Saturday, 10 February 2024

KAMA HIVI NDIVYO UNAVYOISHI MJINI NI BORA URUDI TU KIJIJINI UKAISHI KULINGANA NA KIPATO CHAKO

 KAMA HIVI NDIVYO UNAVYOISHI MJINI NI BORA URUDI TU KIJIJINI UKAISHI KULINGANA NA KIPATO CHAKO.

Yawezekana hii isiwe makala nzuri kwa waishiyo mijini huku wakijisifu kila siku na kuwabeza waishiyo vijijini ila ukimakinika na kuchukulia chanya basi kuna jambo utajifunza. Kuishi mjini ni ndoto ya wengi nafikiri inaweza kuwa zaidi ya asilimia hamsini ya watu wanatamani kuishi mjini na hasa kwenye miji ile mikubwa  lakini uhalisia ukoje huko mjini kwa wengi wao? Kuwa kwenye changamoto  mjini sio sababu pekee ya kusema uhame urudi kijijini/mkoani la hasha ! Hapa namaanisha kwa wale ambo mjini hawapawezi kabisa ila wanapang'ang'ania  tu kwa sababu zisizo na msingi.

Bila shaka utakuwa umewahi sikia ama kuona baadhi ya watu waishio mijini wakiwabeza watu waishio vijijini ama mikoani kama wasemavyo watu  wa Dar es salaam na kibaya zaidi hudiliki kusema watu wa vijijini ni washamba na wasio wabunifu wa maisha, Sio uongo kuwa kuishi mjini kunakomaza akili kulinganisha na kuishi kijijini kutokana na harakati kuwa nyingi mjini na panahitaji wepesi sana katika maamuzi ili uweze kumudu mjini lakini kwenye maamuzi hayo hayo kuna watu wapo mijini kuongeza idadi tu ya watu ila ki uhalisia wanaishi maisha magumu sana kwa lugha isiyo rasmi ni kuwa walikurupuka kuja mjini ilihali hawana mipango ya kuwafanya wanufaike na maisha ya mjini. 

Ikiwa unaishi mjini kwa sababu moja wapo kama  nimevyoelezea hapa chini  basi haraka toka mjini urudi mkoani/kijijini  ama jitafakari zaidi ubadili mtindo wako wa maisha.

Kuishi mjini ki ulimbukeni; Unaishi mjini kutaka tu uonekane nawe unaishi mjini yaani ukisimama na kujitambulisha ama kutambuliswa unaishi mjini hiyo ndiyo furaha yako kuu bila kujali hali ngumu unayokutana nayo huko mjini na kama hii ndio sababu pekee ya wewe kuishi mjini basi haraka ondoka mjini kwa sababu unaongeza tu idadi ya watu na usipokuwa makini maisha yatakuchapa  na kujikuta kwenye hali mbaya kimaisha mpaka kwa uzao wako pia, kwa sababu utatumia gharama kubwa kuwafanya watu wajue kuwa unaishi mjini ilihali hiyo gharama ungeitumia kuboresha maisha yako huko mjini, kila siku utakuwa mtu wa kuchapisha maudhui mitandaoni ya kukuonyesha upo mjini ambapo vocha zitateketea tu bure na hakuna unachokiingiza tofauti na sifa ambazo hazikuingizii pesa. 

Kuishi mjini kwa sababu umepazoea; Kuna mtu maisha ya mjini kwake ni magumu sana na kikawaida tayari yamemshinda ila  ukimpa fursa za kurudi mikoani/kijijini anaweza hata kukutukana na ukitaka kujua sababu anakwambia kapozea mjini hivyo itampa sana tabu kuanza tena upya huko mikoani  kama wewe ndio huyu jua kabisa mjini hapakufai ondoka haraka la sivyo jiandaye kuzeeka maskini.

Kuendelea kuishi mjini kwa maisha magumu ukiogopa kuchekwa endapo utarudi mkoani/kijijini; Huyu pia hafai kuishi mjini kwa sababu hatofautiani sana na mtu limbukeni na asiye na malengo,Huyu yupo tayari kufanya maamuzi ila anaogopa macho ya watu ilihali mjini pememshinda  kuishi sasa nawe jiandaye kuishi maisha magumu sana kwa sababu huna mbinu za kutatua changamoto ili umudu maisha ya mjini bali upo tu kuonekana mtoto wa mjini ilihali maisha yamekushinda .

Kuishi mjini huku unategemea mshahara tu kama chanzo pekee cha pesa na huna chachu yoyote ya kuongeza vyanzo vingine vya pesa; Hili kundi lina watu wengi sana na hapa ndipo utakuta mtu anaishi mjini kimateso sana na hana mpango wowote wa kujinasua na mateso hayo , Kwa mfano unategemea mshahara tu ndio ulipe kodi ya nyumba,ukupe  nauli zako za  kila siku kukupeleka kazini, ukupe ada ya watoto tena shule za mjini hawana huruma kama huna ada mtoto watamfukuza tu sasa hapo kweli utaishi maisha ya furaha? Sio kwamba kila siku utakuwa mtu wa kulalamika tu kwanini mishahara haipandi . Kama wewe ndio huyu ondoka haraka mjini urudi mkoani kwenye nyumba nzima unapanga elfu hamsini na bado zipo jirani na unapofanyia kazi hivyo  huna haja ya kulipa nauli , haya kwako yatakuwa maamuzi sahihi kwa sababu huko mjini pia umekaa tu hutaki biashara hivyo ni bora urudi kuishi kwa kutegemea mshahara sehemu yenye maisha rahisi. 

Kama unaishi mjini huku ukisifia tu maisha mazuri ya mjini na jinsi watu walivyo na majumba makubwa na magari ila wewe huna hiyo nyumba na wala gari pia ; kama wewe pia ni huyu basi  mjini hapakufai tena ondoka haraka kwa sababu upo kwenye kundi lisilo lako na mwisho wa siku shida utapata wewe, upo mjini kushangaa tu wengine wakifanya maendeleo ila wewe unaendelea kuwa mteja wao kwa  kuwaongezea kipato tu sasa unafanya nini mjini? 


Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul kalivubha 

+255652 134707 

Saturday, 3 February 2024

MAMBO UNAYOTAKIWA UFANYE UKIWA NA UMRI KATI YA MIAKA 20 MPAKA 30

 KIJANA JITAHIDI USIJIPOTEZE UKIWA NA UMRI KATI YA MIAKA 20-30

Katika makuzi kuna mgawanyo wa hatua takribani nne ambapo karibu kila mtu kwa kudra za mwenyezi Mungu huzipitia, Vipindi hivyo hugawanywa kwa kuzingatia umri na matukio yake na pia kila kipindi ni muhimu zaidi katika kuandaa kipindi kingine hivyo kumbe hutegemeana.Japo hatua hizo za makuzi hutegemeana ila ipo hatua yenye changamoto nyingi na iliyomuhimu sana na mtu usipokuwa makini utajikuta unajipoteza na ukiwa makini zaidi utajipata .

UMRI KATI YA MWAKA 1 MPAKA MIAKA 18 , Huu ni umri wa kujidanganya sana na kutengeneza malengo ya ukubwani  na kwanini kujidanganya? Kwa sababu unakuwa unaona kila kitu kitawezekana bila kusubiriwa kwa mfano: Utaona utamaliza shule mpaka chuo na baada ya kumaliza tu utapata kazi ya kuajiriwa na pengine ukipata kazi tu utalipa fadhila kwa waliokusomesha /kukusaidia na kisha utaoa/kuolewa na ndani ya mwaka huo huo utapata mtoto wako wa kwanza. Hivi ndivyo wengi tulipanga tukiwa na umri huo na walio kwenye umri huo pia wapo wanapanga wakiamini maisha ni mstari mnyoofu hivyo kila kitu kitaenda bila shaka yoyote, Je ni vibaya kupanga? Sio vibaya ndio maana awali nikatangulia kusema kuwa huu ndio umri wa kujiona ukiwa mkubwa utakuaje, Kwanini ni umri wa kujidanganya? Tuone hatua ya pili kisha hili jibu litapatikana.

UMRI KATI YA MIAKA 20- 30 ( UMRI WA UHALISIA) Huu ndio umri wa kuona vitu kwa vitendo kwa namna kijana alivyojichora akiwa na miaka 18 kurudi nyuma,Kwenye umri huu ndio utaona maisha ni mstari mnyoofu ama ni mstari wenye kona nyingi? Katika umri huu kwa wale ambao walienda shule wengi humaliza elimu zao mpaka za vyuoni na kikawaida ndipo wanakaribishwa rasmi mtaani na hapa ndipo uhalisia unaonekana.

Katika umri huu mambo mengi yanakuja kinyume na namna mtu alivyofikiri japo yanatimia ila kuna kitu kinaitwa Subira ndio hasa kinafaa kitumike kwenye umri huo kwa sababu ukiwa mtu wa pupa lazima utakata tamaa na kuona maisha ni magumu sana.

Sio ajabu kumaliza shule ukajikuta unapata kazi baada ya miaka mitano tofauti na ulivyojiona kuwa utamaliza leo na kesho utaitwa kazini.

Sio ajabu ukaoa/ kuolewa nje umri uliojipangia kwa mfano ulijua utamaliza tu chuo utaingia kwenye familia ila unamaliza unakaa tena miaka mitano mbele ndio unaanza familia. 

Sio ajabu ukaingia kwenye familia mapema tu ila ukakutana na  changamoto za uzazi ukajikuta unapata mtoto wa kwanza baada ya miaka 7 ya ndoa tofauti na ulivyoona ukiingia tu leo kwenye ndoa basi kesho tayari mimba na hata usijaliwe kupata maana yote ni mipango ya Mungu.

Sio ajabu ukavuka miaka 20 bila kuwa na kiwanja wala nyumba ukiwa bado umepanga au hata kuishi kwa wazazi  tofauti na ulivyojiona kumiliki nyumba na usafiri ukiwa kati ya  miaka 20 tu.

Hayo ni baadhi ya matukio ambayo yapo na wengi huyapitia na ndio inakuja ile sababu ya huu umri kuitwa umri wa UHALISIA, na huu umri unatufundisha kuwa maisha sio mstari mnyoofu na kutokuwa mstari mnyoofu haimaanishi kuwa malengo hayawezekani la hasha bali subira inatakiwa sana katika umri huo la sivyo utajipoteza kwa kuwa mtu mwenye haraka na mwisho wa siku unaishi maisha yasiyo ya uhalisia wako kwa mfano ulihisi utapata nyumba na gari haraka sasa ili kutaka yawezekana unaingia kwenye wizi au kwa waganga wa kienyeji wanakwambia utoe kafala mwisho wa siku unaishia gerezani .

Umri huu hutakiwi kuwa na haraka bali kuwa na juhudi tu za kupambania ndoto zako na sio lazima zije kwenye mstari mnyoofu ila ikitokea zinakuja kwenye unyoofu basi shukuru Mungu kwa hilo maana upo kwenye kundi la wachache ambao mambo yao yanakuwa kwenye unyoofu pasi na chenga.Usikubali ujipoteze hapa kwa sababu ukijipoteza kuna uwezekano mkubwa nyakati zitazofuata zisikusaidie kujipata tena.

UMRI KATI YA MIAKA 40- 55, Huu ni umri wenye matukio mawili makubwa la kwanza ni kukubali matokeo  huku ukilazimisha uendelee kuonekana kijana wa miaka 30 ,hii ni wale ambao walikata tamaa na kuona maisha ndio haya haya hivyo wanaamua kuridhika lakini changamoto nyingine inayowakabiri ni kupingana na umri yaani hawataki kukubali kuwa wao ni watu wazima na utajigundua hivyo pale ukianza kuona  unalazimisha kufanya vitu visivyo endana na umri wako, kitaalamu hiki kipindi kinaitwa mid age crisis(kuupinga utu uzima)

Tukio la pili ni wale ambao hawakukata tamaa hivyo wanaendelea kujitafuta na uwezekano wa kujipata upo  .

Changamoto kubwa kwenye umri huu ni kuwa majukumu yanakuwa mengi sana hivyo utegemezi unakuwa mkubwa hivyo kama hukujipanga vizuri utakuwa unapata pesa ila zinaishia kwa wategemezi wako.

UMRI KUANZIA MIAKA 60 KUENDELEA, Hapa ni uzee tu na kupumzika ijapo bado kuna wengine wataendelea na kutafuta tu kama matokeo ya kushindwa kutumia ujana wao vyema au kushindwa kuweka mikakati mizuri ujanani. 

Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul kalivubha 

+255652 134707

Friday, 2 February 2024

JIFUNZE KUTOFAUTISHA WATU HAWA WAWILI WANAOKUJA KWAKO KIMAHUSIANO

 JIFUNZE KUTOFAUTISHA   WATU HAWA WAWILI WANAOKUJA KWAKO KIMAHUSIANO.

Karibu tena ndugu msomaji kwenye blogu hii ya fikia ndoto zako kwa minajiri ya kuongeza maarifa, leo tutazame kidogo kuhusu aina hizi mbili za watu wanaokuja kwako kwenye mahusiano. 

Mahusiano sio kitu kigeni na hasa mahusiano ya kimapenzi yamekuwa yakiimbwa kwa ubaya na uzuri kila uitwao leo, kwenye hii Dunia kila mtu ni lazima ahusiane kama hutofanya hivyo kwenye mahusiano ya kimapenzi basi utafanya hivyo kwenye mahusiano ya kijamii hivyo hakuna namna unaweza kukwepa kuhusiana.

Kwenye mahusiano kuna kufaana na kushindwana ndio maana kila siku tunashuhudia matukio makubwa mawili ambayo ni watu kuendelea kuhusiana na huku wengine wakiafiana kuachana, Kwenye kuendelea kuhusiana haimaanishi kuwa wameendana kwa sababu kuna wengine wafanya hivyo kwa sababu tu wanajiona wamekosa pakwenda na kwenye kuachana yawezekana mnaendana ila mmoja tu kushindwa kuwa na subira ama kushindwa kujifunza kuishi na mwenziwe. 

Kuna makundi makubwa mawili ya watu ambao wanakuja/watakuja kwako kimahusiano hivyo ukiyafahamu hutopata shida ya kukabiliana na matokeo ya kila kundi.

Kundi la kwanza ni yule MTU ANAYEKUJA KUKUANGALIA KWELI WEWE NDIYE?

Huyo ni yule ambaye hajui nani anamtafuta hivyo atakuja kwako kama kubahatisha tu ukiwa ndiye atakaa na ukiwa siye ataondoka, hili ni kundi lenye watu wengi sana na kwa ufupi mimi huwa naliita kundi ambalo linajifuta kwenye mahusiano yaani bado wanachama wake hawajui kipi wanataka hivyo wanapoingia kwenye mahusiano wanakuwa mguu mmoja nje na mwingine ndani, utalitambuaje kundi hili? Huwa wana sifa zao zinazo fanana  kwa kiwango kikubwa.

TABIA YA WANAKIKUNDI HIKI NI KAMA ZIFUATAZO:

1.Wanakuwa kama waamuzi wa mpira tu muda mwingi wanatafuta makosa yako.

2.Hawana subira hivyo changamoto inayohitaji utatuzi wa pamoja wao ndio wanaichukulia kama mlango wa kutokea.

3.Hawasamii lengo moja ipasavyo hasa la kwanini wanahusiana yaani ukimuuliza kuhusu kesho yenu kwenye suala la pamoja anakuwa na maelezo mengi yanayokingana yenyewe, wapo hivi kwa sababu wanakuwa hawana uhakika kweli wewe ndiye?

4.Huwa hawatulii na mtu mmoja kwa sababu hawajui nani wanamtafuta hivyo hujikuta kwenye mahusiano na watu wengi 

5.Muda mwingi wanakuwa kama wapelelezi.

6.Kuachana kwao sio jambo dogo na muda mwingi watatishia hivyo hasa changamoto inapojitokeza.

7.Hawapendi kutafuta suluhisho bali wanakuwa kishari zaidi pindi amani inapotakiwa.

8.Wanakuwa na haraka sana na utalijua hilo kwa kuona wanataka mambo yawezekane bila kughairishwa kwa mfano mmepanga kukutana na bahati mbaya ukakutwa na changamoto na ukatoa taarifa ila kwake anaweza kutumia changamoto hiyo kama fimbo ya kukuadhibu na mkaachana.


Kundi la pili katika eneo hili ni MTU AMBAYE ANAKUJA KWAKO KUKAA.

Huyo anajua nani anamtafuta hivyo haji kwako kwa kubahatisha bali kajiridhisha kabla hajaja kwa lugha nyepesi hawa ni wale ambao hawapo kwenye majaribio labda wakukute wewe ndio upo kwenye majaribio uwakimbize ila ukiwa nawe upo tayari basi watajenga kibanda kwako na maisha yataendelea.

Hili ni kundi lenye wanachama wachache kwa sababu ili uwe mwanachama sifa ya kwanza lazima ujitambue vilivyo na ujue nani unamtaka.  Hili kundi ndio linafanya watu wasifie mahusiano na kuyaimba kwa uzuri wake , wanachama wake wana tabia zinazofanana na sio tabia nyingi hata.

SIFA ZA WANACHAMA WA KUNDI HILI.

1.Hawana mambo mengi hivyo wakija kwako hawaji kama waamuzi wa mpira bali wanakuja kujifunza kuishi na wewe na kufundishana pale mnapopishana.

2.Ni kundi ambalo halifichi lengo lao kuu na kupitia matendo utawaona hivyo pia.

3.Ni watafuta suluhu kwenye changamoto sio wepesi wa kutishia muachane.

Hizo ndio sifa za kila kundi na mpaka kufikia hapo natumai umejitambua upo kundi gani ama una uhusiana na mtu wa kundi gani , ikiwa upo kwenye kundi la kwanza ni bora uachane na mahusiano kwanza na uwekeze nguvu kubwa kwenye kujitafuta ili ujue nani hasa unamtafuta.

Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul kalivubha 

#fikia ndoto zako

+255652 134707

Friday, 26 January 2024

WANAVYUO TUSIISHI KAMA HATUTAHITIMU

 WANAVYUO TUSIISHI KAMA HATUTAHITIMU. 

Habari ndugu msomaji wa gazeti letu pendwa na karibu tena katika safu hii , leo tuangazie wasomi wa vyuo na hasa vyuo vikuu na hatima za maisha yao mtaani( baada ya kuhitimu)

Zama zimebadilika sana kiasi kwamba muhitimu wa chuo wa sasa ni kawaida kukaa nyumbani zaidi ya mwaka akisubiria ajira ambapo kipindi cha miaka kadhaa ya nyuma muhitimu alimaliza na kupitiliza kwenye ajira , ajira ilikuwa ni uhakika tofauti na sasa ajira imebaki ni bahati.Mabadiliko hayo ni ya kawaida sana sio Tanzania tu hata nchi za wenzetu huko ulaya dimbwi la wanachuo kukosa ajira linaongezeka kila siku tukiachana na tekinolojia kuchukua nafasi za ajira zetu mfano mgunduzi wa robot unachukua nafasi ya mtu kutenda kazi lakini pia idadi ya wasomi inazidi kuongezeka sana tofauti na zama zile unakuta mtaa mzima mwana chuo ni mmoja mtaani sasa mtaa mzima kuna zaidi ya wanavyuo ishirini na zaidi. 

Nimekuwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha afya na sayansi shirikishi muhimbili kwa miaka yangu kuishi pale kama mwanafunzi kuna jambo muhimu nilijifunza pengine kwa uliyehitimu tayari linaweza lisikusaidie tena lakini kwa aliye mwanafunzi sasa likamsaidia kwa kusoma makala hii au wewe kuwa balozi wa kufikisha ujumbe kwa anaye husika na umfundishe. 

Kumaliza chuo sio tukio la dharura ni wazi kuwa unaenda chuo leo na baada ya miaka kadhaa utarudi tena mtaani kuendelea na maisha mengine kwa kuitumia elimu yako kukupa pesa ili maisha ya kawaida yaendelee sasa utaishije?.

Ishi kama utahitimu chuo, vyuoni kuna makundi yanayonufaika na mikopo ya serikali yaweza kuwa mkopo ukawa wa 100% au pungufu ya asilimia hizo lakini bado ni mkopo hivyo lazima utaulipa tu sasa unautumiaje mkopo huo kumudu maisha yako ya chuo na kubaki na ziada kwa ajili ya kuendeshea maisha baada ya chuo?. Kuishi maisha chini ya kipato chako hii ni mbinu bora zaidi katika kuijali kesho yako , sio wanavyuo wote lakini wapo wanavyuo maisha yao ni kama tayari wamehitimu na wana kazi zao au wanaishi kama ule mkopo ni bure na wana uhakika kuwa siku wanamaliza tu na ajira watapata hivyo kuanzia utaratibu wa chakula chao, mapambo ya vyumba vyao na uvaaji wao ni gharama kubwa sana kulinganisha na mkopo wanaopewa na muda mwingine hujikuta wakiwa kwenye madeni ya kutosha tu kabla ya kupokea bumu jingine kwa mfumo huo si hata nauli ya kukurudisha kijijini baada ya kuhitimu utaikosa? 

Baada ya kuhitimu kuna maisha kabla ya kupata ajira na maisha hayo tukiachana na kula na kuvaa pamoja na sehemu ya kulala pia kuna kupeleka barua za maombi katika ofisi husika au kuzituma kwa njia ya barua pepe bila kusahau gharama za kwenda pale ulipoitwa mahojiano ( interview) na maisha yote hayo yanahitaji pesa sasa ikiwa una mkopo chuoni achana na imani kuwa pesa haitoshi wewe simamia na kufanya mambo chini ya pesa unayopewa angalia utunze hata elfu hamsini kwa kila ingizo ( bumu) hapo ukimaliza utakuwa na ziada ya kukusukuma kutafuta ajira au namna nyingine ya maisha, jiulize ikiwa utamaliza chuo na ukapata kazi sawa na ingizo la mkopo kwa mwezi maisha yatakushinda? kuna wafanyakazi mnalipwa nao thamani sawa ya pesa lakini maisha yanaendelea na ziada wanabaki nayo kwa nini ushindwe? Chunguza maisha yako kwa siku unaishi kwa gharama za zaidi ya elfu nane miatano? ( ingizo la mkopo kwa siku) jibane sana uishi hata kwa elfu tano basi ili ubaki na elfu tatu miatano itakusaidia hiyo siku ukimaliza mafunzo. 

Kuna fursa kubwa sana ambayo kwa sasa ndio ina nafasi kubwa sana katika kusaidia watu kupata ajira nayo hiyo ni kujitolea, sasa watu wanaojitolea wengi wao ndio huingizwa kwenye mfumo wa ajira iwe taasisi binafsi au za kiserikali na pia katika kujitolea kuna uzoefu unapata katika taaluma yako lakini usisahau kuwa maana halisi ya kujitolea ni kufanya kazi bila malipo ya kifedha sasa utaweza kweli kujitolea ? Kwa namna yoyote ile ukiweza jitahidi utoke chuo ukiwa na pesa ya kukufanya uishi mtaani kwa miezi sita hivyo hata ukipata pa kujitolea nina amini ndani ya miezi sita watakuwa wameshakufikiria kukulipa ndio maana nimesema angalau utoke na ziada ya miezi sita, tumia mkopo wako kwa nidhamu huku ukiishi maisha ya maandalizi. 

Makala hii imeandikwa na Saul Kalivubha , Mwanasayansi. 

+255652 134707

Sunday, 12 November 2023

EPUKA MARAFIKI HAWA ILI UFANIKIWE

 KAMA UNA MARAFIKI HAWA HUWEZI KUFANIKIWA  


Marafiki ni sehemu ya maisha ya kila siku maana sio rahisi kuishi bila marafiki hata mtu awe na tabia ngumu vipi kiasi cha kuonekana havumiliki ila tambua ana marafiki ambao wanamvumilia na tena wanapendana. Kitu ambacho wengi hatukijui ni mahusiano kati ya marafiki na mafanikio, kuna mahusiano makubwa kati ya mafanikio yako na aina ya marafiki ulionao ndio maana kuna mwandishi na mwanafalsafa maarufu aliwahi kusema mafanikio yako ni wastani ya marafiki zako watano ambao mnatumia muda mrefu kuwa pamoja, kwa ufafanuzi wa haraka ni kuwa ukimuona maskini mmoja jua kuna maskini wengine watano anaoshirikiana nao na ukimuona  tajiri mmoja jua kuna matajiri watano anaoshirikiana nao .

Marafiki ni chachu ya mafanikio yako kwa sababu  ni ngumu kuwa na rafiki mfanya biashara ilihali wewe huna biashara kwani maingezi yenu yatapishana tu na kama ikitokea hivyo basi jua kuna unafiki kati yenu yaani maongezi yenu hayana maana na hakuna urafiki hapo kwa sababu.

Kabla hatujaenda kwenye marafiki wa kuwaepuka hebu angalia mifano hii na kisha jichunguze uone ukweli ulivyo.

Mtu ambaye anafeli sana jambo fulani Jaribu kuchunguza marafiki zake utakuta wanafarijiana kuhusu kufeli kwao.

Mtu ambaye ana starehe nyingi ambazo zimeguka kuwa kikwazo chake cha mafanikio Jaribu kumfuatilia utakuta ana marafiki ambao anashirikiana nao na wanajiona wapo sahihi kabisa kufanya hivyo ndio maana wanaendelea.

Ukiona mtoto kuna tabia haachi jua kuna mtu anamuhamisisha kuendelea nayo hiyo tabia. 

Umeona mifano hiyo ? Bila shaka umepata mahusiano kidogo na pengine hata wewe kuna jambo unaendelea nalo kwa sababu kuna mtu nyuma ya jambo hilo , na mfano wa mwisho ni huu hebu angalia michango ya mtu maskini akiwa ana jambo lake kama harusi na kisha angalia michango ya jamaa zake kisha fanya hivyo hivyo kwa tajiri hapo utagundua kila mtu kachangiwa na marafiki wanaofanana uwezo  na hapo ndipo tunarudi kwenye ule ukweli kuwa upo sawa na marafiki zako.

Kuna marafiki ambao unatakiwa kuwakwepa  na kama unao basi tambua kuna hatua hutaziona za kimafanikio, marafiki hao ni hawa wafuatao :

Wanaolalamika sana;hawa watakuambukiza tabia ya kukwepa kuwajibika kwa makosa yako mwenyewe kwa sababu kwa tafasiri ya haraka ya mtu mlalamikaji ni kuwa haoni kuwa anakosea bali muda wote anaona wengine ndio wenye makosa na mwisho wa siku mtu anayelalamika sana huwa anaishia kuwa mtumwa wa wengine, ukiwa na marafiki hawa sio muda mrefu nawe utaanza kuwa mlalamikaji na kunyonyeshea vidole wengine kila muda. 

Marafiki wenye mitizamo ya kimaskini, hawa ni wale ambao wameridhika na hali zao za kuteseka na ukosefu wa fedha yaani tayari wameukubali umaskini, watu hawa wanakuwa na kauli nyingi za kutetea umaskini wao na pia huwa ni wavivu wa uthubutu  kwa sababu tayari wameshahalalisha umaskini wao na utawasikia mara nyingi wakijificha pia kwenye imani za Mungu kama vile kusema ni mpango wa Mungu wao kuwa hivyo na wengine huanini utajiri ni dhambi hivyo kila tajiri wanamuita mshirikina( freemason) ,Kaa mbali na watu hao watakuambukiza umaskini na ikitokea ni ndugu zako ambao huwezi kuwakwepa basi jua una kazi kubwa ya kufanya kutengeneza ukoo tajiri kutokea kwako.

Marafiki wanakutafuta tu kwenye uhitaji, hawa ni wale watu ambao kila mkikutana lazima kuna jambo upoteze , yaani ukiona simu yake tu basi jua lazima mazungumzo yenu yaishie na wewe kumpa kitu au kutoa ahadi utampa lini na ni  siku chache sana wao kukutafuta kwa mijadala mingine ya kimaisha, hawa watu hawakupa mawazo mapya bali wanakufanya uwafikirie wao tu tena kwa kuwapa vitu.Kusaidiana ni sehemu ya maisha ila epuka watu ambao muda wote wamekugeuza kituo cha msaada kwa sababu usipokuwa makini watakugruza mtumwa wao yaani watajiona muda wote wana haki ya kusaidiwa na wewe na siku ukikosa watajua umefanya makusudi watasahau siku ulizowasaidia na kuanza kukulaumu na kumuona yule ambaye hajawsaidia hata siku moja ndio mtu mzuri anayefaa.

Marafiki wanaotaka wewe tu ndio uwatafute, Kaa nao mbali kabisa tena ukiweza futa hata mawasiliano yao na kama ni ndugu  basi ishi nao kama wanavyoishi na wewe acha kuwatafuta mpaka pale kwenye ulazima wa kufanya hivyo kwa sababu ukikubali tu kuwa mtu wa kuwatafuta wewe muda wote jua utakuwa mtumwa wao na utaanza kuwafikiria wao muda wote hali ambayo itafanya ushindwe kufikiria ya kwako vizuri na ushindwe kwenda mbele kwa sababu wao wapo nyuma maana huo ujasiri utaukosa na usipokuwa makini utajikuta kwenye madeni ya kukopa mpaka muda wa maongezi ili tu uwasiliane nao na huku kwenye simu zao wana salio la kutosha , mtu ambaye anataka wewe tu ndio umtafute sio kwamba hiyo ni tabia yake bali kisha ona udhaifu wako na hili uthibitishe hilo fuatllia watu wake wa karibu je anawafanyia kama wewe?

Marafiki wajuaji , hawa ni wale ambao wanakukosoa hata kabla hawajakusikiliza na tena wanamalizia ulichokianzisha bila kujua ungemaliziaje, hawa ni marafiki hatari sana usiruhusu muda mwingi kuwa nao kwa sababu watakufunza ubishi usio na faida.

Marafiki waongo na wambea, Muongo ni mtu ambaye anakusambizia au kukuzuishia habari za uongo ila mmbea yeye ni yule ambaye anakusambazia habari za kweli ila bila idhini yako na kwa watu ambao hawakutakiwa kuzijua hizo habari, hao ni watu hatari sana kwa sababu watakufanya mweupe kwa kutoa siri zako na kufanya rahisi kwa adui zako kukushambulia na ukiwa na marafiki hao yawezekana mipango yako ikawa inasindwa kila mara kwa sababu kuna muda inanidi watu waone tu matokeo na sio maandalizi kwa sababu watakuzuia .


Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul kalivubha, mtafiti 


+255652 134707

Saturday, 20 May 2023

HIZI NDIO SABABU ZA KWA NINI UNANG'ANG'ANIA SEHEMU UNAYOFUKUZWA

 HIZI NDIO SABABU ZA KWA NINI UNANG'ANG'ANIA SEHEMU UNAYOFUKUZWA. 

Yawezekana ukawa muhanga kwa sasa au ukawa tayari umepitia hali hiyo na ukikumbuka unajishangaa ni vipi uliweza kuvumilia ilihali ulikuwa unafukuzwa? Au ulipewa dawa? Muda mwingine sio dawa bali kuna sababu ambazo ndio kiini cha somo hili .

Kuendelea kubakia unapofukuzwa kuna hasara nyingi sana japo hasara kubwa sana ni kujipotezea muda wako maana unakuja tena  kuanza moja muda ambao ungekuwa kwenye kumi  na hasara nyingine ya pili kubwa ni gharama ulizotumia kugharamia sehemu isiyo yako .

Inawezekana ikawa ni kazini kwako, sehemu uliyopanga au kwenye mahusiano kote huko huwa tunafukuzwa lakini tunaendelea kupakumbatia na mwishowe tunakuja kukubali ukweli tayari tulishapoteza muda na gharama. 

Kufukuzwa mara nyingi hakuji kama dharura bali huja kwa maandalizi na lazima kuwepo na viashiria viwili vitatu vinavyokuonyesha kuwa upo unafukuzwa . Swali ni je watu huwa tuna upofu kiasi cha kutoona hivyo viashiria vya Kufukuzwa?  Sababu zipo za majibu hayo zipo kwenye somo letu hili la leo .

SABABU ZINAZOFANYA  UENDELEE  KUNG'ANG'ANIA SEHEMU UNAYOFUKUZWA ;

1. KUTOKUBALI MATOKEO; Hapa mtu anakuwa haamini kama kweli fulani anaweza mfukuza au kumkataa hivyo kila siku unakuwa unajipa sababu za kukutia moyo kuwa hilo haiwezekani labda tu ni mabadiliko ya muda mfupi na kesho mambo yatakuwa sawa lakini siku zinazidi kwenda na mambo hayawi sawa hatimaye unakuja kufukuzwa kwa lazima hapo ndipo unagundua kumbe ilikuwa inamaanisha.

2. KUHISI WEWE NDIO UNAMAKOSA MUDA WOTE;Mara nyingi hii hutokea kwenye mahusiano unakuwa unajiona wewe ndio mkosaji hata kwenye makosa yake kwa mfano anaweza kupunguza mawasiliano lakini ukajiona wewe ndio unakosa la kumtafuta na ukimtafuta sana hapokei simu zako wala hajibu jumbe zako unajiona tena wewe ndio mkosaji kwa sababu unamsumbua sana kumbe ndio kiashiria cha kukufukuza hicho ni wewe tu hutaki kuelewa. 

3. KUJIHISI UTAKOSA PAKWENDA: Hii inatokea kote kwenye mahusiano hata kazini unakuwa unahisi ulipata kazi hiyo kwa bahati tu au ulimpata mtu huyo kwa bahati tu ikitokea unatoka hapo huamini tena kama utapata kazi nyingine au utapata tena mtu wa kukupenda. Unakosea sana ndugu yangu usikubali kuvumilia sehemu unayofkuzwa hapo sio kwako tayari ulishafukuzwa sasa kuendelea kuvumilia ni kujiweka kwenye mateso ambayo yange epukika tu kama ungefanya maamuzi magumu na mapema, usikubali kuwa mtumwa ilihali kuna sehemu unaweza kuwa huru kwa maana utakonda bure na hatimaye kupata magonjwa ya kisaikolojia. 

5. Ujinga; Hii ni kama ukosefu wa ufahamu wa kutosha ambapo mtu yoyote anaweza kuwa mjinga kwa kipindi fulani na akajikuta yupo sehemu analazimisha  kujenga nyumba na mtu ambaye usiku anarudi kuibomoa. Jinsi ya kutoka kwenye ujinga ni kutafuta maarifa ya kutosha kuhusu aina ya safari uliyonayo maana ukiijua vizuri aina ya safari yako hutakubali upotezewe muda na msafiri ambaye hamchangii njia moja. 

Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul Kalivubha.

Pia unaweza pata nakala za vitabu vikakusaidia kukuza ufahamu wako kwa mawasiliano  +255652 134707

Tuesday, 11 April 2023

SABABU ZITAKAZOFANYA UKOSEE KUCHAGUA MWENZI WA MAISHA.

SABABU ZITAKAZOFANYA UKOSEE KUCHAGUA MWENZI WA MAISHA.

Ni jambo la kawaida kuishi wawili( mke na mume) ambapo nyuma ya kuishi pamoja kuna maandalizi ya kumtafuta huyo mwenza hivyo kuna wakati ukifika karibu kila mtu anakuwa na picha ya yupi anamtafuta ndio maana kuna ambao utawakataa na kuna wengine utawakubali , hali ya kumkataa mmoja na kumkubali mwingine ni dalili kuwa kichwani mwako kuna picha ya umtakaye na huyo uliyemkubali ndio picha halisi ya umtakaye, lakini kwa hali isiyoyakawaida kuna kipindi unamchukia uliyemchagua au unaona makwazo kwa aliyekuchagua ilihali yeye ndiye aliyefanya maamuzi ya kukuchagua, hii chanzo chake ni kipi?.

Katika harakati za kumtafuta mwenzi huwa kuna mengi sana nyuma ya zoezi hilo na hapo ndipo huwa kuna kupatia au kukosea zoezi hilo na moja ya sababu hizo ni kama zilivyojadiliwa hapa chini :

Kumtafuta mwenzi kwa ulimbukeni, Limbukeni kwa tafasiri ya haraka ila makinifu ni mtu mshamba au mtu ambaye anakurupukia vitu bila kuwa na ufahamu navyo . Kuna mtu anakuchagua kama mwenzi wake kwa ulimbukeni tu ila kikawaida ingefaa ajitulize sana kabla ya maamuzi yake hayo sasa baadaye mkiwa tayari mpo naye anakuja kugundua kuwa kumbe sio wewe anayekutafuta hapo sasa anaanza kukuchonga ili uwe yule anayemtafuta na hapo ndipo ataanza kukukosoa kila siku .

Kumchagua mwenzi bila utulivu, hii inatokea hasa kwa mtu ambaye anajiona kachelewa hivyo anakuwa haangalii tena vigezo bali anaangalia tu mtu yupi yupo tayari ( kama ni mvulana anaangalia msichana yupi yupo tayari na kama ni mvulana basi anaangalia msichana yupi yupo tayari ) Hapa kukosea ni rahisi sana japo inawezekana ukabahatisha lakini hiyo ni kwa wachache sana wengi hukosea.

Kupitia kipindi cha kukataliwa sana! Mtu aliyepitia kipindi cha kukataliwa sana asipojithibiti kuna uwezekano mkubwa akaja kukosea kuchagua mwenzi kwa sababu atajiona mwenye mkosi sana sasa siku akikubaliwa na yoyote ataona kama bahati hata kama huyo aliyemkubali si sahihi. 

Kufanya maamuzi haraka baada ya kuachwa! mtu anapoachwa huwa hana utulivu na ile hali inamfanya akose utulivu kwa sababu ile hali ya kurudi tena single ( pekee) inampa msongo na anakuwa anataka asionekane hana soko hivyo anaweza kuamua kumkubali yoyote bila kujali ni sahihi au la.

Shinikizo la wengine! Hii ni pale ambapo unataka kuendana na wengine bila kujali kuwa ni wakati sahihi au la bali anataka tu afanye kama wengine kwa mfano marafiki zake wote wameoa bado yeye tu hali hiyo inamfanya na yeye aamue kuoa .

Kukimbia umri! Hii ni sababu nyingine kubwa ya kukosea kwa sababu Kukimbia umri kuna fanya uchague bila kuzingatia ubora wa unachokitaka , na hatimaye kujikuta umekosea. 


Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul Kalivubha 

Kitabu cha siri za urafiki kinapatikana soft copy ( nakala tete) kwa Tsh4000. 

0652 134707/0756388688