ELIMU YA KUJIAJIRI IFUNDISHWE MASHULENI
Katika karne hii ya 21 suala la mtu kumaliza shule na kukosa ajira sasa sio geni tena kwa sababu ongezeko la wakosa ajira limekuwa kubwa sana na sababu inaweza isiwe moja tu serikali kushindwa kuajiri wasomi wake wote bali hata mfumo wa maisha wa sasa umebadilika mbali na kuwa wimbi la wasomi linaongezeka kila siku lakini pia ajira za watu sasa zinachukuliwa na mapinduzi ya kiteknolojia mfano zamani ilitakiwa watu waajiriwe kukata tiketi lakini sasa tiketi zinakatwa na mashine hivyo anatakiwa mtu mmoja tu kuisimamia hiyo mashine.
Baadhi ya viongozi hasa wana siasa wamekuwa wakihimiza suala la wahitimu wa vyuo vikuu kujiajiri pindi wamalizapo masomo yao na wasitegemee kuajiriwa na serikali na mwisho wa siku kosa inaonekana ni la uvivu wa muhitimu kushindwa kujiajiri lakini ki uhalisia sio kweli kwa sababu ni rahisi kumwambia mtu ajiajiri lakini kwa muhitimu wa chuo kikuu sio rahisi kwake kwa sababu zaidi ya miaka kumi darasani anaandaliwa kuajiriwa wafikiri siku moja tu itambadili mtizamo aliojengewa kwa miaka kumi? Serikali iweke mfumo wa mwanafunzi tokea shule ya msingi mpaka chuo kikuu hapo mazingira angalau yatakuwa rafiki kujiajiri kwa sababu msingi utakuwa umemjenga, kwa mfano mtu kamaliza taaluma yake ya ualimu kaandaliwa kufundisha sasa akimaliza ajiajiri vipi? afungue kituo cha kufundisha masomo kwa ziada ( tuition) napo nado ni changamoto kwa sababu sasa serikali inahimiza wanafunzi wamakinike zaidi na darasani na sio kwenye vituo vya kufundisha masomo kwa ziada hivyo inakuwa ngumu kutumia taaluma kujiajiri na kujiajiri kwenye mambo mengine nje ya taaluma ndio hayo ambayo mwanafunzi hakupewa misingi tokea mapema.
Serikali kupitia mitaala ya elimu iweke masomo ya kufundisha maisha nje ya taaluma kwa nadharia na vitendo kwa mfano kuwepo na somo la maisha na kujitegemea ambapo hapo mwanafunzi afundishwe stadi mbali mbali za kuyakabili mazingira tofauti na ile taaluma yake kwa mfano kama ni mwalimu afundishe ni namna gani anaweza kuyakabili mazingira bila kuwa na ajira hivyo apewe stadi hizo kama mbinu za kuanzisha biashara ndogo ndogo na namna ya kuikuza biashara hiyo na mwisho wa siku apewe mtihani wa vitendo kwa kuendesha mradi wa shule au kuleta ubunifu wa mradi hii itasaidia sana kumfanya mwanafunzi azoee mazingira mapema.
Wanafunzi wengi bado wanaamini kujiajiri ni umaskini ndio maana wengi wao hilo wazo la kujiajiri hata hawalifikirii na sio makosa yao kuwaza hivyo ni kwa sababu darasani hawakuambiwa ukweli kuwa kuna kukosa ajira na kuishi maisha nje ya ajira ndio maana kila muhitimu kilio chake ni kupata ajira, kuna uwezekano mkubwa wahitimu wakipewa hata mitaji wengi watashindwa kujitegemea kibiashara kwa sababu elimu ya kujitegemea haikufundishwa darasani ni tofauti na mtu ambaye hakuendelea na masomo tayari akili yake aliiandaa kuwa hakuna namna anaweza kuishi bila kujiajiri mwenyewe hivyo anamakinika zaidi na mwisho wa siku anakuwa na elimu nzuri ya kujitegemea.
Serikali iweke ukweli kwa wanafunzi mapema kuwa kuajiriwa sasa ni bahati ya wachache na tena kwa baadhi ya kada na iziweke wazi kada hizo na kwa kada zile ambazo ajira zake hazitoki sana basi zipunguziwe udahili vyuoni wachukuliwe wachache ili kuepusha mlindikano wa wahitimu wasio na ajira mtaani. Suala la kujiajiri kwa sasa inatikiwa iwe ni kama kampeni kwa wanafunzi kwa sababu hali ya wahitimu sio rafiki sana mtaani bado kuna umuhimu wa serikali kuingilia kati kwa kubadili mitaala ya elimu
Mwanasayansi Saul Kalivubha
+255652 134707
No comments:
Post a Comment