Tuesday, 25 August 2026

NAJUTA KUMPELELEZA MCHUMBA WANGU FACEBOOK 1

 

SEHEMU YA KWANZA “NAPOKEA FRIEND REQUEST”

Ilikuwa Jumapili nikiwa nimetoka ibadani nimetulia tu kitandani kusaka utulivu wa nafsi, masaa sikuwa nayakumbuka vizuri ila nachokumbuka tu ni kwamba nilikuwa kitandani nimejilaza ili nipumzike, katika kupumzika akili ikaniambia, "Peruza kidogo mitandaoni upate starehe."

Nikaanza na na Facebook, Bila kufikiria sana nikaona ombi la urafiki mpya Jina lilikuwa Koku Muganizi. Sikufanya upekuzi wowote kwa sababu ilikuwa si jambo jipya kukubali maombi kama yale hivyo haraka tu nikaibonyeza "kubali" na kuendelea na maisha yangu.

Baada ya dakika chache alama ya meseji ikaonekana, nilipoingia nilikuta jumbe 3 kutoka kwa huyo rafiki mpya:

"Mambo"

"Asante kunikubalia urafiki"

"Nimefurahi kuwa sehemu yako"

Kama mwanaume, ukipata ujumbe kutoka kwa jinsia ya kike moyo unakuwa mwepesi hivyo bila ajizi niliingia haraka kwenye profile yake nikakuta picha tatu tu za binti mtulivu, mstaarabu na mzuri.

Tukaanza kuzungumza kidogo kidogo lakini kitu kimoja kilinisumbua kichwani nacho ni jina lake halikunipa uhakika kwamba ni msichana kweli maana zama za leo utapeli ni mwingi sana hivyo nikaamua kumpima kwa utani ili kuthibitisha 

Mimi: "Yaonekana wewe ni msichana mtulivu sana" 

Yeye: "Kawaida tu hata wewe pia ni kijana mtulivu."

Jibu lake lilikuwa la haraka sana likafanya nikose la kusema zaidi.

Niliamka kwenda chooni, niliporudi nilishangaa kupata meseji yake kwenye WhatsApp na ilikuwa ni yeye yule yule wa Facebook, Moyoni nilisema, "Labda kachukua namba yangu mahali."Lakini kilichonifanya nisimame ni kitu kingine. Alikuwa ananiita kwa majina yangu yote matatu ya kuzaliwa.  Tatizo ni kwamba Facebook yangu ina majina mawili tu hilo la tatu nililificha, Sasa alilijulia wapi?

Sikumuuliza bali niliijaribu kujipa majibu yangu mwenyewe. "Labda Facebook inaongeza kiotomatiki."

 

Tulizidi kuwasliana mpaka kupeana historia zetu na hapo ndipo tukagundua kuwa tunatoka mkoa mmoja ingawa wilaya zetu ni tofauti yeye alikuwa Bukoba na mimi Muleba, Unajua furaha ya kukutana na mtu wa nyumbani nje ya nyumbani? Inaleta utamu tofauti kabisa.

Siku chache tu, tulikuwa tayari tumeshaingia kwenye mahusiano na wote tulikuwa w mbali na nyumbani, yeye kikazi na mimi pia lakini alinihakikishia kitu kimoja kuwa atakapokuwa na nafasi nitapita kukusalimia maana wote tulikuwa Dar es salaam. Maneno hayo kwa mwanaume ni kama mafuta kwenye moto hakuana asiyependa kutembelewa na msichana.

Siku moja akaniuliza: 

"Unajua tarehe 12 Mwezi wa Sita ni siku yangu ya kumbukizi kuzaliwa?"

Nilijibu kwa furaha: "Nitakutumia kitu hata kama ni zawadi ndogo na kama tutaonana tutasheherekea pamoja" 

Akanijibu: "HAPANA SHAKA. KUNA SIKU ITATUKUTA PAMOJA." Japo tulikuwa pamoja Dar ila sikutaka kuonekana ninaharakisha sana kuoanana naye, Japo ndani yangu kulikuwa na swali moja linaninyima usingizi: Alipata wapi namba yangu? Na alijua vipi jina langu la tatu?

Nikaamua kufanya upelelezi wangu mdogo, nikaangalia kama tunachangia marafiki na kweli, nilimkuta ana rafiki mmoja tuliyesomea naye hapo moyo ukatulia kidogo. Lakini kabla sijapumua, akanitumia ujumbe: 

"Mbona unaonekana una hofu?"            

Nikajibu: "Sina hofu." 

Akarudi tena: "Nafahamu una hofu ya wapi nimepata mawasiliano yako ni rafiki zako. Ndio wamenipa namba yako na majina yako yote."

Damu yangu iliganda, kafahamu vipi kuwa nilikuwa na hofu? Nikaamua kuwapigia wale marafiki zangu na wote walinipa jibu moja:  "Tunamjua tu Facebook ila hatujawahi kuzungumza naye" Nikiwa bado kwenye mshtuko huo, ndipo ujumbe wake mpya ukaingia:  "Wale rafiki niliokwambia sio hawa wa Facebook."

Hapo ndipo hofu yangu ilipanda kilele, Huyu mtu ni nani? Nilijaribu kujituliza. "Labda ni mtu tu aliyenifahamu barabarani akampa taarifa zangu."

Tarehe 12 Juni ilifika ambayo ni siku ya kumbukumbu yake ya kuzaliwa na asubuhi nilimtumia ujumbe wa kumpongeza na kumuahidi kumtumia pesa anunue hata soda., Alifurahi. Baadaye mchana Facebook ilinijulisha: "Leo ni siku ya kuzaliwa kwa Koku Muganizi."  Niliingia kwenye ukurasa wake na picha yake ilikuwa nzuri sana hata kwenye sehemu ya maoni watu wengi walikuwa wakimiminika kumtakia heri ya kuzaliwa japo sikufanikiwa kusoma ila niliamini hivyo. Nilijaribu kusoma sasa maoni lakini hayakufunguka, Nikajaribu kuandika yangu ya kumtakia heri nayo yakakataa nikasema, "Labda ni mtandao."

Akanitumia ujumbe: "Leo Facebook yangu haiko sawa." 

Nami nikakubaliana naye lakini akaniambia, "Jaribu tena."

Niliporudi, mwisho maoni yalifunguka nikapiga hatua kuteremka ili nione ni nani kamtakia heri. niliwaza, kama ana mchumba lazima nimpate hapa kisha nikakutana na maoni ambayo yalibadilisha kila kitu kwenye fikra zangu kwanza maoni mengi yalikuwa kwa lugha nisiyoelewa. labda ni lugha ya kwao, nikajidanganya pili nikaona lipo moja kwa Kiswahili hapo Roho yangu ikatetemeka.

Lilisomeka hivi: 

"Vipi mbona msimu huu umetucheleweshea Damu?"

Naye akajibu: 

"Punde tu mtapata. Si mnajua ugumu ulivyo sasa kuipata?"

Damu?

 Malenga wa Kiha

 Mwanasayansi Saul Kalivubha

 255652134707

Saturday, 3 January 2026

HII KAULI YA " KAMA NI WAKO BASI ATAKUWA" IMEHARIBU WENGI WANAOITAFASIRI NDIVYO SIVYO.

Hii kauli imefanya watu washindwe kujitafajari pale wanapopoteza kwa kujifariji kuwa HAIKUWA RIDHIKI .

Inaweza kuwa ni ridhiki yako ndio lakini ukaipoteza kwa ujinga au tabia zako na kwa sababu ya hiyo faraja unayoijipa  unabaki kuamini tu kama ni chako kitakuwa na kama sivyo kitaondoka lakini swali ni je hata kama ni CHAKO KITAKAA KWENYE TABIA ZISIZO RAFIKI?

Wengi hutafasiri kuwa  kwa sababu tu ulipangiwa basi wewe huna mambo ya kufanya ili kufanya hayo mambo yaje na kudumu kwako badala yake unabweteka ukisubiri tu sasa kwa namna hiyo UTASUBIRI SANA BILA MAFANIKIO.

Ukisoma ajira hazikutafuti bali wewe ndio unatakiwa uzitafute .

Mchumba sahihi atakaa kwako ikiwa tu umeweka mazingira rafiki kwake la sivyo watakuja na kuondoka nawe utabakia tu kujifariji kuwa KISICHORIDHIKI HAKIKAI 


#Mwanasayansi Saul kalivubha 

#Fikia Ndoto Zako

Monday, 6 October 2025

MAMBO YA KUFANYA ILI KUVUKA KIPINDI CHA KUKATALIWA BILA WEWE KUDHURIKA

Kukataliwa sio kitu kigeni kwa sababu uzoefu unaonyesha karibu kila mtu ameshaonja kipindi hiki na hata kama bado basi kuna siku utakipitia .

Inaweza kuwa ndugu, marafiki, makazini au katika mahusiano kote kuna kakataliwa .

Ni kipindi kigumu sana kukabiliana nacho kwa sababu ki asili binadamu tunapenda kukubaliwa hivyo ianapotokea kukataliwa maumivu yake huwa ni makali sana bila kuwa na  ukomavu athari huwa kubwa ikiwemo na kujitoa/kutoa uhai .

UFANYEJE SASA UKIWA KWENYE KIPINDI HICHO?

1.Kubali ukweli (Ukiruka hii hatua utakuwa unajidanganya kuwa uko sawa ila ki uhalisia bado unateseka hivyo lazima ukubali kuwa HAKUTAKI)

2.Ondoa matumaini kuwa kuna siku ATAJIRUDI ( Usiwe na hayo matumaini kwa kuamini ipo siku atajirudi ukaanza kuwa unamtumia meseji mara unamjulia hali au kuendelea kumshirikisha mambo yako kwa tumaini kuwa atakuonea huruma arudi , utateseka)

3.Usitake umsahau kwa kutafuta mbadala wake( kosa kubwa sana hili )

4.Wekeza nguvu kwenye mambo mengine na futa matukio ambayo yatafanya umkumbuke ikiwemo picha kama mlipiga wote au kusikia nyimbo ambazo mlizipenda kwa pamoja)

5.Usijione mwenye kasoro za kukataliwa ( usianze kutafuta sababu za kujiona hufai)

6.Usianzishe maigizo ya kuaminisha watu kuwa upo sawa na soko lako lipo juu 

7.Muda ndio kidonge cha mwisho kumaliza maumivu yako( Huwezi kuwa sawa kesho itachukua muda hivyo kubali hilo)

8.SHUKURU MUNGU KUKATALIWA KWA SABABU KUNA SEHEMU KAKUANDALIA YA KUKUBALIWA 🙏 


NB : KUCHELEWA KUKUBALI KUKATALIWA NI KUENDELEA KUJICHELEWESHA WEWE MWENYEWE 😔 

#Mwanasayansi Saul kalivubha 

#Fikia Ndoto Zako 

+255652 134707

Thursday, 26 June 2025

UTULIVU NI JICHO LA TATU KUKUPA MAAMUZI SAHIHI HASA KWENYE NYAKATI ZA KUVURUGWA

 

Walioachwa kwenye mahusiano wakakurupukia mengine haraka wakiwa kwenye hali ya  kuvurugwa wengi  wao walijikuta wakikosea tena vibaya zaidi ya mwanzo.

Waliofumania wenzi wao au kusikia taarifa mbaya dhidi ya wenzi wao na wakafanya maamuzi wakiwa kwenye hali ya kuvurugwa wengi walijikuta kwenye maamuzi mabaya na yenye majuto kama vile kuua au kujiua.

Waliojibizana wakiwa kwenye hali ya kuvurugwa wengi walijikuta wakiongea maneno ya hovyo na yaliyokosa hekima kiasi cha kujipotezea heshima. 


Furaha na huzuni vyote vinaweza kupoteza utulivu wako na utulivu ukipotea basi tarajia maamuzi ya hovyo kwa asilimia kubwa. 

Adui wabobevu wanalijua hilo ndio maana wakitaka kukushambulia kirahisi basi watatafuta namna ya kukuvuruga na kukushinikiza ufanye maamuzi ukiwa kwenye huo mvurogo wakiamini ni lazima utakosea tu.

Utulivu ndio silaha pekee kwenye nyakati kama hizo na hapo utapata jicho la tatu la kuona hali halisi na maamuzi gani uchukue .

#Mwanasayansi Saul kalivubha 

#Fikia Ndoto Zako

#Mitandaoni @Fikia Ndoto Zako 

Wednesday, 14 August 2024

UKIZALIWA FAMILIA MASKINI JUA TAYARI UMEKUWA JESHI LA MTU MMOJA MSITUNI

 UKIZALIWA FAMILIA MASKINI JUA TAYARI UMEKUWA JESHI LA MTU MMOJA MSITUNI, ACHA KUDEKA. 

Maisha hayako sawa hilo lazima tukubali   na usipolikubali basi utashindwa kupambana kulingana na mwanzo wako ulivyo , Kwa mfano kuna kuna ambao wanarithishwa mali waendeleze na kuna wanaorithishwa matatizo wayatatue.

Kuna ambaye akipata kazi tu hupongezwa kwa kupewa  kiwanja cha nyumba ama fungu la pesa na kuna wewe ambaye ukipata kazi tu matatizo yanaongezeka yaani utatakiwa ujengee wazazi, usomeshe watoto wa ndugu zako na kisha ndio uanze kujiimarisha .

Wewe ambaye simu zote unazopigiwa ni za matatizo usijilinganishe na ambaye hupigiwa simu kwa kukumbukwa, Wewe ni jeshi la mtu mmoja tayari hivyo usitegemee msaada wowote wa kivita kutoka nyuma wala mbele hivyo ni kupambana tu mpaka kieleweke .

Mambo ya kudeka waachie wenyewe ila wewe tambua ukifeli ndugu zako wataumia zaidi kuliko hata wewe muhusika kwa sababu umebeba matumaini ya wengine .

Kila siku historia ya ulipotoka iwe inakukumbusha kuwa WEWE NI JESHI LA MTU MMOJA MSITUNI. 

#Mwanasayansi Saul kalivubha.

#Fikia Ndoto zako 

+255652 134707

Thursday, 1 August 2024

MASKINI ATABAKI KUWA MASKINI TU KAMA ATAENDELEA KUWA NA MARAFIKI MASKINI 😔

 MASKINI ATABAKI KUWA MASKINI TU KAMA ATAENDELEA KUWA NA MARAFIKI MASKINI 😔


Hii sio makala nzuri kwa maskini ambao wameridhika na hali hiyo  hivyo kama umeridhika na umaskini basi acha kabisa kusoma ila kama upo kwenye vita ya kujikwamua kama mimi basi inawezekana ikawa makala yenye mwanzo mpya kwako. 

Ukipokea simu kutoka kwa maskini iwe ni ukoo wako au rafiki zako huko kijijini kama sio ya kukuomba pesa basi itakuwa ya majungu tu, mtaongea majungu kisha mtaagana na baada ya hapo kila mmoja atabaki anatafakari hayo majungu mpaka usiku utafika mtalala na siku itakuwa imeisha hivyo , kweli hapo umaskini utaisha?


Ajabu ni kuwa huyo aliyekupigia simu kwa zaidi ya nusu akikupa majungu siku ikitokea fursa inayohitaji mtu wa sifa yako hatokupa na siku ukijua ukamuuliza atakwambia hakuwa na salio ( vocha ) siku hiyo , Inashangaza na kuchekesha kidogo .



Umaskini ukiwa damuni huwa wahusika wanapendana wakiwa na umaskini wao ila wana wivu mkali siku wakisikia una mipango ya kutaka kuagana na umaskini.

Ukitaka kujua hilo wapelelee habari nzuri maskini rafiki zako utachopkea kwa asilimia kubwa ni kukatishwa tu tamaa kwa kupewa mifano ya watu waliokuwa kama wewe ila wanashindwa na na huo ni ujumbe kwako kuwa achana na mipango hiyo na kwa sababu unaogopa usiwapoteze marafiki zako basi unaamua kuwasikiliza na kughairi harakati zako za kuagana na umaskini. 

Waepuke maskini wa namna hiyo kwa kila hali , hili haliwezekani kwa maskini wanaopenda kuwa maskini ila ni rahisi kwa maskini ambao wapo kwenye harakati za kujikomboa ndio maana awali nilikatunguliza hii makala haiwahusu maskini walioridhika kwa umaskini wao.

KWANINI UWAEPUKE MASKINI?

Kwa sababu wengi wao ( sio wote) watakuwa wanakujaza majungu tu na sio kukupa fursa( njia za kujikwamua)  na usipokuwa makini watakufanyia kitu kibaya endapo wakijua una mipango mizuri ya kuwa tajiri.


Mwanasayansi Saul kalivubha 

Instagram @fikia ndoto zako 

+255652 134707

Thursday, 11 July 2024

HII NDIO KANUNI YA KIJASUSI YA KUISHI NA WATU AMBAO HAWATAKI KUONA WENGINE WAKIFANIKIWA

 KIJASUSI WAPE USHINDI WALEWE ILI WAACHE KUKUFUATILIA BALI WASHANGAZWE KWA MATOKEO.


Jasusi yoyote Duniani huwa habishani na mtu zaidi atakubaliana na wewe ili uvimbe kichwa lakini moyoni mwake hajakubali na kitachokushangaza ni matokeo. 

Hii ni mbinu moja wapo ya kuishi na watu ambao hawataki wengine wafanikiwe kwa kujiona wao ndio wanajua kila kitu , ukisema ujionyeshe ni zaidi yao kwa maneno watakufuatilia sana ili kuzima harakati zako hivyo wewe wape ushindi tu .

Sifa kubwa ya wajuaji kama hao huwa wanapenda sana sifa na kuonekana wao ni zaidi ya yeyote na siri kubwa kuhusu watu hawa huwa wanalewa sifa yaani wakipewa sifa tu tayari wanajisahau hivyo tumia madhaifu haya kuishi nao.

Ukiwapa ushindi watakuona wewe ni bwana mdogo tu na hata siku moja hutokuwa juu sasa kipindi wanashangalia kwa kukuona hivyo wewe pambana kwani hawatakuwa na umakini kwako wakijua tu wewe ni wa kushindwa.

Wakikwambia wao ndio wa mjini na hakuna wa kuwashnda wewe wakubalie kuwa ni kweli wapo hivyo ila ki uhalisia unawaona kabisa hawana lolote ila majigambo tu na huo utakuwa muda mzuri sana kufanya vitu vikubwa bila wao kukufuatilia.

Kwanini hawakufuatilii? Kwa sababu umwapa ushindi hivyo wanajiona washindi na kukuona wa kushindwa tu, Tumia huo muda vizuri. 


#Mwanasayansi Saul kalivubha 

#Fikia Ndoto zako 

+255652 134707

Thursday, 4 July 2024

UKIMILIKI PESA UMEMILIKI HISIA ZA KUJIAMINI NA UKIKOSA BASI UMEPOTEZA SEHEMU YA KUJIAMINI.

 UKIMILIKI PESA UMEMILIKI HISIA ZA KUJIAMINI NA UKIKOSA BASI UMEPOTEZA SEHEMU YA KUJIAMINI.

Linapokuja suala la umiliki wa pesa basi tunazungumzia hisia ziletwazo  na pesa ambavyo kwa namna yoyote unatakiwa hisia hizo zisikushinde bali uzitawale.Wengi hatutafuti pesa kama zilivyo karatasi bali tunatafuta ile hisia ambayo mtu anakuwa nayo akiwa na pesa ndio maana leo hii mtu akiwa na pesa kuna namna atajihisi hata akivaa hovyo hatahisi aibu kwa sababu anajua mtaona kaamua kufanya hivyo ila mtu akikosa pesa kitu cha haraka atachohisi ni aibu na hata kutamka mbele za watu kuwa hana pesa anaweza kushindwa kwa aibu .

Hisia kubwa ileteayo na pesa ni kujiamini na hapo ndipo inatakiwa mtu uwe na nguvu kubwa kuliko hisia itokanayo na pesa bila kujali una pesa ama huna.

Kwa sababu hisia ya kuwa na pesa ikikupa maamuzi ndio utaanza kufanya mambo ya kushangaza na sio kwamba ni mazuri bali ya hovyo kwani utakuwa mtumwa wa pesa.

Vipo viashiria vingi kuwa mtu fulani ni mtumwa pesa na hasa tunaangalia matumizi yake na matendo afanyayo muhusika kama vile:

Ulimbukeni kwenye starehe ambapo muhusika utamuona akitumia pesa bila kuinoea huruma pesa.

Kuanzisha vurugu zisizo na lazima ilimradi tu ujulikane kuwa chanzo ni wewe na tena kwa sababu tu una pesa.

Kuanzisha vitendo vya hovyo kama vile dhuluma kwa wanyonge kwa kutumia nguvu ya pesa ukiwa unasmini hata utatumia pesa kununua haki kama ikitokea unashitaakiwa.

Kibaya zaidi ukiongozwa ba hisia za pesa utakuwa na siku za kuhesabika kwenye umiliki wa pesa kwa sababu utakuwa mwenye matumizi mengi yasiyo na lazima na huo ndio utakuwa mwanzo wa kufilisika 

Je inakuwaje kwa mtu ambaye hana pesa? Kukosa pesa ni mwanzo wa kupoteza hisia za kujiamini na hapo utaingiwa na tatizo la kujishtukia kwa mambo ambayo hata hayapo kama vile:

Usiposalimiwa unahisi ni sababu huna pesa ndio maana hata baadhi ya watu hawakupi salaam zao lakini inawezekana tu hawakusalimii kwa sababu zao binafsi na sio sababu huna pesa.

Ukiambiwa ukweli unaona kama vile  unafokewa kwa sababu huna pesa lakini ukweli ni kuwa wanakuonya tu ili uwe kwenye uelekeo mzuri tu na sio sababu huna pesa.

Ukiachwa kwenye mahusiano kwa sababu hata  nyingine kabisa wewe tayari unajua ni vile tu huna  pesa ndio maana umeachwa.

Kanisani/misikitini au kwenye jamii usipopewa uongozi unajua tayari wamekuona huna pesa ndio maana hawakupi uongozi kumbe hata yawezekana wana sababu zao tofauti na unavyojifikiria na muda wote unahisi kuna watu wana  njama mbaya na wewe. 

Muda wote unajitetea kwa kutumia hali yako ya kukosa pesa na hapo ndipo unakuwa unajipotezea heshima yako.

Unaona watu wanakunyima makusudi pesa ili  kukukomoa ,huamini kama na wao hawana.

Dhibiti hisia za umiliki wa pesa au ukosefu wa pesa na ukiliweza hilo basi pesa itakuwa rafiki yako na hata kama huna basi nguvu ya kutafuta itakujia kwani huathiriwi na hisia zake za kutokuwa nayo.

Acha kuunganisha kila tukio na kukosa kwako pesa bali tambua kuwa matukio mengine yangetokea tu  hata kama ungekuwa na hizo pesa. 

Usiruhusu kila mtu ajue hali yako kiuchumi , Shirikisha baadhi ya watu kuhusu hali yako na uwe umejiaminisha kuwa kweli hao ni watu wa maana na busara

Usijitetee sana kwa kutumia hali yako ya ukosefu wa pesa pia usisahau kutafuta pesa ili usiwe mtu wa kujishtukia

Mwanasayansi Saul kalivubha

+255652 134707

Sunday, 23 June 2024

USIFANYE WATOTO WAKO WACHUKIE WAJOMBA NA BABA ZAO WADOGO KWA SABABU YA MATATIZO YAKO.

 USIFANYE WATOTO WAKO WACHUKIE WAJOMBA NA  BABA ZAO WADOGO  KWA SABABU YA MATATIZO YAKO.

Kuhudumia watoto wako ni jukumu lako kwa 100% na tena hutakiwi kulalamika kwenye hilo kwa sababu hawakukulazimisha uwazae  , ikitokea kuna mtu anakusaidia shukuru na isipotokea hayupo usilaumu maana hilo ni jukumu lako wewe kwa 100% na sio vinginevyo.

Usifanye watoto zako wawachukie wajomba na Baba zao wadogo bure kwa sababu ya matatizo yako kwa sababu wewe ndio unatakiwa uwe mstari wa mbele kuwapa malezi bora na mahitaji yote ya msingi hata ukikwama basi angalau uwe umetimiza kwa 90% na ikitokea unasaidiwa iwe kwa 10% tu na tena mshukuru huyo atakayejitoa kufanya hivyo kwa sababu kaingilia majukumu yako 

Ukishindwa kuwasomesha watoto zako basi  wakulaumiwa ni wewe sio uanze kutafuta nani wa kumtupia lawama na hapa wazazi wengi hukosea kwa kuaminisha watoto zako kuwa wameshindwa kusoma shule nzuri kwa sababu ya wajomba ama Baba wadogo hawakuwasaidia na wana maisha mazuri, swali ni je hilo ni jukumu lao? Hapana hilo ni jukumu lako wewe usikwepe kulaumiwa.

Wakikuta milo yako ni ya kubahatisha wa kulaumiwa ni wewe kwa 100% na sio walioshindwa kukusaidia kwa sababu mtoto hakukulazimisha umzae la sivyo kama ilitokea umebakwa au kubambikiziwa mtoto hapo kweli kuna haja ya kusaidiwa kwa sababu imekuwa dharura ila tofauti na hivyo watoto sio dharura hivyo hutakiwi kulaumu wengine bali kujilaumu kutofanya maandalizi na kama mzazi sio vizuri kuuza majukumu yako pengine bali wajibika mwenyewe.

Wakikuta una chumba kimoja mnabanana humo  wa kulaumiwa ni wewe na sio mjomba wao aliyeshindwa kukusaidia kujenga  nyumba kwa sababu ulijua kabisa watoto wakija watahitaji sehemu ya kulala  hivyo ni wajibu wako kuitafuta hiyo sehemu na sio kulalamika , Kama unajiona kabisa huwezi basi acha mchezo wa kubahatisha kwamba kila mtoto huja na baraka zake bali ruhusu waje watoto ambao unajua fika utawamudu bila kulalamika. 

Kama wangejua hauko tayari kuwahudumia basi wasingechagua kuzaliwa na wewe kama tu wangepewa hiyo nafasi ya kuchagua  na hii ni kutokana na wewe kuwasimanga kwa malezi yako , Sio vizuri mzazi kuona kama unateseka kuwahudumia yaani unalipa ada za shule kwa masimango, unawananulia mavazi kwa masimango na kuwaonyesha kama unawahudumia  ili kesho wakulipe.

Mwanasayansi Saul kalivubha 

+255652 134707

Friday, 22 March 2024

USIPOISHI NAO KWA AKILI NYINGI WATU HAWA UTAJIKUTA MATATIZONI MUDA MWINGI.

 USIPOISHI NAO KWA AKILI NYINGI WATU HAWA UTAJIKUTA MATATIZONI MUDA MWINGI.

1.Wanaojiona sahihi muda wote hawa hawachelewi kukubebesha makosa yasiyo kuhusu. 

2.Wajuaji kupitiliza hawa muda wote watakulaumu tu kwani kila jambo watakuona unakosea hata kama wao ndio wamekosea.

3.Wanaokutafuta kwenye shida tu hawa utawaona marafiki ukiwa na kitu cha kuwapa ila  siku ukiwa kwenye uhitaji watakuacha mtaroni.

4.Waropokaji hawa muda wowote watamwaga siri zako mbele ya wasiotakiwa kuzijua hivyo hakikisha hawajui mambo yako ambayo hayatakiwi kujulikana na wengi.

5 Wenye imani za kishirikina kupitiliza hawa hata kwenye jambo la kawaida wao watakushauri uende kwa mganga wa kienyeji kwa sababu wao hawaamini tena kwenye ukawaida

6.Wenye imani za dini kupitiliza, hawa pia kwenye sehemu unayotakiwa utumie akili zako wao watakushauri ufunge na kuomba ili upate majibu sasa ikiwa zaidi hii inakuwa kupoteza muda.

Pia watakushauri uvumilie hata sehemu unayotakiwa kuondoka. 

7 .Wenye wivu wa mapenzi kupitiliza, Hawa kwa muda mfupi watakufanya ufurahie mapenzi ila kwa undani zaidi watafanya ufeli mambo ya msingi kwa mfano unaweza kupata dili la maana la pesa ila watakukataza usiende kalifanya wakihofia kuibiwa kimapenzi. 

8 . Wenye mitizamo ya kimaskini, hawa muda wote wanaamini utajiri ni dhambi hivyo ukiwa nao na wakakumudu basi watakushauri uwe sawa nao.

9.Waliokata tamaa na kuridhika, hawa muda wote watakwambia maisha ndio haya haya.

10 Wenye utoto ilihali ni wakubwa, hawa watalia kwa kila changamoto yaani kwao hawana changamoto ya kuvumilia bali kulia na kukata tamaa, ukiwa nao na wakakumudu utafanana nao.

Mwanasayansi Saul kalivubha.

+255652 134707

Tuesday, 19 March 2024

KOSA LIKIKUFUNZA SIO KOSA TENA BALI NI UPYA ULIOKUWA HUUJUI

KOSA LIKIKUFUNZA SIO KOSA TENA BALI NI UPYA ULIOKUWA HUUJUI.

Sifa ya makosa ni kutoa adhabu na inaweza isiwe muda huo ulipolifanya kosa ila ni lazima litakuadhibu tu mbeleni hivyo hakuna namna unaweza kukwepa adhabu ya kosa lako.

Taarifa inayopendeza ni kuwa kosa likikupa adhabu nawe ukaona kama funzo basi hilo sio kosa tena bali ni upya ambao ulikuwa huujui hapo kabla na njia pekee ya wewe kuujua huo upya imekuwa ni kupitia kukosea.

Usifanye makosa makusudi hapo utakuwa sasa unatafuta adhabu za kujitakia na yawezekana adhabu hiyo isiwe funzo lolote kwako kwa sababu sio jipya bali ulilijua kabla. 

Kwenye mchezo wa mpira timu inafungwa kupitia makosa hiivyo adhabu yake ni kufungwa magoli ila baadaye wachezaji wakimakinika kutafuta walifungwa vipi basi watagundua mbinu zipi wafanye ili wasifungwe tena  na hapo itakuwa wamejifunza kupitia makosa na adhabu waliyo adhibiwa.

Japo makosa mengine adhabu yake ni kali na utaadhibiwa tu bila  kujali hukuwa ukijua kuwa ni kosa hapo kabla ila ukimakinika zaidi utajifunza tu .Kosa bila adhabu ni ngumu kuwa funzo na kikawaida kosa lisilo na adhabu yawezekana lisiwepo labda tu uamue kutuiona hiyo adhabu.

Ukiona maisha yanakuadhibu Kwenye jambo fulani wewe kaa chini tulia utafute wapi ulikosea.


Mwanasayansi Saul kalivubha 

+255652 134707

CHANGAMOTO NI BURUDANI KATIKA MAISHA, BURUDIKA NAZO BADALA YA KULIA LIA HOVYO.

 CHANGAMOTO NI BURUDANI  KATIKA MAISHA, BURUDIKA NAZO  BADALA YA KULIA LIA HOVYO.


Mwanafalsafa mmoja aliwahi kusema ukitaka ufurahie adhabu basi ukipewa usiione kwa sura ya adhabu bali ona kama ni sehemu kama wajibu wako, kwa mfano ukipewa adhabu ya kumwagilia maua wewe ona ni wajibu wako kufanya hiyo ili maua yakue na kustawi.


Changamoto ni burudani kama zilivyo burudani ni ngumu kuburudika bila kuvuja jasho, kwenye suala la burudani kuna upande utavuja jasho na kuna upande utaburudika ila inaitwa burudani na watu hufurahi kwa sababu wameamua kumakinika na upande wa furaha kuliko upande waliovuja jasho.

Maisha ya kukosa kazi kwa muda, kuachwa kwenye mahusiano na mengine mengi yenye sura ya changamoto ni sehemu tu moja wapo  ya burudani ambayo ndio ya kuvuja jasho na kama ukiendelea kukaza utafikia ule upande wa pili wa burudani ambao ni wa kufurahia.

Kwenye hii burudani ya maisha hakuna mtu asiyepitia upande wa kuvuja jasho ambao ndio changamoto na burudani haina maana kama itakuwa na upande mmoja tu wa furaha, ukiona watu kwenye viti virefu au kokote wapo wanajipongeza basi jua wana upande mwingine waliopitia ambao ndio uliwapa hizo pesa.

Ikitokea unafukuzwa ama kukataliwa usione kwa sura ya kukomolewa au kama vile umeadhibiwa bali ona hiyo ni sehemu tu ya burudani ambapo unaandaliwa kwenda kukubalika kwingine tena panaweza kuwa pazuri zaidi ya ulipofukuzwa. Tatizo ni pale ambapo utaiona hiyo changamoto kwa sura ya kukomeshwa hapo utajikuta kwenye maumivu, kulia na kulalamika hovyo kitu ambacho hakitakupa unafuu bali kukuumiza na mbaya zaidi kukufanya uje ukosee tena kwa sababu utafanya maamuzi bila utulivu. 

Maisha yana changamoto nyingi sana na nzito ila ukisema kila moja uione kwa sura yake basi kila siku utakuwa mtu wa kulia hovyo badala ya kujifunza kupitia changamoto hizo.


Mwanasayansi Saul kalivubha

0652 134707

Saturday, 9 March 2024

HARAKATI HAZIMTAKI MTU ANAYEONGOZWA KWA MIHEMKO

HARAKATI HAZITAKI MTU ANAYEONGOZWA KWA MIHEMKO.


1.Mtu ambaye akiambiwa biashara fulani inalipa anaikurupukia.

2.Ambaye akiambiwa alisemwa vibaya muda huo huo anawafuata wahusika.

3.Mtu ambaye akiambiwa kasalitiwa muda huo huo anawasha moto.

4.Mtu ambaye anataka kufanya kila kinachosifiwa sana.


KAMA UNA SIFA HIZO HAPO JUU BASI HUWEZI KUWA MWANAHARAKATI.


Kuwa mwanaharakati uwe na sifa hizi.

1.Usiyekurupuka hovyo.

2.Mchunguzi kabla ya kuongea.

3.Usiyekata tamaa kizembe.

4.Uliyetayari kukoselewa.

Michakato yote haikosi changamoto ni lazima changamoto zije kukupima kuona kweli utaweza kuyamudu mafanikio? 

Changamoto zinapokuja kuna mambo mawili ama hiyo safari sio yako au ni yako ila unatakiwa kukomaaa, sasa kabla hujasema hiyo safari sio yako ni lazima ukomae haswa maana ukiwa mtu wa kukwepa changamoto kwa sababu tu ya mihemko yako basi hakuna safari utakayoiweza hapa Duniani. 


Na ukiwa mtu wa kufanya mambo kwa kukurupukia kwa sababu tu ya mihemko yako basi utakuwa pia mtu wa kuanza upya kila mara kwani itakuwa ukifika njiani unagundua hiyo njia siyo yako bali uliikurupukia tu 


Mwanasayansi Saul kalivubha 

0652 134707

Thursday, 7 March 2024

UKIONA WANAKUNG'ANG'ANIA WAKUPE UTAJIRI WA HARAKA JUA WAMEKUONA AKILI YAKO NI CHENGA

 UkIONA WANAKUNG'ANG'ANIA WAKUPE UTAJIRI WA HARAKA JUA WAMEKUONA AKILI YAKO NI CHENGA 😔 

Umewahi kusikia watu wakijinadi kutoa utajiri wa HARAKA? Yaani kulala maskini na kuamka tajiri? 

Taarifa isiyopendeza ni kuwa kama nawe ni mmoja wa wateja wao basi jua kuna kitu kwako hakipo sawa na tayari wamekiona ndio maana wanakulazimisha uingie kwenye hiyo fursa hiyo.

Wale watu wana akili sana na wapo vizuri kuisoma akili yako hasa kwenye maamuzi yako na utulivu wako na wakiona una maamuzi ya haraka yasiyo na subira basi wanajua wewe ni mteja wao mzuri katika fursa hiyo.

Tangazo lenye lengo la kutoa utajiri wa haraka huwa linawahusu watu wenye sifa hizi:

1.Wasio na utulivu, kama huna utulivu basi utakuwa mteja wao kwa sababu ukikosa utulivu utakuwa mtu wa kufanya mambo bila kufikiria kwa kina, kwa lugha rahisi unakuwa mvivu wa kupima matokeo na matendo ndio maana akija mtu akikwambia jambo fulani ukilifanya leo tu basi kesho utakuwa bilionea unaliendea kwa haraka sana bila kufikiria kuwa kama hilo jambo lingekuwepo si tungekuwa wote mabilionea.

2 Kupenda matokeo ya haraka, kama unapenda matokeo ya haraka basi nawe ni mteja kwa sababu ukiambiwa utajiri utakuja kesho haraka utaamini ila ukiambiwa utakuja baada ya miaka kumi utaona ni utapeli. Kwa lugha nyepesi hawa ni watu ambao hawana subira bali wanataka kila kianzacho leo basi kesho kilete matokeo chanya. 

3.Waliokata tamaa, mkata tamaa ni mtu ambaye haamini tena kwenye kushinda hivyo amebaki kusubiria miujiza tu , kama umekata tamaa kiwango cha mwisho basi nawe utakuwa mteja.

4.Wanaokimbizana na umri, kuna watu ambao kwa namna moja ama nyingine wanajiona kama wameachwa na umri hivyo hawataki tena kitu cha kusubiri bali wanataka tu jambo lianze leo na kesho lije na matokeo, kama upo kundi hili basi nawe ni mteja.

Matangazo haya ya kujinadi kuwa kuna utajiri wa haraka yanzidi kushia kasi kwa sababu watoaji matangazo wamegundua kuwa watu wengi sasa hivi wanataka sana mambo ya miujiza na hawataki tena kusubiria hivyo wapo tayari kulipa gharama ya kupewa utajiri wa haraka usio na uhalisia kuliko kutumia pesa hiyo kutafuta utajiri wenye uhalisia.


Mwanasayansi Saul kalivubha

+255652134707

Monday, 4 March 2024

MAISHA SIO MSTARI MNYOOFU,KONA ZISIKUFANYE UTOKE MCHEZONI

 MAISHA SIO MSTARI MNYOOFU, KONA ZISIKUFANYE UTOKE MCHEZONI.

Kinachotutesa wengi ni kuishi kwa imani kuwa maisha ni mstari mnyoofu na hili sio tu tumelijenga sasa la hasha! Bali hata mifumo ya malezi inachangia hilo.

Kuna ambao wamelelewa kwa kuaminishwa kuwa vitu hupatikana kwa wakati ule watakao  hivyo kufanya ukubwani watu wapate shida sana pindi wanapokutana na uhalisia wa maisha kuwa maisha sio mstari mnyoofu.

Utotoni tuliamini kwa ambao wamefika shule wengi  waliamini shule ikiisha tu leo basi kesho wanapata ajira na wakipata ajira tu tayari wananunua nyumba, gari, kuoa/kuolewa na  kufurahia maisha. Hii nadharia ambayo inaonyesha kuwa maisha ni mstari mnyoofu lakini tukija kwenye michakato ya maisha ni wachache sana wanaopitia mstari mnyoofu na hata kama mambo yako yatakunyookea kwenye jambo moja basi kwenye jambo la pili mambo hayakuwa na unyoofu. 

Utotoni ilikuwa kila ukililia kitu unapewa kwa wakati na  hapa ndio mwanzo wa imani hiyo kuwa maisha ni mstari mnyoofu ilipoanzia ambayo ipo kinyume na uhalisia wa maisha. 

Maisha sio mstari mnyoofu na kuwa hivi haimaanishi kwamba ni changamoto bali ndio uhalisia wenyewe ambao unatakiwa kupambana nao na sio kujiona mtu mwenye mikosi kwa sababu tu umemaliza shule na kukaa mtaani miaka mitano bila kazi, umeachika kwa mchumba uliyempenda au umeanza kazi tu unataka kila kitu ununue kwa mshahara mmoja hilo haliwezekani na ukitaka liwezekane basi utajikuta gerezani. 

Kuna ambao wanaanza mahusiano yao ya kwanza na yanageuka ndoa ila kuna wengi ambao wanapitia dhoruba kadhaa za kuachika ndio baadaye zinakuja ndoa, kuna muda maisha yanakupitisha sehemu ambayo hapo zamani ulijua wanaopitia humo wana dhambi kumbe ni mapito tu kuwa maisha sio mstari mnyoofu bali kuna kona nyingi za kukomaa nazo.

Kuna wanaomaliza vyuo na kupata ajira ila kwa zama hizi kuna mtu mpaka kasahau kuwa na yeye alisoma chuo kwa sababu ana miaka mingi mtaani. Kumaliza chuo na kukosa ajira haimaanishi kuwa maisha ndio yamefikia ukomo bali hiyo ni kona ambayo unafaa ukomae nayo na hapo ndipo ujuzi wako wa udereva unapimwa.

Dereva mzuri haogopi kona za bara bara, ukiona dereva anataka tu apite barabara tambarare na kukwepa kila barabara yenye kona basi kuna shida kwenye ujuzi wake tena cheti chake kichunguzwe na vivyo hivyo hata kwenye harakati za maisha kama unataka kila jambo lako lisiwe na kona basi haya maisha yatakushinda kwa sababu kuna muda utajua kesho utapata ila unakuja kupata kesho kutwa .

Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul kalivubha.

+255652 134707

Sunday, 3 March 2024

KAMA UNATOKA UKOO HUU BASI JUKUMU LA KUTENGENEZA UKOO MPYA TAJIRI LINAKUHUSU LA SIVYO UWE PIA MASKINI NA WEWE

 KAMA UNATOKA UKOO HUU BASI JUKUMU LA KUTENGENEZA UKOO MPYA TAJIRI LINAKUHUSU LA SIVYONAWE MASKINI. .

Dhana kuwa mambo hufuata watu ndani ya ukoo ina ukweli wake na mifano yake ipo wazi tu , tukiachana na mfanano wa vinasaba pia hata mazingira huchangia hali hiyo japo kwa ulimwengu wa kiroho watalaam wanasema kuna roho huwa zinatembea ndani ya ukoo fulani. 

Ulimwengu wa kitajiri na maskini kuna koo utakuta ni tajiri kutoka Babu mpaka mjuu na kuna koo utakuta ni maskini kuanzia Babu mpaka mjukuu na hapo ndipo kwenye dhana ya urithi wa utajiri na umaskini. 

Umewahi kuona ukoo fulani mtu mmoja tu ndio tajiri ila wengine wote ni maskini? Kama ndio Jaribu kufuatilia historia ya huyo mtu lazima katumia nguvu kubwa kuwa hivyo wa pekee na hiyo nguvu ndio inaitwa nguvu ya kujiengua kutoka kwenye ukoo maskini na kujitengenezea ukoo tajiri vivyo hivyo kuna mtu maskini ila wengi kwenye ukoo wake ni matajiri basi huyo yupo anajiengua kutoka ukoo tajiri na kutengeneza ukoo wake maskini. 

Sio kazi kubwa kujijua upo kwenye ukoo upi bali angalia tu viashiria kama kwenu hakuna tajiri na historia ya babu zako pia hali ilikuwa hivyo hivyo basi jua una kazi kubwa ya kufanya kuukana ukoo huo na kutengeneza ukoo mpya tajiri ( sina maana uukane kuwa wewe sio mwana ukoo la hasha bali uukane umaskini unaotembea kwenye ukoo wenu), Sasa uta ukana vipi?

HAYA NDIO MAMBO YA KUFANYA ILI KUACHANA NA UKOO MASKINI NA KUTENGENEZA UKOO MPYA TAJIRI. 

1.Kwenye kuoa/kuolewa jitahidi uambatane na mtu ambaye sio maskini wa fikra ( anaweza kuwa maskini wa kipato ila asiwe maskini wa fikra yaani akilini awe tajiri ajaye tena kwa vitendo).

2.Usisumbuke kumaliza umaskini wa ukoo wenu hili hutaweza bali nawe utaishia kuwa maskini pia bali anza kuandaa utajiri mpaka utakao wazaa waukute ili waanzie pale ulipoishia wewe. 

3.Kubali kulaumiwa na wana ukoo bali usiache kuwa sawa nao maana ukianza kujipata lawama zitakuwa nyingi sana na hasa pale utapokuwa ukikwepa mizigo yao kwa mfano wataanza kutaka usomeshe watoto wao wote, uwajengee nyumba na mengine mengi lakini je kweli ukiwafanyia hivyo utatoboa ?

3.Wekeza kwenye mipango ambayo hata ukifa yenyewe haifi bali itaendelea kuishi na hivi ndivyo wafanyavyo matajiri wote ambao wanataka utajiri wao usife pindi wao wakifa.

4.Usikubali kuwa mshirikina ili upate utajiri hapa nawe utakuwa maskini tu kwa sababu kwenye hizo imani za kishirikina kuna laana tupu na kuna ambao wameishia jela na hata utajiri hawajapata , kufikiria utajiri kwa njia ya kishirikina ni matokeo ya uvivu wa kufikiria na kukosa utulivu wa subira.


4.Andaa watoto wako kuwa matajiri pindi wakiwa wadogo na kwenye hili uwe mkali kidogo kwa sababu wanaweza kulemaa wakihisi hata wasipo pambana bado tu watarithi utajiri wako, waandae zaidi kuendeleza mali na sio kurithi mali .

5.Usikate tamaa kizembe ukiona harakati zinakuwa ngumu kwako usianze kujifariji kwa kauli zisizo faa na za kimaskini kama vile 

" Maisha ndio haya haya"

 "Maskini pia ni mtu"

"Sisi kwetu ndivyo tulivyo hatuwezi biashara "

Hizo ni kauli za kimaskini na zisizo na ukombozi wowote ule kifikra bali kukukandamiza tu kuwa maskini zaidi.

Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul kalivubha 

#fikia ndoto zako 

+255652 134707

Tuesday, 27 February 2024

IFIKE MUDA UJANJARUKE NA WEWE KATAA KUFANYWA FURSA ISIYO NA FAIDA KWAKO

 IFIKE MUDA UJANJARUKE NA WEWE KATAA KUFANYWA FURSA ISIYO NA FAIDA KWAKO. 


1.Unakubalije kuwa na mtu ambaye kila akikutafuta basi ana shida. 

2.Unakubalije kuhusiana na mtu ambaye bila wewe kumtafuta basi mahusiano ndio yanakufa .

3.Unakubalije kuwa na rafiki ambaye anataka umtimizie mambo yake kila anapotaka la sivyo anakuchukia 

4.Unakubalije kuwa mtu wa kuonewa hovyo hovyo?


WATU WA HOVYO WANAWEZA KUWA KIKWAZO KWAKO KUFANIKIWA. 


Kuna watu lazima ufanye tu maamuzi magumu ya kuwaepuka na hapo ndipo utagundua kuwa walikuchelewesha kwa sababu utaanza kuona matokeo chanya kwako.


Taarifa isiyopendeza ni kuwa kuna watu wamekusoma vya kutosha na wamekuona hujielewi hivyo wanakutumia kama mtatuzi wa shida zao huku wewe ukiendelea kuangamia taratibu. 


Kila siku jifunze kuhusu watu bila kusahau kuwatathimini marafiki zako ili ujue nani yupo kwako kweli na nani yupo kwako kukutumia hovyo. 


Mwanasayansi Saul kalivubha

Fikia Ndoto zako 

+255652 134707

Sunday, 18 February 2024

KAMA LENGO LAKO KUU NI KUZAA ILI WATOTO WAJE KUKULIPA FADHILA KWA MALEZI BASI NAKUSHAURI HAIRISHA KUWA MZAZI KWA SABABU WEWE NI MJASIRIAMALI NA SIO MZAZI.

 KAMA LENGO LAKO KUU NI KUZAA ILI WATOTO WAJE KUKULIPA FADHILA KWA MALEZI BASI  NAKUSHAURI HAIRISHA KUWA MZAZI KWA SABABU WEWE NI MJASIRIAMALI NA SIO MZAZI.

Ni ushauri tu sio lazima ufuatwe na wote ila unaweza kuutafakari kabla ya kuupinga kwa mihemko ya hoja zisizo na mashiko.Kama hujui kwanini tunazaliana sio vibaya ukapitia upya tena hata maandiko ya Mungu ili uone hata huko lengo kuu halisemi  kuzaa ili watoto waje kukulipa fadhila kwa malezi yako na kama hapo bado haitoshi basi Jaribu kukaa na wazee hasa wenye umri wa miaka sitini utasikia wengi wao wakilalamika kuwa watoto wao hawawasaidii ila usikomee hapo nenda kafuatilie maisha ya hao wanaopewa lawama utakuta maisha yao bado pia yanahitaji utegemezi yaani bado hata wao hawajajimudu sasa swali ni je ni sawa kulaumiwa?

Kama sio changamoto mfano kubakwa na kusababishiwa ujauzito basi usikurupuke kuwa mzazi ilihali hujajua kwanini unatakiwa kufanya hivyo.


Usiwe  mzazi kwa ulimbukeni tu  bali jiulize upo tayari kulipa gharama za kuwa mzazi? Au ndio unataka uwe yule mzazi ambaye anatoa malezi kwa mkopo ili baadaye alipwe?

Kuna watoto hawasemi tu ila ukweli wanashindwa kuwaelewa wazazi wao kwa sababu mpaka wanatamkiwa maneno ya laana kwa sababu tu hawataki kuwalipa fadhila wazazi wao , wazazi wamekuwa wakiwatamkia maneno makali na kusema bila aibu kuwa waliuza sijui nyumba ili watoto wasome sasa huo ni wajibu wa mzazi kumuandaa mtoto ikiwemo kumpa elimu sio uje kumdai baadaye naye akulipe.

Mzazi jiandaye vizuri kabla ya kuwa Baba au mama na elewa kuwa utatakiwa kuwajibika kimalezi bila kufikiria kulipwa fadhila.

Watoto wengi wamekuwa wanaishi kwa kukosa utulivu kwa sababu wanalazimishwa kuwajengea wazazi nyumba bila hivyo wanatishiwa kupewa laana sasa Kama umri wako wote wa ujana umeshindwa kujenga na tena usikute ni kwa uzembe wako tu iweje uwabane watoto wakufanyie hivyo na kibaya zaidi unakuta ndio kwanza mtoto kapata ajira au ndio kwanza anajitafuta ila tayari mezani umemlundikia matatizo yote ambayo wewe ukiwa na nguvu yalikushinda.

Kushindwa kujiandaa kwako mzazi ni chanzo cha matatizo kwenye familia za watoto wako kwa sababu mtoto ataogopa mpaka kuoa kwa sababu tu akijiongezea majukumu atashindwa kukuhudumia wewe na kwa wale ambao watalazimisha kufanya hivyo basi itazuka vita kati ya mzazi na mkwe wake kwa sababu mzazi ataamini hajaliwi kwa sababu mkwe ameingilia kati.Kwa mtoto wa kike naye ndio pale analazimishwa kuolewa na mtu mwenye pesa tu ili awe Kama kitega uchumi na kama sio hivyo basi ndio akiolewa anabanwa awe anatuma pesa mara nyingi mwisho wa siku mumewe anagundua hivyo tayari ndoa inaanza migogoro na yote hayo ni kosa tu la mzazi Kushindwa kujiandaa kujitegemea na kutaka watoto wamlipe fadhila.


Mzazi tambua kuwa kumtunza mtoto ni wajibu wako sio kumkopesha na jukumu la kujitunza wewe ni lako japo watoto wanaweza kukusaidia ila sio kitu cha kutegemea kwa sababu na wao wana majukumu ya kuanzisha familia na kujitafuta pia kiuchumi ili uzao uendelee, ukizeeka au ukawa unaumwa na huwezi kujimudu basi hapo watoto watachukua jukumu la kukutunza ila bado una nguvu na sio mzee unaanza kuwabana watoto wakulipe fadhila je wakaibe ? 

Kushindwa kujiandaa kwa mzazi ndio mwanzo wa kulaumiana kwenye familia mpaka ukoo na hii ni pale ambapo watoto wako mwenyewe unataka ndugu wakusomeshee na wakisema hawawezi tayari unawatupia lawama nyingi  tena bila aibu unaongea hata mbele za watu kuwa kina fulani hawataki kusomesha watoto zako ilihali wana pesa bila kufikiria kuwa na wao wana mizigo yao pia hata kama wana pesa ila unajua bajeti zao? Kilichofanya yote hayo ni wewe hapo kwanini lawama wapewe wengine?

Mzazi kamili hujiandaa yeye na kuwaandalia watoto pia na kwa kufanya hivi ni rahisi kuvunja mnyororo wa umaskini kwa watoto wakizaliwa wanajipambania  wao na wajukuu zao na sio tena uwape familia nyingine yaani wapambane kwa ajili ya watoto wao na huku pia wakupambanie wewe. 

Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul kalivubha 

+255652 134707

Saturday, 10 February 2024

KAMA HIVI NDIVYO UNAVYOISHI MJINI NI BORA URUDI TU KIJIJINI UKAISHI KULINGANA NA KIPATO CHAKO

 KAMA HIVI NDIVYO UNAVYOISHI MJINI NI BORA URUDI TU KIJIJINI UKAISHI KULINGANA NA KIPATO CHAKO.

Yawezekana hii isiwe makala nzuri kwa waishiyo mijini huku wakijisifu kila siku na kuwabeza waishiyo vijijini ila ukimakinika na kuchukulia chanya basi kuna jambo utajifunza. Kuishi mjini ni ndoto ya wengi nafikiri inaweza kuwa zaidi ya asilimia hamsini ya watu wanatamani kuishi mjini na hasa kwenye miji ile mikubwa  lakini uhalisia ukoje huko mjini kwa wengi wao? Kuwa kwenye changamoto  mjini sio sababu pekee ya kusema uhame urudi kijijini/mkoani la hasha ! Hapa namaanisha kwa wale ambo mjini hawapawezi kabisa ila wanapang'ang'ania  tu kwa sababu zisizo na msingi.

Bila shaka utakuwa umewahi sikia ama kuona baadhi ya watu waishio mijini wakiwabeza watu waishio vijijini ama mikoani kama wasemavyo watu  wa Dar es salaam na kibaya zaidi hudiliki kusema watu wa vijijini ni washamba na wasio wabunifu wa maisha, Sio uongo kuwa kuishi mjini kunakomaza akili kulinganisha na kuishi kijijini kutokana na harakati kuwa nyingi mjini na panahitaji wepesi sana katika maamuzi ili uweze kumudu mjini lakini kwenye maamuzi hayo hayo kuna watu wapo mijini kuongeza idadi tu ya watu ila ki uhalisia wanaishi maisha magumu sana kwa lugha isiyo rasmi ni kuwa walikurupuka kuja mjini ilihali hawana mipango ya kuwafanya wanufaike na maisha ya mjini. 

Ikiwa unaishi mjini kwa sababu moja wapo kama  nimevyoelezea hapa chini  basi haraka toka mjini urudi mkoani/kijijini  ama jitafakari zaidi ubadili mtindo wako wa maisha.

Kuishi mjini ki ulimbukeni; Unaishi mjini kutaka tu uonekane nawe unaishi mjini yaani ukisimama na kujitambulisha ama kutambuliswa unaishi mjini hiyo ndiyo furaha yako kuu bila kujali hali ngumu unayokutana nayo huko mjini na kama hii ndio sababu pekee ya wewe kuishi mjini basi haraka ondoka mjini kwa sababu unaongeza tu idadi ya watu na usipokuwa makini maisha yatakuchapa  na kujikuta kwenye hali mbaya kimaisha mpaka kwa uzao wako pia, kwa sababu utatumia gharama kubwa kuwafanya watu wajue kuwa unaishi mjini ilihali hiyo gharama ungeitumia kuboresha maisha yako huko mjini, kila siku utakuwa mtu wa kuchapisha maudhui mitandaoni ya kukuonyesha upo mjini ambapo vocha zitateketea tu bure na hakuna unachokiingiza tofauti na sifa ambazo hazikuingizii pesa. 

Kuishi mjini kwa sababu umepazoea; Kuna mtu maisha ya mjini kwake ni magumu sana na kikawaida tayari yamemshinda ila  ukimpa fursa za kurudi mikoani/kijijini anaweza hata kukutukana na ukitaka kujua sababu anakwambia kapozea mjini hivyo itampa sana tabu kuanza tena upya huko mikoani  kama wewe ndio huyu jua kabisa mjini hapakufai ondoka haraka la sivyo jiandaye kuzeeka maskini.

Kuendelea kuishi mjini kwa maisha magumu ukiogopa kuchekwa endapo utarudi mkoani/kijijini; Huyu pia hafai kuishi mjini kwa sababu hatofautiani sana na mtu limbukeni na asiye na malengo,Huyu yupo tayari kufanya maamuzi ila anaogopa macho ya watu ilihali mjini pememshinda  kuishi sasa nawe jiandaye kuishi maisha magumu sana kwa sababu huna mbinu za kutatua changamoto ili umudu maisha ya mjini bali upo tu kuonekana mtoto wa mjini ilihali maisha yamekushinda .

Kuishi mjini huku unategemea mshahara tu kama chanzo pekee cha pesa na huna chachu yoyote ya kuongeza vyanzo vingine vya pesa; Hili kundi lina watu wengi sana na hapa ndipo utakuta mtu anaishi mjini kimateso sana na hana mpango wowote wa kujinasua na mateso hayo , Kwa mfano unategemea mshahara tu ndio ulipe kodi ya nyumba,ukupe  nauli zako za  kila siku kukupeleka kazini, ukupe ada ya watoto tena shule za mjini hawana huruma kama huna ada mtoto watamfukuza tu sasa hapo kweli utaishi maisha ya furaha? Sio kwamba kila siku utakuwa mtu wa kulalamika tu kwanini mishahara haipandi . Kama wewe ndio huyu ondoka haraka mjini urudi mkoani kwenye nyumba nzima unapanga elfu hamsini na bado zipo jirani na unapofanyia kazi hivyo  huna haja ya kulipa nauli , haya kwako yatakuwa maamuzi sahihi kwa sababu huko mjini pia umekaa tu hutaki biashara hivyo ni bora urudi kuishi kwa kutegemea mshahara sehemu yenye maisha rahisi. 

Kama unaishi mjini huku ukisifia tu maisha mazuri ya mjini na jinsi watu walivyo na majumba makubwa na magari ila wewe huna hiyo nyumba na wala gari pia ; kama wewe pia ni huyu basi  mjini hapakufai tena ondoka haraka kwa sababu upo kwenye kundi lisilo lako na mwisho wa siku shida utapata wewe, upo mjini kushangaa tu wengine wakifanya maendeleo ila wewe unaendelea kuwa mteja wao kwa  kuwaongezea kipato tu sasa unafanya nini mjini? 


Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul kalivubha 

+255652 134707 

Saturday, 3 February 2024

MAMBO UNAYOTAKIWA UFANYE UKIWA NA UMRI KATI YA MIAKA 20 MPAKA 30

 KIJANA JITAHIDI USIJIPOTEZE UKIWA NA UMRI KATI YA MIAKA 20-30

Katika makuzi kuna mgawanyo wa hatua takribani nne ambapo karibu kila mtu kwa kudra za mwenyezi Mungu huzipitia, Vipindi hivyo hugawanywa kwa kuzingatia umri na matukio yake na pia kila kipindi ni muhimu zaidi katika kuandaa kipindi kingine hivyo kumbe hutegemeana.Japo hatua hizo za makuzi hutegemeana ila ipo hatua yenye changamoto nyingi na iliyomuhimu sana na mtu usipokuwa makini utajikuta unajipoteza na ukiwa makini zaidi utajipata .

UMRI KATI YA MWAKA 1 MPAKA MIAKA 18 , Huu ni umri wa kujidanganya sana na kutengeneza malengo ya ukubwani  na kwanini kujidanganya? Kwa sababu unakuwa unaona kila kitu kitawezekana bila kusubiriwa kwa mfano: Utaona utamaliza shule mpaka chuo na baada ya kumaliza tu utapata kazi ya kuajiriwa na pengine ukipata kazi tu utalipa fadhila kwa waliokusomesha /kukusaidia na kisha utaoa/kuolewa na ndani ya mwaka huo huo utapata mtoto wako wa kwanza. Hivi ndivyo wengi tulipanga tukiwa na umri huo na walio kwenye umri huo pia wapo wanapanga wakiamini maisha ni mstari mnyoofu hivyo kila kitu kitaenda bila shaka yoyote, Je ni vibaya kupanga? Sio vibaya ndio maana awali nikatangulia kusema kuwa huu ndio umri wa kujiona ukiwa mkubwa utakuaje, Kwanini ni umri wa kujidanganya? Tuone hatua ya pili kisha hili jibu litapatikana.

UMRI KATI YA MIAKA 20- 30 ( UMRI WA UHALISIA) Huu ndio umri wa kuona vitu kwa vitendo kwa namna kijana alivyojichora akiwa na miaka 18 kurudi nyuma,Kwenye umri huu ndio utaona maisha ni mstari mnyoofu ama ni mstari wenye kona nyingi? Katika umri huu kwa wale ambao walienda shule wengi humaliza elimu zao mpaka za vyuoni na kikawaida ndipo wanakaribishwa rasmi mtaani na hapa ndipo uhalisia unaonekana.

Katika umri huu mambo mengi yanakuja kinyume na namna mtu alivyofikiri japo yanatimia ila kuna kitu kinaitwa Subira ndio hasa kinafaa kitumike kwenye umri huo kwa sababu ukiwa mtu wa pupa lazima utakata tamaa na kuona maisha ni magumu sana.

Sio ajabu kumaliza shule ukajikuta unapata kazi baada ya miaka mitano tofauti na ulivyojiona kuwa utamaliza leo na kesho utaitwa kazini.

Sio ajabu ukaoa/ kuolewa nje umri uliojipangia kwa mfano ulijua utamaliza tu chuo utaingia kwenye familia ila unamaliza unakaa tena miaka mitano mbele ndio unaanza familia. 

Sio ajabu ukaingia kwenye familia mapema tu ila ukakutana na  changamoto za uzazi ukajikuta unapata mtoto wa kwanza baada ya miaka 7 ya ndoa tofauti na ulivyoona ukiingia tu leo kwenye ndoa basi kesho tayari mimba na hata usijaliwe kupata maana yote ni mipango ya Mungu.

Sio ajabu ukavuka miaka 20 bila kuwa na kiwanja wala nyumba ukiwa bado umepanga au hata kuishi kwa wazazi  tofauti na ulivyojiona kumiliki nyumba na usafiri ukiwa kati ya  miaka 20 tu.

Hayo ni baadhi ya matukio ambayo yapo na wengi huyapitia na ndio inakuja ile sababu ya huu umri kuitwa umri wa UHALISIA, na huu umri unatufundisha kuwa maisha sio mstari mnyoofu na kutokuwa mstari mnyoofu haimaanishi kuwa malengo hayawezekani la hasha bali subira inatakiwa sana katika umri huo la sivyo utajipoteza kwa kuwa mtu mwenye haraka na mwisho wa siku unaishi maisha yasiyo ya uhalisia wako kwa mfano ulihisi utapata nyumba na gari haraka sasa ili kutaka yawezekana unaingia kwenye wizi au kwa waganga wa kienyeji wanakwambia utoe kafala mwisho wa siku unaishia gerezani .

Umri huu hutakiwi kuwa na haraka bali kuwa na juhudi tu za kupambania ndoto zako na sio lazima zije kwenye mstari mnyoofu ila ikitokea zinakuja kwenye unyoofu basi shukuru Mungu kwa hilo maana upo kwenye kundi la wachache ambao mambo yao yanakuwa kwenye unyoofu pasi na chenga.Usikubali ujipoteze hapa kwa sababu ukijipoteza kuna uwezekano mkubwa nyakati zitazofuata zisikusaidie kujipata tena.

UMRI KATI YA MIAKA 40- 55, Huu ni umri wenye matukio mawili makubwa la kwanza ni kukubali matokeo  huku ukilazimisha uendelee kuonekana kijana wa miaka 30 ,hii ni wale ambao walikata tamaa na kuona maisha ndio haya haya hivyo wanaamua kuridhika lakini changamoto nyingine inayowakabiri ni kupingana na umri yaani hawataki kukubali kuwa wao ni watu wazima na utajigundua hivyo pale ukianza kuona  unalazimisha kufanya vitu visivyo endana na umri wako, kitaalamu hiki kipindi kinaitwa mid age crisis(kuupinga utu uzima)

Tukio la pili ni wale ambao hawakukata tamaa hivyo wanaendelea kujitafuta na uwezekano wa kujipata upo  .

Changamoto kubwa kwenye umri huu ni kuwa majukumu yanakuwa mengi sana hivyo utegemezi unakuwa mkubwa hivyo kama hukujipanga vizuri utakuwa unapata pesa ila zinaishia kwa wategemezi wako.

UMRI KUANZIA MIAKA 60 KUENDELEA, Hapa ni uzee tu na kupumzika ijapo bado kuna wengine wataendelea na kutafuta tu kama matokeo ya kushindwa kutumia ujana wao vyema au kushindwa kuweka mikakati mizuri ujanani. 

Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul kalivubha 

+255652 134707