SEHEMU YA KWANZA “NAPOKEA FRIEND REQUEST”
Ilikuwa Jumapili nikiwa nimetoka ibadani nimetulia tu
kitandani kusaka utulivu wa nafsi, masaa sikuwa nayakumbuka vizuri ila nachokumbuka
tu ni kwamba nilikuwa kitandani nimejilaza ili nipumzike, katika kupumzika akili
ikaniambia, "Peruza kidogo mitandaoni upate starehe."
Nikaanza na na Facebook, Bila kufikiria sana nikaona
ombi la urafiki mpya Jina lilikuwa Koku Muganizi. Sikufanya upekuzi wowote kwa
sababu ilikuwa si jambo jipya kukubali maombi kama yale hivyo haraka tu nikaibonyeza
"kubali" na kuendelea na maisha yangu.
Baada ya dakika chache alama ya meseji ikaonekana,
nilipoingia nilikuta jumbe 3 kutoka kwa huyo rafiki mpya:
"Mambo"
"Asante kunikubalia urafiki"
"Nimefurahi kuwa sehemu yako"
Kama mwanaume, ukipata ujumbe kutoka kwa jinsia ya
kike moyo unakuwa mwepesi hivyo bila ajizi niliingia haraka kwenye profile yake
nikakuta picha tatu tu za binti mtulivu, mstaarabu na mzuri.
Tukaanza kuzungumza kidogo kidogo lakini kitu kimoja
kilinisumbua kichwani nacho ni jina lake halikunipa uhakika kwamba ni msichana
kweli maana zama za leo utapeli ni mwingi sana hivyo nikaamua kumpima kwa utani
ili kuthibitisha
Mimi: "Yaonekana wewe ni msichana mtulivu
sana"
Yeye: "Kawaida tu hata wewe pia ni kijana
mtulivu."
Jibu lake lilikuwa la haraka sana likafanya nikose la
kusema zaidi.
Niliamka kwenda chooni, niliporudi nilishangaa kupata
meseji yake kwenye WhatsApp na ilikuwa ni yeye yule yule wa Facebook, Moyoni
nilisema, "Labda kachukua namba yangu mahali."Lakini kilichonifanya
nisimame ni kitu kingine. Alikuwa ananiita kwa majina yangu yote matatu ya
kuzaliwa. Tatizo ni kwamba Facebook
yangu ina majina mawili tu hilo la tatu nililificha, Sasa alilijulia wapi?
Sikumuuliza bali niliijaribu kujipa majibu yangu
mwenyewe. "Labda Facebook inaongeza kiotomatiki."
Tulizidi kuwasliana mpaka kupeana historia zetu na
hapo ndipo tukagundua kuwa tunatoka mkoa mmoja ingawa wilaya zetu ni tofauti
yeye alikuwa Bukoba na mimi Muleba, Unajua furaha ya kukutana na mtu wa
nyumbani nje ya nyumbani? Inaleta utamu tofauti kabisa.
Siku chache tu, tulikuwa tayari tumeshaingia kwenye mahusiano
na wote tulikuwa w mbali na nyumbani, yeye kikazi na mimi pia lakini
alinihakikishia kitu kimoja kuwa atakapokuwa na nafasi nitapita kukusalimia
maana wote tulikuwa Dar es salaam. Maneno hayo kwa mwanaume ni kama mafuta
kwenye moto hakuana asiyependa kutembelewa na msichana.
Siku moja akaniuliza:
"Unajua tarehe 12 Mwezi wa Sita ni siku yangu ya
kumbukizi kuzaliwa?"
Nilijibu kwa furaha: "Nitakutumia kitu hata kama
ni zawadi ndogo na kama tutaonana tutasheherekea pamoja"
Akanijibu: "HAPANA SHAKA. KUNA SIKU ITATUKUTA
PAMOJA." Japo tulikuwa pamoja Dar ila sikutaka kuonekana ninaharakisha
sana kuoanana naye, Japo ndani yangu kulikuwa na swali moja linaninyima
usingizi: Alipata wapi namba yangu? Na alijua vipi jina langu la tatu?
Nikaamua kufanya upelelezi wangu mdogo, nikaangalia
kama tunachangia marafiki na kweli, nilimkuta ana rafiki mmoja tuliyesomea naye
hapo moyo ukatulia kidogo. Lakini kabla sijapumua, akanitumia ujumbe:
"Mbona unaonekana
una hofu?"
Nikajibu: "Sina hofu."
Akarudi tena: "Nafahamu una hofu ya wapi nimepata
mawasiliano yako ni rafiki zako. Ndio wamenipa namba yako na majina yako
yote."
Damu yangu iliganda, kafahamu vipi kuwa nilikuwa na
hofu? Nikaamua kuwapigia wale marafiki zangu na wote walinipa jibu moja: "Tunamjua tu Facebook ila hatujawahi
kuzungumza naye" Nikiwa bado kwenye mshtuko huo, ndipo ujumbe wake mpya
ukaingia: "Wale rafiki niliokwambia
sio hawa wa Facebook."
Hapo ndipo hofu yangu ilipanda kilele, Huyu mtu ni
nani? Nilijaribu kujituliza. "Labda ni mtu tu aliyenifahamu barabarani
akampa taarifa zangu."
Tarehe 12 Juni ilifika ambayo ni siku ya kumbukumbu
yake ya kuzaliwa na asubuhi nilimtumia ujumbe wa kumpongeza na kumuahidi
kumtumia pesa anunue hata soda., Alifurahi. Baadaye mchana Facebook
ilinijulisha: "Leo ni siku ya kuzaliwa kwa Koku Muganizi." Niliingia kwenye ukurasa wake na picha yake
ilikuwa nzuri sana hata kwenye sehemu ya maoni watu wengi walikuwa wakimiminika
kumtakia heri ya kuzaliwa japo sikufanikiwa kusoma ila niliamini hivyo.
Nilijaribu kusoma sasa maoni lakini hayakufunguka, Nikajaribu kuandika yangu ya
kumtakia heri nayo yakakataa nikasema, "Labda ni mtandao."
Akanitumia ujumbe: "Leo Facebook yangu haiko
sawa."
Nami nikakubaliana naye lakini akaniambia,
"Jaribu tena."
Niliporudi, mwisho maoni yalifunguka nikapiga hatua
kuteremka ili nione ni nani kamtakia heri. niliwaza, kama ana mchumba lazima
nimpate hapa kisha nikakutana na maoni ambayo yalibadilisha kila kitu kwenye
fikra zangu kwanza maoni mengi yalikuwa kwa lugha nisiyoelewa. labda ni lugha
ya kwao, nikajidanganya pili nikaona lipo moja kwa Kiswahili hapo Roho yangu
ikatetemeka.
Lilisomeka hivi:
"Vipi mbona msimu huu umetucheleweshea
Damu?"
Naye akajibu:
"Punde tu mtapata. Si mnajua ugumu ulivyo sasa
kuipata?"
Damu?
Malenga wa Kiha
Mwanasayansi Saul Kalivubha
255652134707
Nzuri mwanasayansi.
ReplyDeleteTunasubiri mwendelezo