Saturday, 14 January 2023

 HIZI NDIO SABABU ZINAZOFANYA UWE MTU WA KUJUTIA MAAMUZI YAKO

 HIZI NDIO SABABU ZINAZOFANYA UWE MTU WA KUJUTIA MAAMUZI YAKO 


Na Mwanasayansi Saul Kalivubha ✍ 


Ulijawa na furaha siku hiyo na hata kama angetokea mtu wa kukwambia kuwa unachotaka kufanya ni hatari pengine ungemuona ni adui asiyependa mafanikio yako lakini furaha yako leo haipo tena 😞 Unajutia  maamuzi yale .Kwa nini umekuwa mtu wa kujutia maamuzi yako ? Na ilihali jana ulijiona upo sahihi kwa maamuzi hayo? Twende darasani. 

Maamuzi ni eneo muhimu sana kwenye maisha yetu kwa sababu maamuzi ndio miguu yetu ya kutembelea , upo hapo ulipo leo  kwa sababu kuna maamuzi uliyafanya jana na hata hao unaowashangaa leo wapo hivyo kwa sababu kuna maamuzi waliyafanya jana .

Kujutia sio kitu kigeni kwa sababu karibu kila mtu ana siku moja au zaidi za kujutia maamuzi yake, hakuna ambaye hajawahi kujutia katika maisha yake lakini wapo watu ambao kwao ni zaidi yaani kwenye maamuzi kumi waliyofanya basi   zaidi ya maamuzi matano kwao sio sahihi ni lazima wayajutie.

Kwa nini leo ujione umekosea na wakati jana ulijiona sahihi kwa maamuzi yale yale?  Yapo mambo mengi ambayo yanachangia hali hiyo kutokea  na vizuri uyafahamu mambo hayo ili ujue namna ya kupunguza majuto , na kama unakuwa mwingi wa majuto kuna uwezekano mkubwa ukawa ni mtu ambaye huna furaha kwenye maisha yako kwa sababu unakuwa unafikiria  yaliyopita tu .

Ufahamu wako wakati wa maamuzi ni sababu kubwa sana ya majuto kwa wengi, wajua ni kwa sababu gani? Ni kwa sababu kinachofanya uamue ni Ufahamu wako wa muda huo hivyo kama ufahahamu wako ni mdogo sana basi hata maamuzi yako kwa asilimia kubwa  yatakuwa sio bora pia na siku ufahahamu wako ukikua ni lazima utaona kuwa ulikosea maamuzi . Tunajutia maamuzi yetu ya jana kwa sababu tuliyafanya tukiwa na ufahahamu mdogo tofauti na leo tulivyo kwa mfano  kama jana ulifanya maamuzi ya kuacha shule kwa ufahahamu kuwa shule inakupotezea muda  ni bora ufanye biashara lakini ulipoanza biashara ukakutana na changamoto zikakumbusha kuwa kuna kiwango cha elimu kinatakiwa ili uweze kuimudu hiyo biashara na hapo ndipo utaaanza kujiona ulikurupuka kwenye maamuzi. 

Matokeo ya maamuzi yetu tuliyoyafanya jana ndio yanasema na sisi leo kutu onyesha ni jinsi gani tulikosea/kupatia  kwenye maamuzi yetu hayo , kuna kanuni moja ya kimaamuzi inasema kuwa kila maamuzi uliofanya ni lazima matokeo yake yaje kusema na wewe siku moja na hapo ndipo utagundua ni jinsi gani ulikuwa sahihi. Matokeo hufanya watu tujifahamu vizuri tukoje na kama utakuwa mtu chanya basi utatumia matokeo hayo kujifunza. 

Mihemko pia ni sababu nyingine inayofanya tukosee maamuzi kwa sababu maamuzi yako yatakuwa ni matokeo ya hisia za muda mfupi tu zisizo na fikra ndani yake ndio maana unashauriwa kuwa na utulivu kabla ya maamuzi japo kuna maamuzi mengine ni lazima tuyafanye kwa haraka kulingana na uhitaji wake lakini hayo ni kama dharura  tu ila maamuzi mengi lazima kuna muda utapata wa kufikiria hivyo kabla hujaamua jitahidi huna mihemko . Mihemko mara nyingi chanzo chake ni kukosa utulivu na muda mwingine kuchochewa na mazingira ya nje ikiwemo kuishi kwa kujilinganisha sana. Ukiishi kwa kujilinganisha utakuwa mtu wa kujiona umechelewa kwenye maisha na mwishowe utaanza kufanya vitu bila utulivu .

Kushindwa kuitawala shauku yako pia ni sababu inayoweza kukufanya ukosee maamuzi kwa sababu utakuwa mtu wa kukurupukia mambo kabla ya wakati wake ili tu ukidhi shauku yako Maamuzi yako Hayawezi kuwa sahihi kama unayafanya kwa shauku ambayo haikudhibitiwa .

Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul Kalivubha 

Mitandaoni tunapatikana kwa jina la fikiandotozako. 

Pia kitabu cha namna ya kudhibiti mwili kinapatikana kwa soft copy Tsh 3000 

+255652134707

No comments:

Post a Comment