MBINU ZA KUISHI NA WATU WENYE TABIA NGUMU MAKAZINI.
Kama sio wewe basi utakuwa umewahi kutana na mtu akilalamika dhidi ya watu ambao wana tabia zisizo rafiki na pengine mpaka mtu huyo anatamani kuachana na kazi hiyo ili aepuke kukutana na watu hao , ni kweli wapo watu wana tabia ambazo ni ngumu kuvumilikika kiasi kiasi cha kufanya wengine wakose amani pindi wakiwa na watu watu hao wenye tabia zisizo rafiki.
Pengine hata wewe kuna mtu ana tabia ambazo zimekufanya ujiulize swali hili " hivi huyu mtu anaishije na familia yake kwa tabia hizi?" Maana kama yuko hivyo kazini inakuwaje nyumbani kwa ndugu zake ambao wengine analala nao kitanda kimoja na kula nao meza moja si pengine ikawa kila siku makwazo kwenye nyumba hiyo ? Lakini ukweli ni kuwa hakuna makwazo kabisa anaishi na familia yake vizuri tu kwa sababu walipomfahamu walijifunza kuishi naye kwa kumzoea alivyo changamoto ipo kwako ambaye hujazaliwa naye bado hujajifunza kuishi naye na pengine hutaki kujifunza kuishi naye.
Hakuna namna utaishi bila kukutana na watu wenye tabia zote nzuri na mbaya ili uepuke hilo basi kajifungie kisiwani peke yako lakini tofauti na hivyo lazima utakutana na watu wenye tabia zote nzuri na mbaya sasa itategemea na watu hao umekutana nao wapi na wana nafasi gani kwako kama ni kazini na ofisi moja je utaacha kazi kwa sababu ya watu hao? Au utakuwa unakaa nje ya ofisi kuwakwepa watu hao ? Haiwezekani hilo na sio suluhisho lake lazima ujifunze kuishi nao watu hao.
Jitahidi ujue mnapishana sana kwenye kipi kwa sababu sio kweli kwamba mtapishana kwenye kila kitu lazima tu kuna sehemu moja ndio huwa chanzo cha kupishana naye na ukilitambua eneo hilo basi tenga siku moja tafuta eneo tulivu jitafakari ni kwa nini mtapishana? na kwa nini eneo hilo? Anza kutengeneza mbinu za kuishi naye mtu huyo kwenye eneo hilo na moja wapo ya mbinu nzuri ni kutojibana naye sana kwenye eneo hilo jifunze kupuuzia baadhi ya kauli zake , pengine uone ugumu kukaa kimya pindi anapoongea kama tabia yake ilivyo lakini baadaye utazoea tu na itakuwa akiongea mambo yake unajibu machache mengine unamsikiliza.
Mbinu nyingine ni kumpuuza kwenye baadhi ya mambo yake lakini usimuonyeshe kuwa unampuuza bali usifanyie kazi kila tukio lake kwako kwa mfano mmekutana kazini umemsalimia hajaitika au yeye hakusalimii hilo lisikupe msongo wa mawazo kwa kujiuliza kwa nini haitikii salamu zako bali mpuuzie tu kwa sababu ndivyo alivyo na usiache kutabasamu pindi ukikutana naye na wala usilipe kisasi kwa anayokufanyia na hapo itakuwa mwanzo wa wewe kuishi naye mtu huyo.
Mbinu nyingine ya tatu ni kujitahidi unaepuka mazingira ya kukaa na mtu huyo muda mrefu ila isipokuwa pale tu inapobidi kwa sababu za kikazi tofauti na hivyo muepuke mtu huyo kwa kujishugulisha na mambo yako mengine.
Mbinu nyingine ni usiitizame tabia yake kama kikwazo kwako bali muone kama ndivyo aliumbwa hivyo na ukiliweza hili basi usiwe unamuongelea jinsi alivyo mbele ya wengine bali muombee kubadilika kwa sababu tabia yake sio kwamba unaiyona wewe tu bali kuna wengine pia wanaiyona hivyo tabia yake inakuwa kikwazo kwake sio kikwazo kwako wewe kazi yako ni moja tu kujifunza kuishi naye
Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul Kalivubha
+255652134707
No comments:
Post a Comment