Monday, 22 February 2021

MIAKA 29 YA SAUL KALIVUBHA

 Karibu katika blogu yetu ya fikiandotozako na kama ilivyo ada leo nitajibu maswali ambayo yaliuzwa katika siku yangu ya kumbukizi ya kuzaliwa tarehe 22 February , maswali yalikuwa jumla 150 na nilipitia yote ijapo yalikuwa sehemu mbili tu 

Mahusiano 

Mafanikio binafsi 

Mahusiano, hapa maswali yalikuwa mengi sana zaidi ya robo tatu yalikuwa ni maswali ya mahusiano sikushangaa sana kuulizwa maswali mengi namna hiyo kwa sababu mfumo wangu wa maisha moja ya eneo ambalo silionyeshi wazi ni mahusiano na mafanikio yangu binafsi.

Kwa sasa watu wengi hupima mahusiano ya mtu mitandaoni na ukifuatilia kurasa zangu sijawahi chapisha ( post) chapisho lolote iwe picha au maneno yenye viashiria vya mahusiano huo ni utaratibu wa mtu mwenyewe kwangu upo hivyo sina maana kuwa anayeweka wazi mitandaoni anakosea la hasha.Wengi waliuliza nitaowa lini na nitamuoa nani? 

Katika mahojiano fulani niliwahi kuzungumza kuwa siku nikitoa kitabu changu cha tatu itakuwa sambamba na harusi yangu na tayari michakato ya kutoa kitabu hicho cha jina la NTAOWA BILA UCHUMBA ipo mbioni kwa hiyo sina haja ya kusema siku bali tusubirie, nani nitamuoa?  nikijibu swali hilo itakuwa nimerudi kule kule kupost ( chapisha mirandaoni) hivyo mniwie radhi kwa hilo siku ikifika kwa mwenye kutaka kumjua atamjua. 

Sipendi sana kuweka maisha binafsi mitandaoni kwa sababu kuu mbili;

1.Maisha binafsi sio biashara niitangaze 

2.Huduma zangu mitandaoni sio kuwaambia watu ninaishije bali kuwaonyesha matokeo ya ninavyoishi ikiwemo kuhamasisha kwa kilicho ndani ya uwezo wangu 

Mafanikio binafsi,watu walitaka kujua uandishi umenipa nini mpaka sasa ni kweli nina miaka minne sasa kwenye tasnia hii na kwanza kabisa kama mafanikio kwangu ni kujiweka kwenye orodha ya watu kama msaidizi wa mafanikio yao hayo ndio mafanikio zaidi kwangu lakini pia mafanikio ya kiuchumi kwa uandishi yapo pia kwa sababu kuna kipindi nimeishi karibia mwaka sina kazi yoyote tofauti na uandishi na maisha yaliendelea,pia kupitia uandishi niliweza kununua mshamba nikalima na kiasi fulani nikaingiza kwenye ujenzi wa nyumba yangu.Nimedokeza machache na kuvunja utaratibu wangu wa kutoweka wazi maisha binafsi bali nimefanya hivyo kama hamasa kwa watu kuwa hatuapaswi kuchoka na safari 

Maisha ya uandishi ni kipaji hivyo tokea nitambue hilo nikaamua kuayapa nafasi kwangu kwa sababu kuna watu wanauliza naweza vipi ilihali nimesoma afya? Inawezekana kabisa ni suala la nidhamu tu nikiwa kwenye mambo ya afya nakuwa makini huko nikitoka mashmabulizi huamia kwenye uandishi. Uandishi nina ufanya kama sehemu ya maisha lakini miaka ya mbele itakuwa ndio shughuli yangu kuu.

Mashairi ni kipaji? Mashairi ni kipaji ijapo pia mtu anaweza kusomea hivyo kwangu ni kipaji lakini baadaye nikajiboresha huko zaidi kupitia vitabu

Kwanini riwaya ya NTAOWA BILA UCHUMBA?  hiyo ni hadithi tu ambayo nimeamua kuiandika na sina maana kuwa nitaowa bila uchumba na pengine zama zetu hizi ikawa ngumu kufanya hivyo kwa sababu inahitaji muda kukaa na mlengwa ili mufahamiane katika mbili tatu kisha ndio hatua nyingine ifuate lakini kwenye hadithi hiyo nilimaanisha  hakuna haja ya uchumba bandia .

Kila mtu anatamani kufikia eneo fulani kimafanikio na hiyo ndio chachu inayochochea upambanaji wa mtu husika kama hauko tayari kuyasaliti malengo yako lazima kila siku ujitume 


Mwanasayansi Saul Kalivubha 

0652 134707

Tuesday, 8 December 2020

WASHABIKI WA MICHEZO TUWE NA KIASI



Habari za kwako ndugu msomaji wa blogu yetu pendwa karibu tena katika safu hii tuweze kuwekana sawa katika mambo halisi ya maisha yetu ya kila siku. 


Watafiti wa takwimu wanaendelea kuja na takwimu zenye kuongezeka kila siku katika mchezo wa mpira wa miguu kuwa na washabiki wengi zaidi Duniani,unweza usiwe mshabiki wa mpira lakini utakuwa tayari umeshangazwa na taarifa kadhaa kuhusu matukio ya washabiki wa mpira  mfano kujiua, kupigana mpaka kuvunja urafiki sababu tu ya upenzi wa mpira.Zamani hayo tuliyasikia katika nchi za ulaya lakini sasa mpaka nchini kwetu tayari kuna visa kadhaa vya kushangaza kutoka kwa mashabiki wanaojiita kindakindaki. 


Nimeona vyema kuchagua eneo la mpira wa miguu kwa sababu ndiko visa vingi hutokea huko lakini upo ushabiki wa aina nyingi mfano ushabiki wa ndondi, muziki nk, ikiwa sio mshabiki wa mpira lazima kuna eneo jingine unashabikia kwani ushabiki ni moja ya hitaji la kihisia la kila mtu hivyo lazima kuna eneo tu wewe ni mpenzi. 


Ushabiki ni eneo la kihisia ambalo humpa utulivu wa kihisia mshabiki wa eneo hilo  mfano mshabiki wa timu fulani hujisikia vizuri pindi anaposikia taarifa za kupendeza kuhusu timu yake na hujisikia vibaya pindi akisikia taarifa zisizo pendeza kuhusu timu yake anayoshabikia ndio maana tunasema ushabiki ni eneo la kihisia na lenye uraibu ( addiction ) hivyo kadri unavyozidi kuwa karibu na eneo unaloshabikia ndivyo unazidi kuwa kupoteza uwezo wa kujizuia na hatimaye kufikia kiwango cha kufanya jambo lolote la kushangaza kisa ushabiki,bila shaka umewahi kusikia watu wakitembea utupu kwa sababu tu wamefunga au kufungwa.


Eneo lolote linalotawaliwa na hisia huwa linahitaji uwezo mkubwa sana wa kujizuia pia kwani maamuzi ya kihisia huwa ni ya kushangaza siku zote na ndio maana somo letu leo linasema tuwe na Kiasi kwenye ushabiki,ushabiki uwepo lakini usiathiri maisha mengine kuendelea mpaka kuvunja urafiki na undugu. 


Kuwa mshabiki kwa wakati na baada ya hapo endelea na maisha mengine ya kawaida kwa mfano ikiwa kesho timu yako inacheza  basi leo endelea na mambo yako mengine kawaida kabisa na ikifika kesho muda stahiki nenda kashabikie uwanjani,kibanda umiza au redioni na rafiki zako pengine na baada ya mchezo kuisha kaendelee na miasha yako mengine kabisa bila kuathiriwa na matokeo ya mchezo na hapo utakuwa tayari umejipa kiasi katika ushabiki. 


Kwa nini uwe na kiasi katika ushabiki ? Kama sio wewe basi utakuwa umewahi kusikia au kushuhudia mtu siku moja kabla ya timu yake kuwa uwanjani anakuwa bize na timu hiyo na kuacha shughuli zake nyingine za ki uzalishaji kwa siku nzima na kesho pia hivyo hivyo na ikitokea timu yake pengine inafungwa basi mpaka kesho kutwa yake bado atakosa msukumo wa kuendelea na shughuli zingine za ki uzalishaji,kwa hali hiyo tayari huna kiasi bali mtumwa wa ushabiki .


Malipo ya ushabiki sio pesa bali ni msawazo tu wa kihisia,ukilijua hilo nafikiri utakuwa na kiasi cha ushabiki kwani kuna maisha mengine yataendelea yanoyohitaji pesa sasa ukiacha shughuli kwa siku tatu utakuwa umepotea kiasi gani? Matajiri wengi Duniani ni washabiki wa mpira lakini utakubalina na mimi kuwa wana kiasi katika ushabiki ndio maana ukifuatilia huwa wanajitokeza au kuongea sana siku ya tukio na baada ya hapo watakuwa kimya kuendelea na maisha mengine ya ki uzalishaji pengine ikiwa ni wameajiriwa kushabikia na wanalipwa pesa ndio muda wote wote watakuwa ki ushabiki kwa sababu ndio eneo lao la ajira. 



Pengine ulianza taratibu kuwa mshabiki na sasa umefikia hatua ya uraibu kiasi cha kukosa kiasi katika ushabiki basi tambua kurudi kuwa na kiasi inawezekana pia japo sio kazi ya siku moja lakini unaweza kuanza na kanuni hii kubwa isemayo kwamba sio lazima kila mchezo uhudhuria au kuangalia ,yaani uwe na uwezo wa kuacha kufuatilia ushabiki na sio uwe na uwezo wa kuacha shughuli uende kushabikia hivyo siku michezo ukichezwa na wewe upo kibandani kwako kibiashara basi endelea na biashara bila kuathiriwa  na matokeo ya kutokwenda kwako uwanjani kwa maneno mengine ushabiki uwe ni sehemu tu na sio sehemu kamili katika maisha yako.


Makala hiii imendikwa na Saul Kalivubha,Mwanasayansi tiba katika maabara za binadamu kitaaluma na mwalimu. 


0652 134707

Wednesday, 18 November 2020

IJUE MILANGO YA CHANGAMOTO NA JINSI YA KUIFUNGA



Habari ndugu msomaji wa blogu  yetu pendwa  , karibu tena katika mwendelezo wa masomo yetu


Kama sio kila siku basi pengine haishi wiki bila kukutana na changamoto au kumsikia mtu akilalimika dhidi ya changamoto anazopambana nazo,hivi umewahi kaa chini ukajiuliza kwa nini changamoto zikuandame? .


Ni kawaida kukutwa na changamoto  haijalishi ni changamoto za aina gani lakini huwezi kuishi bila kukutana na aina yoyote ya vikwazo ( changamoto) na hii ni kwa sababu ili  tuwe watu wapya ni lazima tusafishe vikwazo vilivyo katika njia zetu la sivyo itakuwa ngumu kusonga mbele, je changamoto hupitia wapi mpaka kutufikia sisi? 


Ipo milango ya changamoto ambapo asilimia kubwa ya changamoto kupitia huko hivyo ni muhimu kujua milango hiyo ili ikiwa kuna uwezekano basi marekebisho yafanyike kuzipunguza aina hizo za changamoto, bila shaka umewahi kuandamwa na aina fulani tu ya changamoto au umewahi kusikia mtu fulani akilalimika kusumbuliwa na aina fulani tu ya changamoto hayo ni matokeo ya kuacha mlango fulani wazi wa changamoto ndio maana changamoto hujirudia za aina fulani. 



Sifa uliyonayo, una sifa gani?  yaweza kuwa cheo, uzuri, upole  , utajiri  n.k , hapo nazungumza sifa yoyote ile ya mtu uliyonayo usipojitambua na kujidhibiti lazima kuna aina fulani za changamoto zitakufuata kwa sababu ya kuwa na sifa hiyo .Upole ni sifa  na kuna watu fulani watakufanyia mambo mabaya wakijua ikiwemo kukudhulumu pesa wakijua kwa upole wako utakaa kimya hivyo na wewe ukiendekeza upole wako basi utaandamwa na changamoto za kudhulumiwa kila siku , kuna watu wakijitambua wazuri huanzisha tabia fulani ya dharau  ambapo matokeo yake ni kuandamwa na changamoto za kukimbiwa na marafiki . Sifa yoyote uliyonayo yafaa kuiidhibiti isikupe maamuzi kwani itakuwa ndio mlango wako wa changamoto. 



Ufahamu wako, Karibu kila mtu endapo angeongezewa ufahamu zaidi pengine asingefanya maamuzi anayojutia leo kumbe tunafanya maamuzi kutoksna na ufahamu wetu wa sasa  hivyo ufahamu wako ni mlango wa changamoto fulani kwako  mfano  ukiona mtu anaandamwa na changamoto kujutia maamuzi yake kuna uwezekano mkubwa akawa na shida kwenye ufahamu anaotumia kufanyia maamuzi. Jitahidi kujiongezea ufahamu wa kutosha kwenye eneo ambalo unataka kulifanyia maamuzi la sivyo utakuwa unatumia taarifa chache kutoa hitimisho na kesho ukipata taarifa nyingine ndipo unaanza kujutia kuwa hitimisho uliyofanya sio sahihi. 


Mtindo wa maisha ( life style) , karibu kila mtu ana mtindo wake wa maisha yaweza kuwa ndivyo umezaliwa hivyo au ni uchaguzi wako umefanya kuishi hivyo lakini huo ndio mtindo wako wa maisha, mtindo wako ni upi? .Nakumbuka kipindi nipo shule nilikuwa na mtindo wangu wa maisha unaotakana na asili yangu ya kuumbwa na mtindo huo ilikuwa ni kupenda kutojichanganya  na watu nilikuwa mtu wa kukaa sana peke yangu mtindo huo ulifanya nikutane na changamoto za kukosa habari nyingi ikiwemo kukosa makundi ya kufanya nao mijadala  ya kimasomo ( discussion), nilikaa chini nikaona huo mtindo wangu utafanya nifeli hivyo nikajilizamisha kuwa mtu wa jamii ( social) ili tu nipunguze changamoto za kufeli masomo kwa kukosa watu wa kujadili nao.Nimekushirikisha mtindo wangu wa maisha bila shaka utakuwa umejitafakari ukaona kuna changamoto nyingi hazikuachi kwa sababu ya mtindo wako maisha , mtindo wako maisha  ni upi ? Kuna changamoto zinakufata kwa kuvutiwa na namna unavyoishi?  Jitafakari uchukue maamuzi ya kurekebisha mtindo wako inawezekana. 


Utakubaliana na mimi kuwa kama sio sifa yako basi itakuwa mtindo wako wa maisha au ufahamu wako ndio chanzo cha aina fulani ya changamoto zilikukuta au zinazoendelea kukufuata hivyo ni kazi kwako kujifanyia mabadiliko katika maeneo hayo ili kuzipunguza changamoto za aina fulani kukufuata muda wote .


Makala hii imeandikwa na Saul Kalivubha , Mwanasayansi tiba katika maabara za binadamu na mwalimu. 


0652 134707

Monday, 26 October 2020

VITABU MLO KAMILI

 VITABU NI MLO KAMILI .


Habari ndugu msomaji wa blogu yetu pendwa na karibu katika safu hii ya kila wiki ya   vitabu na uchambuzi na leo tukiangazia  namna ambavyo vitabu ni chakula ambacho kina virutubisho vyote muhimu kwa afya ya mafanikio yetu , karibu. 


Usomaji wa vitabu ni utamaduni wa kawaida katika nchi za ulaya  lakini ni utamaduni mpya na usiopendwa na wengi katika nchi za Africa  licha ya kuwa uhamasishaji dhidi ya usomaji vitabu unazidi kukua Africa lakini wasomaji bado sio wengi  wa kuridhisha, leo naungana na wahamasishaji dhidi ya usomaji vitabu kukueleza kuwa maarifa ya vitabuni ni chakula cha ajabu sana, watalaam wa afya lishe wanahimiza kila siku kula chakula chenye karibu virutubisho vyote muhimu ili kuujenga mwili   na ili kupata mlo huo itakukagharimu  kuandaa menu yenye vyakula hivyo    kisha uende sokoni kununua na baadaye kuvipika na mwishoni kufurahia mlo huo  mezani .


Kwenye vitabu ni tofauti kidogo ndani ya kitabu kimoja mwandishi anakuwa kafanya maandalizi yeye kwa kufanya utafiti wa kutosha na kisha kukuwekea kwenye kitabu kimoja hivyo unapo kaa mezani na kitabu tayari upo kwenye mlo kamili wa maarifa  yaliyoandaliwa kwa weredi wa kutosha. Napoleon Hill mwandishi wa kitabu cha THINK AND GROW RICH  aliandika kitabu hicho miaka imepita  ( kabla ya vita ya pili ya Dunia)  lakini  bado ni mlo kamili mpaka sasa unajua kwa nini ni mlo kamili?  Maandalizi ya kuandika kitabu hicho yalifanyika kwa miaka isiyopungua ishirini kwa mwandishi kufanya mahojiano na watu mbali mbali waliofanikiwa ikiwemo mgunduzi maarufu wa bulbu Thomas Edson, unajisikaje kusoma kitabu kiliichoandaliwa kwa takribani miaka 25? tena kikiwa na mbinu za Thomas Edson ambaye hakukuta tamaa kwa kufanya majaribio zaidi ya 999 na kufanikiwa kwenye jaribio la 1000 .


Napoleon hill katupa mlo kamili kwenye kitabu chake aliyoandika miaka hiyo mpaka sasa ukiyasoma  bado ni chakula chenye virutubisho muhimu kwako, machache kati ya mengi ambayo mwandishi alijihakikishia kutoka kwa watu waliyofanya ni kutojipa ukomo wa uvumilivu  hili ni jambo muhimu sana miaka yote  kwa sababu tunashindwa kufikia malengo sio kwa sababu hatujui njia za kupita la hasha muda mwingine ni kwa sababu tunaishia njiani lakini njia ndiyo yenyewe, tunapata mbinu moja muhimu ya kutoichoka safari isemayo kabla hujakata tamaa jiambie nitafanya mara tano tena zaidi mfano umefanya biashara imekufa kabla ya kusema sitofanya tena biashara jiambie nitafanya tena mara tano zaidi nione matokeo. 


Kusoma vitabu ni tabia ya hekima  ya kujilisha kimaarifa  ambapo pishi linakuwa tayari limepikwa na mwandishi inabaki ni wewe kukaa mezani na kula chakula hicho chenye virutubisho vyote muhimu, mwandishi Napoleon hill katika kufanya utafiti wake wa kutuandalia mlo kamili  anatoa mbinu nyingine nzuri sana inayofanya kazi mpaka sasa nayo ni kuacha tabia ya kuaga kila mtu kabla ya kusafiri, mwandishi anasema unapotaka kuthubutu jambo jipya na ukataka ruhusa kutoka kwa watu wako wa karibu inawezekana idadi kubwa itakuonea huruma na hatimaye kukukataza usifanye kwa sababu ni hatari hivyo ukiwa na tabia ya kuaga kila mtu unaweza usiende uendapo kwani utakatazwa ni bora wengine waone matokeo ndio uwaambie uliwezaje , nenda kisha utarudi baadaye kuwaambia kuwa uliondoka . Thomas Edson aliweza kuthubutu mara elfu moja sio kwa sababu alikuwa na moyo mgumu wa kutokota tamaa kuliko watu wote Duniani la hasha pia hata tabia ya kutoaga kila mtu ilimsaidia wengi walikuja kuona tu matokeo.


Mwandishi bado akaendelea kutuonyesha kuwa vitabu ni mlo kamili kwa kutuletea mbinu zilizotumiwa na Henry Ford ( mwana mapinduzi katika ulimwengu wa magari) , mwandishi katika mahojiano na kampuni ya Ford hakuwa mchoyo kuziweka mbinu  wazi kwenye kitabu chake cha think and grow rich , moja ya mbinu aliyotuwekea ni  kufikiria kwa kuendana na nyakati kwa sababu sio mtu wa kwanza kugundua gari lakini alichokifanya ni ugunduzi wa gari kutokana na mahitaji ya jamii  na vipato vyao.Henry Ford alifariki mwaka 1947 lakini mpaka leo bado ujuzi wake na mfumo wake unatumiwa na watu mbalimbali wanaofanikiwa huoni kama vitabu ni mlo kamili? Mpaka sasa bado ukisoma kitabu cha think and grow rich unapata chakula ambacho hakijachachcha kutoka kwa mwandishi aliyetumia muda mrefu kukuandalia. 



Nyuma ya vitabu kuna maandalizi ya kutosha hadi kuja kukisoma wewe hivyo waandishi wanaingia gharama za kukutafutia viini lishe vyote muhimu na kukuwekea kwenye kitabu kimoja kazi ibaki kwako kula na kufanyia kazi, vitabu ni hazina na utajiri .


Makala hii imeandikwa Saul Kalivubha, Mwanasayansi tiba katika maabara za binadamu na mwalimu. 

0652 134707

JIAMBIE UKWELI UPIGE HATUA

 JIAMBIE UKWELI UPIGE HATUA 


Habari ndugu msomaji wa blogu  yetu pendwa na karibu tena katika safu hii ya kila wiki ya NASAHA ZA WIKI , leo tuna somo ambalo litafumbua macho yetu kuona hatua mpya mbele  hivyo tuambatane sote. 


Mara ya mwisho kujiambia ukweli ni lini?  Kwa uaminifu jipe majibu stahiki katika swali hilo  kwa sababu wengi tunajidanganya ndio maana leo nimekuja na somo hili ili tuone madhara ya kujidanganya na jinsi ya kuachana na tabia hiyo ya kujiadanganya .

Unapenda kudanganywa?  Jibu litakuwa hapana! sidhani kama kuna mtu hupenda kudanganywa  .Kudanganya  ni hali ya kuaminisha uongo utumike kama ukweli  mfano umelala kitandani unapigiwa simu ukiulizwa uko wapi?  Unajibu upo kazini  tayari hapo umemuaminisha uongo ya kuwa upo kazini lakini ukweli upo kitandani hivyo umemfanya mwenzako aamini ulichomuaminisha. Sifa ya uongo ni kuendelezwa hivyo ukidanganya mtu utajitahidi utafute tena mazingira ya uongo ili kuujazia nyama uongo wako uonekane ukweli  ndio maana mtu akidanganya kwa jambo moja kuna uwezekano mkubwa hata jambo la pili litalokofuata likawa sio la kweli .Bila shaka umepata picha ya uongo sasa tumeona mtu akiwa anadanganya mwingine ni vipi ukiwa unajidanganya? 

KUJIDANGANYA. 

Kujidanganya ni kutafuta usahihi kwa kuwalaumu wengine kwa makosa yako  mfano umechelewa kufika kazini hivyo ukachelewa pia kumaliza majukumu ya siku lakini  badala ujiambie ukweli kuwa tatizo ni kuchelewa ndio chanzo cha yote  wewe unajitetea kwa  kujiambia kuwa kazi zilikuwa nyingi sana hivyo kosa ni la mwajiri kukupanga peke yako kitengo hicho, tayari hapo umejidanganya kuhalalisha kuchelewa kwako kuwa sio tatizo bali tatizo ni la mwajiri. Tunajidanganya kila siku katika mambo mengi sana na hali inayofanya tujione kila siku tupo sahihi kwa 100% .

Wayajua madhara ya kujidanganya?  Moja ya dalili za kuwa mtu fulani anajidanganya ni hizi kuu mbili 

1.Kuwa na idadi kubwa ya watu ambao anawalaumu kila siku ikiwa sio watu basi atakuwa na idadi kubwa ya mazingira tofauti tofauti ya kuyalaumu mfano utasikia ni kwa sababu ya mvua, jua kali, foleni, nk na hata siku moja hutamsikia akisema ni sababu ya uvivu wake wa kuchelewa kuamka. 

2.Kuwa na changamoto zinazojirudia hii ni kutokana na sababu kuwa tatizo linakuwa ni yeye ila anajidanganya kuwa sio yeye na kwa sababu tatizo ndio mwanzo wa changamoto ndio maana changamoto za aina moja hujitokeza sana kwake mfano   mwanzo atakwambia tatizo ni pesa ndio maana hafanyi biashara lakini ukimpa pesa  tatizo atakwambia ni muda sio rafiki  na ukimpa muda wa kutosha utasikia akisema tena biashara anayotaka kuifanya sio msimu wake lakini pengine tatizo ni hofu yake au matumizi mabaya tu ya pesa  ndio maana changamoto ya kushindwa kuanzisha biashara imejirudia kila wakati. 

Dalili hizo mbili zinaonyesha wazi madhara apatayo mtu ambaye anakwepa ukweli kwa kuwajibisha wengine katika makosa yake  . Tatizo ukiwa ni wewe utalikwepa kwa kujitetea lakini matokeo ya tatizo hilo yatakurudia kila mara  hivyo utakuwa mtu wa kujitetea kila siku lakini makosa yale yale kila siku unarudia. Kujidanganya ni tabia inayofunga miguu yetu kutembea  kwa sababu huwezi kuendelea mbele ilihali bado hujatatua tatizo linalofanya miguu iwe mizito.  Mfano ukiwa unaendesha gari  betri ikapata shida taa zikazima  badala ya kushughurikia betri ipone wewe ukaamua utafute barabara mbazo zinataa za bararani ndio upite  hapo utakuwa unakwepa ukweli na tatizo litabaki palepale kwa sababu taa za barabarani zikizima na zenyewe? 

JIAMBIE UKWELI. Kila kwenye changamoto wewe tafuta uhusika wako uliofanya changamoto hiyo itokee kisha anza kupambana na tabia hiyo yako. Moja ya mbinu nzuri za kutumia ili uwe unajiambia ukweli ni kutafuta  muda wa tathmini binafsi  ikiwezekana kila wiki au kila mwezi au kila siku ni wewe tu jiwekee ratiba zako , katika kujitathmini huko binafsi   angalia changamoto unazokumbana nazo kwa siku/wiki/mwezi nk na jiulize kwa nini zinatokea na kuendelea kisha orodhesha sababu za kimazingira zinazopelekea changamoto hizo zitokee na orodhesha sababu kutoka kwako namna gani unachangia changamoto hizo zitokee kisha anza kujidhibiti na kujitibu na kama ikiwa ngumu kujitibu peke yako basi tafuta watalaamu wakusaisie.

Makala hii imeandikwa na Saul Kalivubha Mwanasayansi tiba katika maabara za binadamu na mwalimu. 


+255652 134707



Saturday, 17 October 2020

TIBA YA HISIA ZILIZOJERUHIWA

 TIBA YA HISIA ZILIZOJERUHIWA. 


Habari ndugu msomaji wa blugu yetu pendwa ya fikiandotozako , leo tuna somo ambalo nina hakika litakuwa tiba kwa wahanga wengi  hivyo twende sambamba. 


HISIA ni msukumo ambao unahitaji kutimilizwa , mfano  mtu ukiwa na hisia za kupenda utafurahi ukipendwa, ukiwa na hisia za hasira utataka ufanye jambo fulani kuimaliza hasira n.k, sasa tunapata picha kuwa kila kwenye hisia kuna jambo litatakiwa kufanywa ili kutimiliza lengo la hisia.Tuangalie kisa  hiki ambapo najua kwa namna moja au nyingine utakuwa umewahi kuwa muhanga, mmepanga kukutana na rafiki yako mnayependana kweli   mara ghafla siku moja kabla anakutumia ujumbe kuwa hatoweza kuja tena siku hiyo kapatwa na dharura  hivyo mpaka siku nyingine kama wewe utajisikiaje? Kwa jibu la haraka utajisikia vibaya na sababu kubwa sio kuwa kakupotezea muda kama wengi wanavyodai la hasha ni kwa sababu ujio wake kwako ulikuwa ni tiba ya hisia fulani ambazo tayari zilikupanda pale tu mlipokubaliana  kukutana  tena kibaya zaidi mkiwa mna mahusiano ya kimapenzi ndio utatumia zaidi  kwa sababu kajeruhi hisia zako. 


KUJERUHIWA KWA HISIA. 

Tumeona kuwa kila kwenye hisia kuna jambo linatakiwa hivyo lisipofanyika basi hisia zako zitakuwa zimejeruhiwa. Jeraha la kuhisia ( psychological trauma)   linatofautiana ukubwa kutokana na aina ya hisia iliyojeruhiwa  mfano hasira uliyonayo dhidi ya mtu unayemdai na unataka uonane naye umwambie bayana endapo hutaonana naye utaumia lakini muda sio mrefu jeraha lake litapona utaendelea na maisha lakini hisia za kupenda ikitokea umempenda mtu  lakini mwenzako akawa msaliti na mwisho mkavunja uhusiano hilo jeraha lake  kupona sio rahisi na litakuathiri sana kama utakosa mbinu za kujitibu.


TIBA YA HISIA ZILIZOJERUHIWA. 


Bila shaka umewahi kuona watu wakiwa na tabia mpya punde tu baada ya kukutwa na maswaibu fulani, ulevi, wizi, uhuni , kuchelewa kuoa/kuolewa kwa kutoamini tena mahusiano  n.k, hayo ni moja ya matokeo ya kushindwa kujitibu majeraha ya hisia zilizojeruhiwa au  kujitibu kwa mbinu zisizo sahihi  kwa sababu baada ya hisia kujeruhiwa  kinachofuata  ni muhusika kutafuta tabia mpya itakayomsaidia kusahau maumivu  sasa hapo ndipo kuna tatizo  wengi huchagua tabia ambayo ndio badala ya kuwatibu ndio inawakandamiza zaidi mfano baada ya mtu kuachwa kwenye mahusiano anaamua kutokuwa tena muaminifu au kutowaamini tena watu tabia ambayo inamfanya aendelee kuteseka kwa sababu ataachwa tena kwa kukosa uaminifu. 


Hisia zinapojeruhiwa jitahidi ukubali kwanza hali  na pia katika machaguzi ya tabia mpya itayokufanya ujione sawa usichague vilevi  na wala usichague kulipiza kisasi bali chagua kujiboresha zaidi ili hata ikitokea tena basi sababu nyingi zisilalie kwako , fuata hatua hizi :


1.ikubali hali. 

2.Usianzishe tabia za kujisaulisha kwa muda  mfano kuanza ulevi n.k,bali tafuta tabia itayokuboresha zaidi 

3. Jipe muda mrefu wa kujiboresha ukiwa bora itakujengea kujiamini. 

4.Ukiridhika kuwa umejiboresha sasa unaweza kuendelea na maisha mengine na ukiweza epuka vichocheo vitavyokufanya ukumbuke namna ulivyojeruhiwa kihisia.


Makala hii imeandikwa na Saul Kalivubha ambaye ni Mwanasayansi tiba katika maabara za binadamu na mwalimu. 

0652 134707