Monday, 26 October 2020

JIAMBIE UKWELI UPIGE HATUA

 JIAMBIE UKWELI UPIGE HATUA 


Habari ndugu msomaji wa blogu  yetu pendwa na karibu tena katika safu hii ya kila wiki ya NASAHA ZA WIKI , leo tuna somo ambalo litafumbua macho yetu kuona hatua mpya mbele  hivyo tuambatane sote. 


Mara ya mwisho kujiambia ukweli ni lini?  Kwa uaminifu jipe majibu stahiki katika swali hilo  kwa sababu wengi tunajidanganya ndio maana leo nimekuja na somo hili ili tuone madhara ya kujidanganya na jinsi ya kuachana na tabia hiyo ya kujiadanganya .

Unapenda kudanganywa?  Jibu litakuwa hapana! sidhani kama kuna mtu hupenda kudanganywa  .Kudanganya  ni hali ya kuaminisha uongo utumike kama ukweli  mfano umelala kitandani unapigiwa simu ukiulizwa uko wapi?  Unajibu upo kazini  tayari hapo umemuaminisha uongo ya kuwa upo kazini lakini ukweli upo kitandani hivyo umemfanya mwenzako aamini ulichomuaminisha. Sifa ya uongo ni kuendelezwa hivyo ukidanganya mtu utajitahidi utafute tena mazingira ya uongo ili kuujazia nyama uongo wako uonekane ukweli  ndio maana mtu akidanganya kwa jambo moja kuna uwezekano mkubwa hata jambo la pili litalokofuata likawa sio la kweli .Bila shaka umepata picha ya uongo sasa tumeona mtu akiwa anadanganya mwingine ni vipi ukiwa unajidanganya? 

KUJIDANGANYA. 

Kujidanganya ni kutafuta usahihi kwa kuwalaumu wengine kwa makosa yako  mfano umechelewa kufika kazini hivyo ukachelewa pia kumaliza majukumu ya siku lakini  badala ujiambie ukweli kuwa tatizo ni kuchelewa ndio chanzo cha yote  wewe unajitetea kwa  kujiambia kuwa kazi zilikuwa nyingi sana hivyo kosa ni la mwajiri kukupanga peke yako kitengo hicho, tayari hapo umejidanganya kuhalalisha kuchelewa kwako kuwa sio tatizo bali tatizo ni la mwajiri. Tunajidanganya kila siku katika mambo mengi sana na hali inayofanya tujione kila siku tupo sahihi kwa 100% .

Wayajua madhara ya kujidanganya?  Moja ya dalili za kuwa mtu fulani anajidanganya ni hizi kuu mbili 

1.Kuwa na idadi kubwa ya watu ambao anawalaumu kila siku ikiwa sio watu basi atakuwa na idadi kubwa ya mazingira tofauti tofauti ya kuyalaumu mfano utasikia ni kwa sababu ya mvua, jua kali, foleni, nk na hata siku moja hutamsikia akisema ni sababu ya uvivu wake wa kuchelewa kuamka. 

2.Kuwa na changamoto zinazojirudia hii ni kutokana na sababu kuwa tatizo linakuwa ni yeye ila anajidanganya kuwa sio yeye na kwa sababu tatizo ndio mwanzo wa changamoto ndio maana changamoto za aina moja hujitokeza sana kwake mfano   mwanzo atakwambia tatizo ni pesa ndio maana hafanyi biashara lakini ukimpa pesa  tatizo atakwambia ni muda sio rafiki  na ukimpa muda wa kutosha utasikia akisema tena biashara anayotaka kuifanya sio msimu wake lakini pengine tatizo ni hofu yake au matumizi mabaya tu ya pesa  ndio maana changamoto ya kushindwa kuanzisha biashara imejirudia kila wakati. 

Dalili hizo mbili zinaonyesha wazi madhara apatayo mtu ambaye anakwepa ukweli kwa kuwajibisha wengine katika makosa yake  . Tatizo ukiwa ni wewe utalikwepa kwa kujitetea lakini matokeo ya tatizo hilo yatakurudia kila mara  hivyo utakuwa mtu wa kujitetea kila siku lakini makosa yale yale kila siku unarudia. Kujidanganya ni tabia inayofunga miguu yetu kutembea  kwa sababu huwezi kuendelea mbele ilihali bado hujatatua tatizo linalofanya miguu iwe mizito.  Mfano ukiwa unaendesha gari  betri ikapata shida taa zikazima  badala ya kushughurikia betri ipone wewe ukaamua utafute barabara mbazo zinataa za bararani ndio upite  hapo utakuwa unakwepa ukweli na tatizo litabaki palepale kwa sababu taa za barabarani zikizima na zenyewe? 

JIAMBIE UKWELI. Kila kwenye changamoto wewe tafuta uhusika wako uliofanya changamoto hiyo itokee kisha anza kupambana na tabia hiyo yako. Moja ya mbinu nzuri za kutumia ili uwe unajiambia ukweli ni kutafuta  muda wa tathmini binafsi  ikiwezekana kila wiki au kila mwezi au kila siku ni wewe tu jiwekee ratiba zako , katika kujitathmini huko binafsi   angalia changamoto unazokumbana nazo kwa siku/wiki/mwezi nk na jiulize kwa nini zinatokea na kuendelea kisha orodhesha sababu za kimazingira zinazopelekea changamoto hizo zitokee na orodhesha sababu kutoka kwako namna gani unachangia changamoto hizo zitokee kisha anza kujidhibiti na kujitibu na kama ikiwa ngumu kujitibu peke yako basi tafuta watalaamu wakusaisie.

Makala hii imeandikwa na Saul Kalivubha Mwanasayansi tiba katika maabara za binadamu na mwalimu. 


+255652 134707



No comments:

Post a Comment