Thursday, 4 July 2024

UKIMILIKI PESA UMEMILIKI HISIA ZA KUJIAMINI NA UKIKOSA BASI UMEPOTEZA SEHEMU YA KUJIAMINI.

 UKIMILIKI PESA UMEMILIKI HISIA ZA KUJIAMINI NA UKIKOSA BASI UMEPOTEZA SEHEMU YA KUJIAMINI.

Linapokuja suala la umiliki wa pesa basi tunazungumzia hisia ziletwazo  na pesa ambavyo kwa namna yoyote unatakiwa hisia hizo zisikushinde bali uzitawale.Wengi hatutafuti pesa kama zilivyo karatasi bali tunatafuta ile hisia ambayo mtu anakuwa nayo akiwa na pesa ndio maana leo hii mtu akiwa na pesa kuna namna atajihisi hata akivaa hovyo hatahisi aibu kwa sababu anajua mtaona kaamua kufanya hivyo ila mtu akikosa pesa kitu cha haraka atachohisi ni aibu na hata kutamka mbele za watu kuwa hana pesa anaweza kushindwa kwa aibu .

Hisia kubwa ileteayo na pesa ni kujiamini na hapo ndipo inatakiwa mtu uwe na nguvu kubwa kuliko hisia itokanayo na pesa bila kujali una pesa ama huna.

Kwa sababu hisia ya kuwa na pesa ikikupa maamuzi ndio utaanza kufanya mambo ya kushangaza na sio kwamba ni mazuri bali ya hovyo kwani utakuwa mtumwa wa pesa.

Vipo viashiria vingi kuwa mtu fulani ni mtumwa pesa na hasa tunaangalia matumizi yake na matendo afanyayo muhusika kama vile:

Ulimbukeni kwenye starehe ambapo muhusika utamuona akitumia pesa bila kuinoea huruma pesa.

Kuanzisha vurugu zisizo na lazima ilimradi tu ujulikane kuwa chanzo ni wewe na tena kwa sababu tu una pesa.

Kuanzisha vitendo vya hovyo kama vile dhuluma kwa wanyonge kwa kutumia nguvu ya pesa ukiwa unasmini hata utatumia pesa kununua haki kama ikitokea unashitaakiwa.

Kibaya zaidi ukiongozwa ba hisia za pesa utakuwa na siku za kuhesabika kwenye umiliki wa pesa kwa sababu utakuwa mwenye matumizi mengi yasiyo na lazima na huo ndio utakuwa mwanzo wa kufilisika 

Je inakuwaje kwa mtu ambaye hana pesa? Kukosa pesa ni mwanzo wa kupoteza hisia za kujiamini na hapo utaingiwa na tatizo la kujishtukia kwa mambo ambayo hata hayapo kama vile:

Usiposalimiwa unahisi ni sababu huna pesa ndio maana hata baadhi ya watu hawakupi salaam zao lakini inawezekana tu hawakusalimii kwa sababu zao binafsi na sio sababu huna pesa.

Ukiambiwa ukweli unaona kama vile  unafokewa kwa sababu huna pesa lakini ukweli ni kuwa wanakuonya tu ili uwe kwenye uelekeo mzuri tu na sio sababu huna pesa.

Ukiachwa kwenye mahusiano kwa sababu hata  nyingine kabisa wewe tayari unajua ni vile tu huna  pesa ndio maana umeachwa.

Kanisani/misikitini au kwenye jamii usipopewa uongozi unajua tayari wamekuona huna pesa ndio maana hawakupi uongozi kumbe hata yawezekana wana sababu zao tofauti na unavyojifikiria na muda wote unahisi kuna watu wana  njama mbaya na wewe. 

Muda wote unajitetea kwa kutumia hali yako ya kukosa pesa na hapo ndipo unakuwa unajipotezea heshima yako.

Unaona watu wanakunyima makusudi pesa ili  kukukomoa ,huamini kama na wao hawana.

Dhibiti hisia za umiliki wa pesa au ukosefu wa pesa na ukiliweza hilo basi pesa itakuwa rafiki yako na hata kama huna basi nguvu ya kutafuta itakujia kwani huathiriwi na hisia zake za kutokuwa nayo.

Acha kuunganisha kila tukio na kukosa kwako pesa bali tambua kuwa matukio mengine yangetokea tu  hata kama ungekuwa na hizo pesa. 

Usiruhusu kila mtu ajue hali yako kiuchumi , Shirikisha baadhi ya watu kuhusu hali yako na uwe umejiaminisha kuwa kweli hao ni watu wa maana na busara

Usijitetee sana kwa kutumia hali yako ya ukosefu wa pesa pia usisahau kutafuta pesa ili usiwe mtu wa kujishtukia

Mwanasayansi Saul kalivubha

+255652 134707

Sunday, 23 June 2024

USIFANYE WATOTO WAKO WACHUKIE WAJOMBA NA BABA ZAO WADOGO KWA SABABU YA MATATIZO YAKO.

 USIFANYE WATOTO WAKO WACHUKIE WAJOMBA NA  BABA ZAO WADOGO  KWA SABABU YA MATATIZO YAKO.

Kuhudumia watoto wako ni jukumu lako kwa 100% na tena hutakiwi kulalamika kwenye hilo kwa sababu hawakukulazimisha uwazae  , ikitokea kuna mtu anakusaidia shukuru na isipotokea hayupo usilaumu maana hilo ni jukumu lako wewe kwa 100% na sio vinginevyo.

Usifanye watoto zako wawachukie wajomba na Baba zao wadogo bure kwa sababu ya matatizo yako kwa sababu wewe ndio unatakiwa uwe mstari wa mbele kuwapa malezi bora na mahitaji yote ya msingi hata ukikwama basi angalau uwe umetimiza kwa 90% na ikitokea unasaidiwa iwe kwa 10% tu na tena mshukuru huyo atakayejitoa kufanya hivyo kwa sababu kaingilia majukumu yako 

Ukishindwa kuwasomesha watoto zako basi  wakulaumiwa ni wewe sio uanze kutafuta nani wa kumtupia lawama na hapa wazazi wengi hukosea kwa kuaminisha watoto zako kuwa wameshindwa kusoma shule nzuri kwa sababu ya wajomba ama Baba wadogo hawakuwasaidia na wana maisha mazuri, swali ni je hilo ni jukumu lao? Hapana hilo ni jukumu lako wewe usikwepe kulaumiwa.

Wakikuta milo yako ni ya kubahatisha wa kulaumiwa ni wewe kwa 100% na sio walioshindwa kukusaidia kwa sababu mtoto hakukulazimisha umzae la sivyo kama ilitokea umebakwa au kubambikiziwa mtoto hapo kweli kuna haja ya kusaidiwa kwa sababu imekuwa dharura ila tofauti na hivyo watoto sio dharura hivyo hutakiwi kulaumu wengine bali kujilaumu kutofanya maandalizi na kama mzazi sio vizuri kuuza majukumu yako pengine bali wajibika mwenyewe.

Wakikuta una chumba kimoja mnabanana humo  wa kulaumiwa ni wewe na sio mjomba wao aliyeshindwa kukusaidia kujenga  nyumba kwa sababu ulijua kabisa watoto wakija watahitaji sehemu ya kulala  hivyo ni wajibu wako kuitafuta hiyo sehemu na sio kulalamika , Kama unajiona kabisa huwezi basi acha mchezo wa kubahatisha kwamba kila mtoto huja na baraka zake bali ruhusu waje watoto ambao unajua fika utawamudu bila kulalamika. 

Kama wangejua hauko tayari kuwahudumia basi wasingechagua kuzaliwa na wewe kama tu wangepewa hiyo nafasi ya kuchagua  na hii ni kutokana na wewe kuwasimanga kwa malezi yako , Sio vizuri mzazi kuona kama unateseka kuwahudumia yaani unalipa ada za shule kwa masimango, unawananulia mavazi kwa masimango na kuwaonyesha kama unawahudumia  ili kesho wakulipe.

Mwanasayansi Saul kalivubha 

+255652 134707

Friday, 22 March 2024

USIPOISHI NAO KWA AKILI NYINGI WATU HAWA UTAJIKUTA MATATIZONI MUDA MWINGI.

 USIPOISHI NAO KWA AKILI NYINGI WATU HAWA UTAJIKUTA MATATIZONI MUDA MWINGI.

1.Wanaojiona sahihi muda wote hawa hawachelewi kukubebesha makosa yasiyo kuhusu. 

2.Wajuaji kupitiliza hawa muda wote watakulaumu tu kwani kila jambo watakuona unakosea hata kama wao ndio wamekosea.

3.Wanaokutafuta kwenye shida tu hawa utawaona marafiki ukiwa na kitu cha kuwapa ila  siku ukiwa kwenye uhitaji watakuacha mtaroni.

4.Waropokaji hawa muda wowote watamwaga siri zako mbele ya wasiotakiwa kuzijua hivyo hakikisha hawajui mambo yako ambayo hayatakiwi kujulikana na wengi.

5 Wenye imani za kishirikina kupitiliza hawa hata kwenye jambo la kawaida wao watakushauri uende kwa mganga wa kienyeji kwa sababu wao hawaamini tena kwenye ukawaida

6.Wenye imani za dini kupitiliza, hawa pia kwenye sehemu unayotakiwa utumie akili zako wao watakushauri ufunge na kuomba ili upate majibu sasa ikiwa zaidi hii inakuwa kupoteza muda.

Pia watakushauri uvumilie hata sehemu unayotakiwa kuondoka. 

7 .Wenye wivu wa mapenzi kupitiliza, Hawa kwa muda mfupi watakufanya ufurahie mapenzi ila kwa undani zaidi watafanya ufeli mambo ya msingi kwa mfano unaweza kupata dili la maana la pesa ila watakukataza usiende kalifanya wakihofia kuibiwa kimapenzi. 

8 . Wenye mitizamo ya kimaskini, hawa muda wote wanaamini utajiri ni dhambi hivyo ukiwa nao na wakakumudu basi watakushauri uwe sawa nao.

9.Waliokata tamaa na kuridhika, hawa muda wote watakwambia maisha ndio haya haya.

10 Wenye utoto ilihali ni wakubwa, hawa watalia kwa kila changamoto yaani kwao hawana changamoto ya kuvumilia bali kulia na kukata tamaa, ukiwa nao na wakakumudu utafanana nao.

Mwanasayansi Saul kalivubha.

+255652 134707

Tuesday, 19 March 2024

KOSA LIKIKUFUNZA SIO KOSA TENA BALI NI UPYA ULIOKUWA HUUJUI

KOSA LIKIKUFUNZA SIO KOSA TENA BALI NI UPYA ULIOKUWA HUUJUI.

Sifa ya makosa ni kutoa adhabu na inaweza isiwe muda huo ulipolifanya kosa ila ni lazima litakuadhibu tu mbeleni hivyo hakuna namna unaweza kukwepa adhabu ya kosa lako.

Taarifa inayopendeza ni kuwa kosa likikupa adhabu nawe ukaona kama funzo basi hilo sio kosa tena bali ni upya ambao ulikuwa huujui hapo kabla na njia pekee ya wewe kuujua huo upya imekuwa ni kupitia kukosea.

Usifanye makosa makusudi hapo utakuwa sasa unatafuta adhabu za kujitakia na yawezekana adhabu hiyo isiwe funzo lolote kwako kwa sababu sio jipya bali ulilijua kabla. 

Kwenye mchezo wa mpira timu inafungwa kupitia makosa hiivyo adhabu yake ni kufungwa magoli ila baadaye wachezaji wakimakinika kutafuta walifungwa vipi basi watagundua mbinu zipi wafanye ili wasifungwe tena  na hapo itakuwa wamejifunza kupitia makosa na adhabu waliyo adhibiwa.

Japo makosa mengine adhabu yake ni kali na utaadhibiwa tu bila  kujali hukuwa ukijua kuwa ni kosa hapo kabla ila ukimakinika zaidi utajifunza tu .Kosa bila adhabu ni ngumu kuwa funzo na kikawaida kosa lisilo na adhabu yawezekana lisiwepo labda tu uamue kutuiona hiyo adhabu.

Ukiona maisha yanakuadhibu Kwenye jambo fulani wewe kaa chini tulia utafute wapi ulikosea.


Mwanasayansi Saul kalivubha 

+255652 134707

CHANGAMOTO NI BURUDANI KATIKA MAISHA, BURUDIKA NAZO BADALA YA KULIA LIA HOVYO.

 CHANGAMOTO NI BURUDANI  KATIKA MAISHA, BURUDIKA NAZO  BADALA YA KULIA LIA HOVYO.


Mwanafalsafa mmoja aliwahi kusema ukitaka ufurahie adhabu basi ukipewa usiione kwa sura ya adhabu bali ona kama ni sehemu kama wajibu wako, kwa mfano ukipewa adhabu ya kumwagilia maua wewe ona ni wajibu wako kufanya hiyo ili maua yakue na kustawi.


Changamoto ni burudani kama zilivyo burudani ni ngumu kuburudika bila kuvuja jasho, kwenye suala la burudani kuna upande utavuja jasho na kuna upande utaburudika ila inaitwa burudani na watu hufurahi kwa sababu wameamua kumakinika na upande wa furaha kuliko upande waliovuja jasho.

Maisha ya kukosa kazi kwa muda, kuachwa kwenye mahusiano na mengine mengi yenye sura ya changamoto ni sehemu tu moja wapo  ya burudani ambayo ndio ya kuvuja jasho na kama ukiendelea kukaza utafikia ule upande wa pili wa burudani ambao ni wa kufurahia.

Kwenye hii burudani ya maisha hakuna mtu asiyepitia upande wa kuvuja jasho ambao ndio changamoto na burudani haina maana kama itakuwa na upande mmoja tu wa furaha, ukiona watu kwenye viti virefu au kokote wapo wanajipongeza basi jua wana upande mwingine waliopitia ambao ndio uliwapa hizo pesa.

Ikitokea unafukuzwa ama kukataliwa usione kwa sura ya kukomolewa au kama vile umeadhibiwa bali ona hiyo ni sehemu tu ya burudani ambapo unaandaliwa kwenda kukubalika kwingine tena panaweza kuwa pazuri zaidi ya ulipofukuzwa. Tatizo ni pale ambapo utaiona hiyo changamoto kwa sura ya kukomeshwa hapo utajikuta kwenye maumivu, kulia na kulalamika hovyo kitu ambacho hakitakupa unafuu bali kukuumiza na mbaya zaidi kukufanya uje ukosee tena kwa sababu utafanya maamuzi bila utulivu. 

Maisha yana changamoto nyingi sana na nzito ila ukisema kila moja uione kwa sura yake basi kila siku utakuwa mtu wa kulia hovyo badala ya kujifunza kupitia changamoto hizo.


Mwanasayansi Saul kalivubha

0652 134707

Saturday, 9 March 2024

HARAKATI HAZIMTAKI MTU ANAYEONGOZWA KWA MIHEMKO

HARAKATI HAZITAKI MTU ANAYEONGOZWA KWA MIHEMKO.


1.Mtu ambaye akiambiwa biashara fulani inalipa anaikurupukia.

2.Ambaye akiambiwa alisemwa vibaya muda huo huo anawafuata wahusika.

3.Mtu ambaye akiambiwa kasalitiwa muda huo huo anawasha moto.

4.Mtu ambaye anataka kufanya kila kinachosifiwa sana.


KAMA UNA SIFA HIZO HAPO JUU BASI HUWEZI KUWA MWANAHARAKATI.


Kuwa mwanaharakati uwe na sifa hizi.

1.Usiyekurupuka hovyo.

2.Mchunguzi kabla ya kuongea.

3.Usiyekata tamaa kizembe.

4.Uliyetayari kukoselewa.

Michakato yote haikosi changamoto ni lazima changamoto zije kukupima kuona kweli utaweza kuyamudu mafanikio? 

Changamoto zinapokuja kuna mambo mawili ama hiyo safari sio yako au ni yako ila unatakiwa kukomaaa, sasa kabla hujasema hiyo safari sio yako ni lazima ukomae haswa maana ukiwa mtu wa kukwepa changamoto kwa sababu tu ya mihemko yako basi hakuna safari utakayoiweza hapa Duniani. 


Na ukiwa mtu wa kufanya mambo kwa kukurupukia kwa sababu tu ya mihemko yako basi utakuwa pia mtu wa kuanza upya kila mara kwani itakuwa ukifika njiani unagundua hiyo njia siyo yako bali uliikurupukia tu 


Mwanasayansi Saul kalivubha 

0652 134707

Thursday, 7 March 2024

UKIONA WANAKUNG'ANG'ANIA WAKUPE UTAJIRI WA HARAKA JUA WAMEKUONA AKILI YAKO NI CHENGA

 UkIONA WANAKUNG'ANG'ANIA WAKUPE UTAJIRI WA HARAKA JUA WAMEKUONA AKILI YAKO NI CHENGA 😔 

Umewahi kusikia watu wakijinadi kutoa utajiri wa HARAKA? Yaani kulala maskini na kuamka tajiri? 

Taarifa isiyopendeza ni kuwa kama nawe ni mmoja wa wateja wao basi jua kuna kitu kwako hakipo sawa na tayari wamekiona ndio maana wanakulazimisha uingie kwenye hiyo fursa hiyo.

Wale watu wana akili sana na wapo vizuri kuisoma akili yako hasa kwenye maamuzi yako na utulivu wako na wakiona una maamuzi ya haraka yasiyo na subira basi wanajua wewe ni mteja wao mzuri katika fursa hiyo.

Tangazo lenye lengo la kutoa utajiri wa haraka huwa linawahusu watu wenye sifa hizi:

1.Wasio na utulivu, kama huna utulivu basi utakuwa mteja wao kwa sababu ukikosa utulivu utakuwa mtu wa kufanya mambo bila kufikiria kwa kina, kwa lugha rahisi unakuwa mvivu wa kupima matokeo na matendo ndio maana akija mtu akikwambia jambo fulani ukilifanya leo tu basi kesho utakuwa bilionea unaliendea kwa haraka sana bila kufikiria kuwa kama hilo jambo lingekuwepo si tungekuwa wote mabilionea.

2 Kupenda matokeo ya haraka, kama unapenda matokeo ya haraka basi nawe ni mteja kwa sababu ukiambiwa utajiri utakuja kesho haraka utaamini ila ukiambiwa utakuja baada ya miaka kumi utaona ni utapeli. Kwa lugha nyepesi hawa ni watu ambao hawana subira bali wanataka kila kianzacho leo basi kesho kilete matokeo chanya. 

3.Waliokata tamaa, mkata tamaa ni mtu ambaye haamini tena kwenye kushinda hivyo amebaki kusubiria miujiza tu , kama umekata tamaa kiwango cha mwisho basi nawe utakuwa mteja.

4.Wanaokimbizana na umri, kuna watu ambao kwa namna moja ama nyingine wanajiona kama wameachwa na umri hivyo hawataki tena kitu cha kusubiri bali wanataka tu jambo lianze leo na kesho lije na matokeo, kama upo kundi hili basi nawe ni mteja.

Matangazo haya ya kujinadi kuwa kuna utajiri wa haraka yanzidi kushia kasi kwa sababu watoaji matangazo wamegundua kuwa watu wengi sasa hivi wanataka sana mambo ya miujiza na hawataki tena kusubiria hivyo wapo tayari kulipa gharama ya kupewa utajiri wa haraka usio na uhalisia kuliko kutumia pesa hiyo kutafuta utajiri wenye uhalisia.


Mwanasayansi Saul kalivubha

+255652134707