Sunday, 13 March 2022

MBINU ZA KUWEKA AKIBA

 JINSI YA KUWEKA AKIBA 

Elimu ya pesa kila siku inakuwa changamoto mpya kwa watu wengi ndio maana  bado kuna watu wanaingiza pesa ya kutosha lakini matumizi yao sio rafiki kiasi cha kuwafanya wabaki na ziada ya pesa . Inawezekana hata wewe ukawa kwenye kundi hilo la watu ambao wanaweka malengo ya kujikomboa kiuchumi kila siku lakini utekekelezaji wake ni mdogo au haupo kabisa, ukijiona wa hali hiyo basi tambua una changamoto katika namna nzima ya kuitawala pesa  na njia rahisi kwa watu  hali zote za vipato ni uwekaji wa akiba na mipango madhubuti ya namna ya kuizalisha hiyo akiba ili nayo ilete faida. 

Akiba kwa tafasiri isiyo rasmi ni namna mtu anavyoijali kesho yake ndio maana leo unajinyima ili kesho ufanikiwe katika jambo fulani , mfano  unaingiza shilingi elfu kumi kila mwezi na unataka baada ya mwaka uwe na mtaji wa laki mbili hapo lengo ni wewe upate mtaji wa laki mbili lakini mfukoni una shilingi elfu kumi ambayo kila mwezi utaipata, kwa kawaida unaweza kuiona ndogo lakini  kuna uwekano mkubwa mtu asiifikishe kwa mwaka .

Kuna elimu nyingi kuhusu uwekaji wa akiba ambazo hutolewa kila leo na pengine ukawa moja kati ya watu ambao tayari wamewahi kuzitumia njia hizo lakini bila mafanikio yoyote, unafikiri tatizo ni nini?  Kuna kitu muhimu kutambua kabla ya kuanza zoezi la kuweka akiba ya pesa nacho ni wazo kuu la kesho, jiulize kesho unataka ufanye nini?  na ili ufanikiwe jambo hilo wahitaji kiasi gani cha fedha?  Ukifahamu kiasi cha fedha unachohitaji ili kufikia lengo hilo utatakiwa kujua kwa sasa wewe unapata kiasi gani cha fedha? iwe ni kwa mwezi au kwa kila siku muhimu uwe na uhakika na kiasi hicho cha fedha. 

Ukijua unaingia shilingi ngapi labda kwa mwezi sasa utatakiwa ujue pia matumizi yako kwa mwezi yakoje? Yanagharimu kiasi kipi cha fedha?  Na je matumizi yako kwa siku mpaka mwezi yanakuruhusu uweze kuyafikia malengo yako? Ukiwa na majibu ya maswali hayo ndipo utaangalia sasa kipi kinawezekana kupuguzwa ili matumizi yako kwa mwezi yapungue. 

Hatua ya pili ni kuorodhesha matumizi yako katika safu mbili , moja iwe ya matumizi ya lazima mfano chakula  n.k na ya pili iwe ni ya matumizi yasiyo ya lazima kisha  tafuta uwezekano wa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ili pesa ambayo ilikuwa inatumika kwenye matumizi hayo  iingie kwenye akiba na pia uanze kujinyima kimatumizi  ili upate pesa ya ziada .

Hatua ya tatu ni kujiwekea mikakati ya kujikumbusha malengo yako kwa mfano unaweza kuwa na utaratibu wa kila siku jioni unapitia daftari lako la malengo ili uwe na shauku ya kuendelea na mapambano bila kuchoka. Unatakiwa Kuheshimu mikakati yako kwa kuwa na nidhamu katika  kuweka akiba ili uweze kufikia malengo yako. 

Hatua ya mwisho ni kuhakikisha pale upatapo pesa  unatoa kwanza kiasi ambacho umeridhia kukiweka kabla ya matumizi mengine yoyote  usifanye makosa kwa kuanza kutumia pesa kwanza kisha ndio ubakize akiba , fanya zoezi hilo kwa nidhamu yote na lifanye kwa kuongozwa  na malengo ya kesho.

Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul Kalivubha 

+255652 134707 

No comments:

Post a Comment