Friday 22 March 2024

USIPOISHI NAO KWA AKILI NYINGI WATU HAWA UTAJIKUTA MATATIZONI MUDA MWINGI.

 USIPOISHI NAO KWA AKILI NYINGI WATU HAWA UTAJIKUTA MATATIZONI MUDA MWINGI.

1.Wanaojiona sahihi muda wote hawa hawachelewi kukubebesha makosa yasiyo kuhusu. 

2.Wajuaji kupitiliza hawa muda wote watakulaumu tu kwani kila jambo watakuona unakosea hata kama wao ndio wamekosea.

3.Wanaokutafuta kwenye shida tu hawa utawaona marafiki ukiwa na kitu cha kuwapa ila  siku ukiwa kwenye uhitaji watakuacha mtaroni.

4.Waropokaji hawa muda wowote watamwaga siri zako mbele ya wasiotakiwa kuzijua hivyo hakikisha hawajui mambo yako ambayo hayatakiwi kujulikana na wengi.

5 Wenye imani za kishirikina kupitiliza hawa hata kwenye jambo la kawaida wao watakushauri uende kwa mganga wa kienyeji kwa sababu wao hawaamini tena kwenye ukawaida

6.Wenye imani za dini kupitiliza, hawa pia kwenye sehemu unayotakiwa utumie akili zako wao watakushauri ufunge na kuomba ili upate majibu sasa ikiwa zaidi hii inakuwa kupoteza muda.

Pia watakushauri uvumilie hata sehemu unayotakiwa kuondoka. 

7 .Wenye wivu wa mapenzi kupitiliza, Hawa kwa muda mfupi watakufanya ufurahie mapenzi ila kwa undani zaidi watafanya ufeli mambo ya msingi kwa mfano unaweza kupata dili la maana la pesa ila watakukataza usiende kalifanya wakihofia kuibiwa kimapenzi. 

8 . Wenye mitizamo ya kimaskini, hawa muda wote wanaamini utajiri ni dhambi hivyo ukiwa nao na wakakumudu basi watakushauri uwe sawa nao.

9.Waliokata tamaa na kuridhika, hawa muda wote watakwambia maisha ndio haya haya.

10 Wenye utoto ilihali ni wakubwa, hawa watalia kwa kila changamoto yaani kwao hawana changamoto ya kuvumilia bali kulia na kukata tamaa, ukiwa nao na wakakumudu utafanana nao.

Mwanasayansi Saul kalivubha.

+255652 134707

Tuesday 19 March 2024

KOSA LIKIKUFUNZA SIO KOSA TENA BALI NI UPYA ULIOKUWA HUUJUI

KOSA LIKIKUFUNZA SIO KOSA TENA BALI NI UPYA ULIOKUWA HUUJUI.

Sifa ya makosa ni kutoa adhabu na inaweza isiwe muda huo ulipolifanya kosa ila ni lazima litakuadhibu tu mbeleni hivyo hakuna namna unaweza kukwepa adhabu ya kosa lako.

Taarifa inayopendeza ni kuwa kosa likikupa adhabu nawe ukaona kama funzo basi hilo sio kosa tena bali ni upya ambao ulikuwa huujui hapo kabla na njia pekee ya wewe kuujua huo upya imekuwa ni kupitia kukosea.

Usifanye makosa makusudi hapo utakuwa sasa unatafuta adhabu za kujitakia na yawezekana adhabu hiyo isiwe funzo lolote kwako kwa sababu sio jipya bali ulilijua kabla. 

Kwenye mchezo wa mpira timu inafungwa kupitia makosa hiivyo adhabu yake ni kufungwa magoli ila baadaye wachezaji wakimakinika kutafuta walifungwa vipi basi watagundua mbinu zipi wafanye ili wasifungwe tena  na hapo itakuwa wamejifunza kupitia makosa na adhabu waliyo adhibiwa.

Japo makosa mengine adhabu yake ni kali na utaadhibiwa tu bila  kujali hukuwa ukijua kuwa ni kosa hapo kabla ila ukimakinika zaidi utajifunza tu .Kosa bila adhabu ni ngumu kuwa funzo na kikawaida kosa lisilo na adhabu yawezekana lisiwepo labda tu uamue kutuiona hiyo adhabu.

Ukiona maisha yanakuadhibu Kwenye jambo fulani wewe kaa chini tulia utafute wapi ulikosea.


Mwanasayansi Saul kalivubha 

+255652 134707

CHANGAMOTO NI BURUDANI KATIKA MAISHA, BURUDIKA NAZO BADALA YA KULIA LIA HOVYO.

 CHANGAMOTO NI BURUDANI  KATIKA MAISHA, BURUDIKA NAZO  BADALA YA KULIA LIA HOVYO.


Mwanafalsafa mmoja aliwahi kusema ukitaka ufurahie adhabu basi ukipewa usiione kwa sura ya adhabu bali ona kama ni sehemu kama wajibu wako, kwa mfano ukipewa adhabu ya kumwagilia maua wewe ona ni wajibu wako kufanya hiyo ili maua yakue na kustawi.


Changamoto ni burudani kama zilivyo burudani ni ngumu kuburudika bila kuvuja jasho, kwenye suala la burudani kuna upande utavuja jasho na kuna upande utaburudika ila inaitwa burudani na watu hufurahi kwa sababu wameamua kumakinika na upande wa furaha kuliko upande waliovuja jasho.

Maisha ya kukosa kazi kwa muda, kuachwa kwenye mahusiano na mengine mengi yenye sura ya changamoto ni sehemu tu moja wapo  ya burudani ambayo ndio ya kuvuja jasho na kama ukiendelea kukaza utafikia ule upande wa pili wa burudani ambao ni wa kufurahia.

Kwenye hii burudani ya maisha hakuna mtu asiyepitia upande wa kuvuja jasho ambao ndio changamoto na burudani haina maana kama itakuwa na upande mmoja tu wa furaha, ukiona watu kwenye viti virefu au kokote wapo wanajipongeza basi jua wana upande mwingine waliopitia ambao ndio uliwapa hizo pesa.

Ikitokea unafukuzwa ama kukataliwa usione kwa sura ya kukomolewa au kama vile umeadhibiwa bali ona hiyo ni sehemu tu ya burudani ambapo unaandaliwa kwenda kukubalika kwingine tena panaweza kuwa pazuri zaidi ya ulipofukuzwa. Tatizo ni pale ambapo utaiona hiyo changamoto kwa sura ya kukomeshwa hapo utajikuta kwenye maumivu, kulia na kulalamika hovyo kitu ambacho hakitakupa unafuu bali kukuumiza na mbaya zaidi kukufanya uje ukosee tena kwa sababu utafanya maamuzi bila utulivu. 

Maisha yana changamoto nyingi sana na nzito ila ukisema kila moja uione kwa sura yake basi kila siku utakuwa mtu wa kulia hovyo badala ya kujifunza kupitia changamoto hizo.


Mwanasayansi Saul kalivubha

0652 134707

Saturday 9 March 2024

HARAKATI HAZIMTAKI MTU ANAYEONGOZWA KWA MIHEMKO

HARAKATI HAZITAKI MTU ANAYEONGOZWA KWA MIHEMKO.


1.Mtu ambaye akiambiwa biashara fulani inalipa anaikurupukia.

2.Ambaye akiambiwa alisemwa vibaya muda huo huo anawafuata wahusika.

3.Mtu ambaye akiambiwa kasalitiwa muda huo huo anawasha moto.

4.Mtu ambaye anataka kufanya kila kinachosifiwa sana.


KAMA UNA SIFA HIZO HAPO JUU BASI HUWEZI KUWA MWANAHARAKATI.


Kuwa mwanaharakati uwe na sifa hizi.

1.Usiyekurupuka hovyo.

2.Mchunguzi kabla ya kuongea.

3.Usiyekata tamaa kizembe.

4.Uliyetayari kukoselewa.

Michakato yote haikosi changamoto ni lazima changamoto zije kukupima kuona kweli utaweza kuyamudu mafanikio? 

Changamoto zinapokuja kuna mambo mawili ama hiyo safari sio yako au ni yako ila unatakiwa kukomaaa, sasa kabla hujasema hiyo safari sio yako ni lazima ukomae haswa maana ukiwa mtu wa kukwepa changamoto kwa sababu tu ya mihemko yako basi hakuna safari utakayoiweza hapa Duniani. 


Na ukiwa mtu wa kufanya mambo kwa kukurupukia kwa sababu tu ya mihemko yako basi utakuwa pia mtu wa kuanza upya kila mara kwani itakuwa ukifika njiani unagundua hiyo njia siyo yako bali uliikurupukia tu 


Mwanasayansi Saul kalivubha 

0652 134707

Thursday 7 March 2024

UKIONA WANAKUNG'ANG'ANIA WAKUPE UTAJIRI WA HARAKA JUA WAMEKUONA AKILI YAKO NI CHENGA

 UkIONA WANAKUNG'ANG'ANIA WAKUPE UTAJIRI WA HARAKA JUA WAMEKUONA AKILI YAKO NI CHENGA 😔 

Umewahi kusikia watu wakijinadi kutoa utajiri wa HARAKA? Yaani kulala maskini na kuamka tajiri? 

Taarifa isiyopendeza ni kuwa kama nawe ni mmoja wa wateja wao basi jua kuna kitu kwako hakipo sawa na tayari wamekiona ndio maana wanakulazimisha uingie kwenye hiyo fursa hiyo.

Wale watu wana akili sana na wapo vizuri kuisoma akili yako hasa kwenye maamuzi yako na utulivu wako na wakiona una maamuzi ya haraka yasiyo na subira basi wanajua wewe ni mteja wao mzuri katika fursa hiyo.

Tangazo lenye lengo la kutoa utajiri wa haraka huwa linawahusu watu wenye sifa hizi:

1.Wasio na utulivu, kama huna utulivu basi utakuwa mteja wao kwa sababu ukikosa utulivu utakuwa mtu wa kufanya mambo bila kufikiria kwa kina, kwa lugha rahisi unakuwa mvivu wa kupima matokeo na matendo ndio maana akija mtu akikwambia jambo fulani ukilifanya leo tu basi kesho utakuwa bilionea unaliendea kwa haraka sana bila kufikiria kuwa kama hilo jambo lingekuwepo si tungekuwa wote mabilionea.

2 Kupenda matokeo ya haraka, kama unapenda matokeo ya haraka basi nawe ni mteja kwa sababu ukiambiwa utajiri utakuja kesho haraka utaamini ila ukiambiwa utakuja baada ya miaka kumi utaona ni utapeli. Kwa lugha nyepesi hawa ni watu ambao hawana subira bali wanataka kila kianzacho leo basi kesho kilete matokeo chanya. 

3.Waliokata tamaa, mkata tamaa ni mtu ambaye haamini tena kwenye kushinda hivyo amebaki kusubiria miujiza tu , kama umekata tamaa kiwango cha mwisho basi nawe utakuwa mteja.

4.Wanaokimbizana na umri, kuna watu ambao kwa namna moja ama nyingine wanajiona kama wameachwa na umri hivyo hawataki tena kitu cha kusubiri bali wanataka tu jambo lianze leo na kesho lije na matokeo, kama upo kundi hili basi nawe ni mteja.

Matangazo haya ya kujinadi kuwa kuna utajiri wa haraka yanzidi kushia kasi kwa sababu watoaji matangazo wamegundua kuwa watu wengi sasa hivi wanataka sana mambo ya miujiza na hawataki tena kusubiria hivyo wapo tayari kulipa gharama ya kupewa utajiri wa haraka usio na uhalisia kuliko kutumia pesa hiyo kutafuta utajiri wenye uhalisia.


Mwanasayansi Saul kalivubha

+255652134707

Monday 4 March 2024

MAISHA SIO MSTARI MNYOOFU,KONA ZISIKUFANYE UTOKE MCHEZONI

 MAISHA SIO MSTARI MNYOOFU, KONA ZISIKUFANYE UTOKE MCHEZONI.

Kinachotutesa wengi ni kuishi kwa imani kuwa maisha ni mstari mnyoofu na hili sio tu tumelijenga sasa la hasha! Bali hata mifumo ya malezi inachangia hilo.

Kuna ambao wamelelewa kwa kuaminishwa kuwa vitu hupatikana kwa wakati ule watakao  hivyo kufanya ukubwani watu wapate shida sana pindi wanapokutana na uhalisia wa maisha kuwa maisha sio mstari mnyoofu.

Utotoni tuliamini kwa ambao wamefika shule wengi  waliamini shule ikiisha tu leo basi kesho wanapata ajira na wakipata ajira tu tayari wananunua nyumba, gari, kuoa/kuolewa na  kufurahia maisha. Hii nadharia ambayo inaonyesha kuwa maisha ni mstari mnyoofu lakini tukija kwenye michakato ya maisha ni wachache sana wanaopitia mstari mnyoofu na hata kama mambo yako yatakunyookea kwenye jambo moja basi kwenye jambo la pili mambo hayakuwa na unyoofu. 

Utotoni ilikuwa kila ukililia kitu unapewa kwa wakati na  hapa ndio mwanzo wa imani hiyo kuwa maisha ni mstari mnyoofu ilipoanzia ambayo ipo kinyume na uhalisia wa maisha. 

Maisha sio mstari mnyoofu na kuwa hivi haimaanishi kwamba ni changamoto bali ndio uhalisia wenyewe ambao unatakiwa kupambana nao na sio kujiona mtu mwenye mikosi kwa sababu tu umemaliza shule na kukaa mtaani miaka mitano bila kazi, umeachika kwa mchumba uliyempenda au umeanza kazi tu unataka kila kitu ununue kwa mshahara mmoja hilo haliwezekani na ukitaka liwezekane basi utajikuta gerezani. 

Kuna ambao wanaanza mahusiano yao ya kwanza na yanageuka ndoa ila kuna wengi ambao wanapitia dhoruba kadhaa za kuachika ndio baadaye zinakuja ndoa, kuna muda maisha yanakupitisha sehemu ambayo hapo zamani ulijua wanaopitia humo wana dhambi kumbe ni mapito tu kuwa maisha sio mstari mnyoofu bali kuna kona nyingi za kukomaa nazo.

Kuna wanaomaliza vyuo na kupata ajira ila kwa zama hizi kuna mtu mpaka kasahau kuwa na yeye alisoma chuo kwa sababu ana miaka mingi mtaani. Kumaliza chuo na kukosa ajira haimaanishi kuwa maisha ndio yamefikia ukomo bali hiyo ni kona ambayo unafaa ukomae nayo na hapo ndipo ujuzi wako wa udereva unapimwa.

Dereva mzuri haogopi kona za bara bara, ukiona dereva anataka tu apite barabara tambarare na kukwepa kila barabara yenye kona basi kuna shida kwenye ujuzi wake tena cheti chake kichunguzwe na vivyo hivyo hata kwenye harakati za maisha kama unataka kila jambo lako lisiwe na kona basi haya maisha yatakushinda kwa sababu kuna muda utajua kesho utapata ila unakuja kupata kesho kutwa .

Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul kalivubha.

+255652 134707

Sunday 3 March 2024

KAMA UNATOKA UKOO HUU BASI JUKUMU LA KUTENGENEZA UKOO MPYA TAJIRI LINAKUHUSU LA SIVYO UWE PIA MASKINI NA WEWE

 KAMA UNATOKA UKOO HUU BASI JUKUMU LA KUTENGENEZA UKOO MPYA TAJIRI LINAKUHUSU LA SIVYONAWE MASKINI. .

Dhana kuwa mambo hufuata watu ndani ya ukoo ina ukweli wake na mifano yake ipo wazi tu , tukiachana na mfanano wa vinasaba pia hata mazingira huchangia hali hiyo japo kwa ulimwengu wa kiroho watalaam wanasema kuna roho huwa zinatembea ndani ya ukoo fulani. 

Ulimwengu wa kitajiri na maskini kuna koo utakuta ni tajiri kutoka Babu mpaka mjuu na kuna koo utakuta ni maskini kuanzia Babu mpaka mjukuu na hapo ndipo kwenye dhana ya urithi wa utajiri na umaskini. 

Umewahi kuona ukoo fulani mtu mmoja tu ndio tajiri ila wengine wote ni maskini? Kama ndio Jaribu kufuatilia historia ya huyo mtu lazima katumia nguvu kubwa kuwa hivyo wa pekee na hiyo nguvu ndio inaitwa nguvu ya kujiengua kutoka kwenye ukoo maskini na kujitengenezea ukoo tajiri vivyo hivyo kuna mtu maskini ila wengi kwenye ukoo wake ni matajiri basi huyo yupo anajiengua kutoka ukoo tajiri na kutengeneza ukoo wake maskini. 

Sio kazi kubwa kujijua upo kwenye ukoo upi bali angalia tu viashiria kama kwenu hakuna tajiri na historia ya babu zako pia hali ilikuwa hivyo hivyo basi jua una kazi kubwa ya kufanya kuukana ukoo huo na kutengeneza ukoo mpya tajiri ( sina maana uukane kuwa wewe sio mwana ukoo la hasha bali uukane umaskini unaotembea kwenye ukoo wenu), Sasa uta ukana vipi?

HAYA NDIO MAMBO YA KUFANYA ILI KUACHANA NA UKOO MASKINI NA KUTENGENEZA UKOO MPYA TAJIRI. 

1.Kwenye kuoa/kuolewa jitahidi uambatane na mtu ambaye sio maskini wa fikra ( anaweza kuwa maskini wa kipato ila asiwe maskini wa fikra yaani akilini awe tajiri ajaye tena kwa vitendo).

2.Usisumbuke kumaliza umaskini wa ukoo wenu hili hutaweza bali nawe utaishia kuwa maskini pia bali anza kuandaa utajiri mpaka utakao wazaa waukute ili waanzie pale ulipoishia wewe. 

3.Kubali kulaumiwa na wana ukoo bali usiache kuwa sawa nao maana ukianza kujipata lawama zitakuwa nyingi sana na hasa pale utapokuwa ukikwepa mizigo yao kwa mfano wataanza kutaka usomeshe watoto wao wote, uwajengee nyumba na mengine mengi lakini je kweli ukiwafanyia hivyo utatoboa ?

3.Wekeza kwenye mipango ambayo hata ukifa yenyewe haifi bali itaendelea kuishi na hivi ndivyo wafanyavyo matajiri wote ambao wanataka utajiri wao usife pindi wao wakifa.

4.Usikubali kuwa mshirikina ili upate utajiri hapa nawe utakuwa maskini tu kwa sababu kwenye hizo imani za kishirikina kuna laana tupu na kuna ambao wameishia jela na hata utajiri hawajapata , kufikiria utajiri kwa njia ya kishirikina ni matokeo ya uvivu wa kufikiria na kukosa utulivu wa subira.


4.Andaa watoto wako kuwa matajiri pindi wakiwa wadogo na kwenye hili uwe mkali kidogo kwa sababu wanaweza kulemaa wakihisi hata wasipo pambana bado tu watarithi utajiri wako, waandae zaidi kuendeleza mali na sio kurithi mali .

5.Usikate tamaa kizembe ukiona harakati zinakuwa ngumu kwako usianze kujifariji kwa kauli zisizo faa na za kimaskini kama vile 

" Maisha ndio haya haya"

 "Maskini pia ni mtu"

"Sisi kwetu ndivyo tulivyo hatuwezi biashara "

Hizo ni kauli za kimaskini na zisizo na ukombozi wowote ule kifikra bali kukukandamiza tu kuwa maskini zaidi.

Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul kalivubha 

#fikia ndoto zako 

+255652 134707