya kuanza zoezi la kuweka akiba ya pesa nacho ni wazo kuu la kesho, jiulize kesho unataka ufanye nini?  na ili ufanikiwe jambo hilo wahitaji kiasi gani cha fedha?  Ukifahamu kiasi cha fedha unachohitaji ili kufikia lengo hilo utatakiwa kujua kwa sasa wewe unapata kiasi gani cha fedha? iwe ni kwa mwezi au kwa kila siku muhimu uwe na uhakika na kiasi hicho cha fedha. 

Ukijua unaingia shilingi ngapi labda kwa mwezi sasa utatakiwa ujue pia matumizi yako kwa mwezi yakoje? Yanagharimu kiasi kipi cha fedha?  Na je matumizi yako kwa siku mpaka mwezi yanakuruhusu uweze kuyafikia malengo yako? Ukiwa na majibu ya maswali hayo ndipo utaangalia sasa kipi kinawezekana kupuguzwa ili matumizi yako kwa mwezi yapungue. 

Hatua ya pili ni kuorodhesha matumizi yako katika safu mbili , moja iwe ya matumizi ya lazima mfano chakula  n.k na ya pili iwe ni ya matumizi yasiyo ya lazima kisha  tafuta uwezekano wa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ili pesa ambayo ilikuwa inatumika kwenye matumizi hayo  iingie kwenye akiba na pia uanze kujinyima kimatumizi  ili upate pesa ya ziada .

Hatua ya tatu ni kujiwekea mikakati ya kujikumbusha malengo yako kwa mfano unaweza kuwa na utaratibu wa kila siku jioni unapitia daftari lako la malengo ili uwe na shauku ya kuendelea na mapambano bila kuchoka. Unatakiwa Kuheshimu mikakati yako kwa kuwa na nidhamu katika  kuweka akiba ili uweze kufikia malengo yako. 

Hatua ya mwisho ni kuhakikisha pale upatapo pesa  unatoa kwanza kiasi ambacho umeridhia kukiweka kabla ya matumizi mengine yoyote  usifanye makosa kwa kuanza kutumia pesa kwanza kisha ndio ubakize akiba , fanya zoezi hilo kwa nidhamu yote na lifanye kwa kuongozwa  na malengo ya kesho.

Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul Kalivubha 

+255652 134707