Karibu kwenye blog hii yenye kutoa mafunzo ya maisha na jinsi ya kufikia ndoto zetu.
Saturday, 30 April 2022
MAISHA HAYA HAPA
Saturday, 9 April 2022
NAMNA YA KUTIBU MAJERAHA YA KIHISIA
TIBA YA HISIA ZILIZOJERUHIWA.
HISIA ni msukumo ambao unahitaji kutimilizwa , mfano mtu ukiwa na hisia za kupenda utafurahi ukipendwa, ukiwa na hisia za hasira utataka ufanye jambo fulani kuimaliza hasira n.k, sasa tunapata picha kuwa kila kwenye hisia kuna jambo litatakiwa kufanywa ili kutimiliza lengo la hisia.Tuangalie kisa hiki ambapo najua kwa namna moja au nyingine utakuwa umewahi kuwa muhanga, mmepanga kukutana na rafiki yako mnayependana kweli mara ghafla siku moja kabla anakutumia ujumbe kuwa hatoweza kuja tena siku hiyo kapatwa na dharura hivyo mpaka siku nyingine kama wewe utajisikiaje? Kwa jibu la haraka utajisikia vibaya na sababu kubwa sio kuwa kakupotezea muda kama wengi wanavyodai la hasha ni kwa sababu ujio wake kwako ulikuwa ni tiba ya hisia fulani ambazo tayari zilikupanda pale tu mlipokubaliana kukutana tena kibaya zaidi mkiwa mna mahusiano ya kimapenzi ndio utatumia zaidi kwa sababu kajeruhi hisia zako.
Tumeona kuwa kila kwenye hisia kuna jambo linatakiwa hivyo lisipofanyika basi hisia zako zitakuwa zimejeruhiwa. Jeraha la kihisia ( psychological trauma) linatofautiana ukubwa kutokana na aina ya hisia iliyojeruhiwa mfano hasira uliyonayo dhidi ya mtu unayemdai na unataka uonane naye umwambie bayana endapo hutaonana naye utaumia lakini muda sio mrefu jeraha lake litapona utaendelea na maisha lakini hisia za kupenda ikitokea umempenda mtu lakini mwenzako akawa msaliti na mwisho mkavunja uhusiano hilo jeraha lake kupona sio rahisi na litakuathiri sana kama utakosa mbinu za kujitibu.
Bila shaka umewahi kuona watu wakiwa na tabia mpya punde tu baada ya kukutwa na maswaibu fulani, ulevi, wizi, uhuni , kuchelewa kuoa/kuolewa kwa kutoamini tena mahusiano n.k, hayo ni moja ya matokeo ya kushindwa kujitibu majeraha ya hisia zilizojeruhiwa au kujitibu kwa mbinu zisizo sahihi kwa sababu baada ya hisia kujeruhiwa kinachofuata ni muhusika kutafuta tabia mpya itakayomsaidia kusahau maumivu sasa hapo ndipo kuna tatizo wengi huchagua tabia ambayo ndio badala ya kuwatibu ndio inawakandamiza zaidi mfano baada ya mtu kuachwa kwenye mahusiano anaamua kutokuwa tena muaminifu au kutowaamini tena watu tabia ambayo inamfanya aendelee kuteseka kwa sababu ataachwa tena kwa kukosa uaminifu.
Hisia zinapojeruhiwa jitahidi ukubali kwanza hali na pia katika machaguzi ya tabia mpya itayokufanya ujione sawa usichague vilevi na wala usichague kulipiza kisasi bali chagua kujiboresha zaidi ili hata ikitokea tena basi sababu nyingi zisilalie kwako , fuata hatua hizi :
1.ikubali hali.
2.Usianzishe tabia za kujisaulisha kwa muda mfano kuanza ulevi n.k,bali tafuta tabia itayokuboresha zaidi
3. Jipe muda mrefu wa kujiboresha ukiwa bora itakujengea kujiamini.
4.Ukiridhika kuwa umejiboresha sasa unaweza kuendelea na maisha mengine na ukiweza epuka vichocheo vitavyokufanya ukumbuke namna ulivyojeruhiwa kihisia.
Saul Kalivubha ,Mwanasayansi tiba
+255652 134707
Saturday, 26 March 2022
MUMBO MUHIMU KABLA YA KUCHUKUA MKOPO
MAMBO MUHIMU YA KUJIULIZA KABLA YA KUCHUKUA MKOPO
Mikopo ni mkombozi kwa watu wa tabaka zote wenye kipato kidogo na matajiri pia hivyo sio kitu kibaya bali ni sehemu ya kujikomboa kiuchumi, mikopo hutolewa na taasisi nyingi za kifedha na hata zisizo za kifedha kuna mashirika na makampuni nayo hutoa mikopo vilevile, lakini mikopo yote hiyo huwa na masharti na sharti kubwa ni riba pamoja na ukomo wa muda wa kulipa huo mkopo na kabla ya mteja kukopeshwa lazima ukidhi vigezo ikiwemo pamoja na mteja kukubaliana na masharti kwa kutia saini fomu ya maridhiano hayo .
Makazini kuna kila aina ya watu katika suala la mafanikio na maamuzi pia, kuna ambao tayari wanahatua fulani katika maendeleo na kuna ambao bado kwanza wanaanza nikimaanisha waajiriwa wapya na wengine sio waajiriwa wapya bali kipato chao sio kikubwa kiasi cha kufanya mambo makubwa ya kifedha hivyo na hapo ndipo suala la kujilinganisha na waliowatungulia kunaanza lakini kosa huja pale ambapo hamasa ya kufanya vitu vikubwa ndani ya muda mfupi inamuandama mfanyakazi na bila kufikiria mara ya pili anaamua kuchukua mkopo ulio nje ya uwezo wake.
Mfanyakazi kabla hujachukua mkopo kwanza hakikisha una ufahamu wako timamu na umejihakikishia kuwa masharti ya mkopo husika na muda husika wa ukomo wa mkopo wako umejiridhisha kuwa hakuna madhara makubwa utapata bali faida kubwa hapo sasa waweza chukua mikopo huo na isiwe una shauku ya kutaka mafanikio makubwa au ukawa umejilinganisha na wafanyakazi wenzako ukajiona uko nyuma kimafanikio sasa unataka uchukue mkopo ili ukimbizane nao kwa sababu hizo ikiwa ndio unazo basi hustahili kuchukua huo mkopo acha kabisa.
Kabla ya kuchukua mkopo utambue kuwa kuna makato mengine yanafanyika kwenya mshahara wako wa msingi hivyo mkopo utakuja kuongeza asilimia ya makato yako kama ilikuwa unakatwa asilimia kumi sasa itakuwa pengine asilimia ishirini hivyo utaweza kuishi kwa mshahara wa asilimia themanini mpaka hapo utakapomaliza kukatwa na wadeni wako?
Jambo lingine muhimu la kuzingatia ni kuwa huo mkopo unachukua kwa ajili ya kutimizia jambo fulani sasa ikiwa ungeweka akiba ungefikisha kiasi sawa na mkopo unaotoka kuuchukua kwa miaka hiyo ambayo utamaliza kuulipa? ikiwa ndio basi tambua huo mkopo uko ndani ya uwezo wako na ikiwa huoni ikiwa hivyo jitafakari upya kabla ya kuingia huo mkataba wa mkopo.
Kutokana na majukumu kuongezeka kila siku na kipato kuwa kilekile sio vibaya kufikiria mikopo kama suluhisho la kutatua uhuru wako kiuchumi hilo ni wazo zuri lakini isiwe ni kwa mihemko ukifanya kwa mihemko utajikuta kwenye matatizo na majuto ya kuulipa huo mkopo na pengine ukaingiwa na msongo wa mawazo hadi mwishowe ukaamua kujikatisha uhai wako wa thamani na wakati ikiwa ungekaa vizuri na akili yako ungepata maamuzi sahihi kabla ya kuuchukua huo mkopo.
Ikiwa ni mkopo unahitaji kwa ajili ya biashara basi jitahidi uwe na uhakika na wazo lako la biashara kwa kufanya utafiti wa kutosha kujiridhisha kabla ya uanzishaji huo na ikiwezekana usitumie pesa yote ya mkopo kwenye biashara bali anza kwa kiasi fulani kisha uende unaongeza mtaji taratibu kwa sababu mara nyingi biashara ikiwa unaanza huwa ni za majaribio chako zitakuwa nyingi sana na inaweza kufa na kuanza tena upya hivyo lazima ujihami katika hilo pia
Mwanasayansi Saul Kalivubha
+255652 134707
Saturday, 19 March 2022
ELIMU YA KUJIAJIRI KWA WANAFUNZI
ELIMU YA KUJIAJIRI IFUNDISHWE MASHULENI
Katika karne hii ya 21 suala la mtu kumaliza shule na kukosa ajira sasa sio geni tena kwa sababu ongezeko la wakosa ajira limekuwa kubwa sana na sababu inaweza isiwe moja tu serikali kushindwa kuajiri wasomi wake wote bali hata mfumo wa maisha wa sasa umebadilika mbali na kuwa wimbi la wasomi linaongezeka kila siku lakini pia ajira za watu sasa zinachukuliwa na mapinduzi ya kiteknolojia mfano zamani ilitakiwa watu waajiriwe kukata tiketi lakini sasa tiketi zinakatwa na mashine hivyo anatakiwa mtu mmoja tu kuisimamia hiyo mashine.
Baadhi ya viongozi hasa wana siasa wamekuwa wakihimiza suala la wahitimu wa vyuo vikuu kujiajiri pindi wamalizapo masomo yao na wasitegemee kuajiriwa na serikali na mwisho wa siku kosa inaonekana ni la uvivu wa muhitimu kushindwa kujiajiri lakini ki uhalisia sio kweli kwa sababu ni rahisi kumwambia mtu ajiajiri lakini kwa muhitimu wa chuo kikuu sio rahisi kwake kwa sababu zaidi ya miaka kumi darasani anaandaliwa kuajiriwa wafikiri siku moja tu itambadili mtizamo aliojengewa kwa miaka kumi? Serikali iweke mfumo wa mwanafunzi tokea shule ya msingi mpaka chuo kikuu hapo mazingira angalau yatakuwa rafiki kujiajiri kwa sababu msingi utakuwa umemjenga, kwa mfano mtu kamaliza taaluma yake ya ualimu kaandaliwa kufundisha sasa akimaliza ajiajiri vipi? afungue kituo cha kufundisha masomo kwa ziada ( tuition) napo nado ni changamoto kwa sababu sasa serikali inahimiza wanafunzi wamakinike zaidi na darasani na sio kwenye vituo vya kufundisha masomo kwa ziada hivyo inakuwa ngumu kutumia taaluma kujiajiri na kujiajiri kwenye mambo mengine nje ya taaluma ndio hayo ambayo mwanafunzi hakupewa misingi tokea mapema.
Serikali kupitia mitaala ya elimu iweke masomo ya kufundisha maisha nje ya taaluma kwa nadharia na vitendo kwa mfano kuwepo na somo la maisha na kujitegemea ambapo hapo mwanafunzi afundishwe stadi mbali mbali za kuyakabili mazingira tofauti na ile taaluma yake kwa mfano kama ni mwalimu afundishe ni namna gani anaweza kuyakabili mazingira bila kuwa na ajira hivyo apewe stadi hizo kama mbinu za kuanzisha biashara ndogo ndogo na namna ya kuikuza biashara hiyo na mwisho wa siku apewe mtihani wa vitendo kwa kuendesha mradi wa shule au kuleta ubunifu wa mradi hii itasaidia sana kumfanya mwanafunzi azoee mazingira mapema.
Wanafunzi wengi bado wanaamini kujiajiri ni umaskini ndio maana wengi wao hilo wazo la kujiajiri hata hawalifikirii na sio makosa yao kuwaza hivyo ni kwa sababu darasani hawakuambiwa ukweli kuwa kuna kukosa ajira na kuishi maisha nje ya ajira ndio maana kila muhitimu kilio chake ni kupata ajira, kuna uwezekano mkubwa wahitimu wakipewa hata mitaji wengi watashindwa kujitegemea kibiashara kwa sababu elimu ya kujitegemea haikufundishwa darasani ni tofauti na mtu ambaye hakuendelea na masomo tayari akili yake aliiandaa kuwa hakuna namna anaweza kuishi bila kujiajiri mwenyewe hivyo anamakinika zaidi na mwisho wa siku anakuwa na elimu nzuri ya kujitegemea.
Serikali iweke ukweli kwa wanafunzi mapema kuwa kuajiriwa sasa ni bahati ya wachache na tena kwa baadhi ya kada na iziweke wazi kada hizo na kwa kada zile ambazo ajira zake hazitoki sana basi zipunguziwe udahili vyuoni wachukuliwe wachache ili kuepusha mlindikano wa wahitimu wasio na ajira mtaani. Suala la kujiajiri kwa sasa inatikiwa iwe ni kama kampeni kwa wanafunzi kwa sababu hali ya wahitimu sio rafiki sana mtaani bado kuna umuhimu wa serikali kuingilia kati kwa kubadili mitaala ya elimu
Mwanasayansi Saul Kalivubha
+255652 134707
Sunday, 13 March 2022
MBINU ZA KUWEKA AKIBA
JINSI YA KUWEKA AKIBA
Elimu ya pesa kila siku inakuwa changamoto mpya kwa watu wengi ndio maana bado kuna watu wanaingiza pesa ya kutosha lakini matumizi yao sio rafiki kiasi cha kuwafanya wabaki na ziada ya pesa . Inawezekana hata wewe ukawa kwenye kundi hilo la watu ambao wanaweka malengo ya kujikomboa kiuchumi kila siku lakini utekekelezaji wake ni mdogo au haupo kabisa, ukijiona wa hali hiyo basi tambua una changamoto katika namna nzima ya kuitawala pesa na njia rahisi kwa watu hali zote za vipato ni uwekaji wa akiba na mipango madhubuti ya namna ya kuizalisha hiyo akiba ili nayo ilete faida.
Akiba kwa tafasiri isiyo rasmi ni namna mtu anavyoijali kesho yake ndio maana leo unajinyima ili kesho ufanikiwe katika jambo fulani , mfano unaingiza shilingi elfu kumi kila mwezi na unataka baada ya mwaka uwe na mtaji wa laki mbili hapo lengo ni wewe upate mtaji wa laki mbili lakini mfukoni una shilingi elfu kumi ambayo kila mwezi utaipata, kwa kawaida unaweza kuiona ndogo lakini kuna uwekano mkubwa mtu asiifikishe kwa mwaka .
Kuna elimu nyingi kuhusu uwekaji wa akiba ambazo hutolewa kila leo na pengine ukawa moja kati ya watu ambao tayari wamewahi kuzitumia njia hizo lakini bila mafanikio yoyote, unafikiri tatizo ni nini? Kuna kitu muhimu kutambua kabla ya kuanza zoezi la kuweka akiba ya pesa nacho ni wazo kuu la kesho, jiulize kesho unataka ufanye nini? na ili ufanikiwe jambo hilo wahitaji kiasi gani cha fedha? Ukifahamu kiasi cha fedha unachohitaji ili kufikia lengo hilo utatakiwa kujua kwa sasa wewe unapata kiasi gani cha fedha? iwe ni kwa mwezi au kwa kila siku muhimu uwe na uhakika na kiasi hicho cha fedha.
Ukijua unaingia shilingi ngapi labda kwa mwezi sasa utatakiwa ujue pia matumizi yako kwa mwezi yakoje? Yanagharimu kiasi kipi cha fedha? Na je matumizi yako kwa siku mpaka mwezi yanakuruhusu uweze kuyafikia malengo yako? Ukiwa na majibu ya maswali hayo ndipo utaangalia sasa kipi kinawezekana kupuguzwa ili matumizi yako kwa mwezi yapungue.
Hatua ya pili ni kuorodhesha matumizi yako katika safu mbili , moja iwe ya matumizi ya lazima mfano chakula n.k na ya pili iwe ni ya matumizi yasiyo ya lazima kisha tafuta uwezekano wa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ili pesa ambayo ilikuwa inatumika kwenye matumizi hayo iingie kwenye akiba na pia uanze kujinyima kimatumizi ili upate pesa ya ziada .
Hatua ya tatu ni kujiwekea mikakati ya kujikumbusha malengo yako kwa mfano unaweza kuwa na utaratibu wa kila siku jioni unapitia daftari lako la malengo ili uwe na shauku ya kuendelea na mapambano bila kuchoka. Unatakiwa Kuheshimu mikakati yako kwa kuwa na nidhamu katika kuweka akiba ili uweze kufikia malengo yako.
Hatua ya mwisho ni kuhakikisha pale upatapo pesa unatoa kwanza kiasi ambacho umeridhia kukiweka kabla ya matumizi mengine yoyote usifanye makosa kwa kuanza kutumia pesa kwanza kisha ndio ubakize akiba , fanya zoezi hilo kwa nidhamu yote na lifanye kwa kuongozwa na malengo ya kesho.
Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul Kalivubha
+255652 134707
Friday, 18 February 2022
MBINU ZA KUISHI NA WATU WENYE TABIA NGUMU
MBINU ZA KUISHI NA WATU WENYE TABIA NGUMU MAKAZINI.
Kama sio wewe basi utakuwa umewahi kutana na mtu akilalamika dhidi ya watu ambao wana tabia zisizo rafiki na pengine mpaka mtu huyo anatamani kuachana na kazi hiyo ili aepuke kukutana na watu hao , ni kweli wapo watu wana tabia ambazo ni ngumu kuvumilikika kiasi kiasi cha kufanya wengine wakose amani pindi wakiwa na watu watu hao wenye tabia zisizo rafiki.
Pengine hata wewe kuna mtu ana tabia ambazo zimekufanya ujiulize swali hili " hivi huyu mtu anaishije na familia yake kwa tabia hizi?" Maana kama yuko hivyo kazini inakuwaje nyumbani kwa ndugu zake ambao wengine analala nao kitanda kimoja na kula nao meza moja si pengine ikawa kila siku makwazo kwenye nyumba hiyo ? Lakini ukweli ni kuwa hakuna makwazo kabisa anaishi na familia yake vizuri tu kwa sababu walipomfahamu walijifunza kuishi naye kwa kumzoea alivyo changamoto ipo kwako ambaye hujazaliwa naye bado hujajifunza kuishi naye na pengine hutaki kujifunza kuishi naye.
Hakuna namna utaishi bila kukutana na watu wenye tabia zote nzuri na mbaya ili uepuke hilo basi kajifungie kisiwani peke yako lakini tofauti na hivyo lazima utakutana na watu wenye tabia zote nzuri na mbaya sasa itategemea na watu hao umekutana nao wapi na wana nafasi gani kwako kama ni kazini na ofisi moja je utaacha kazi kwa sababu ya watu hao? Au utakuwa unakaa nje ya ofisi kuwakwepa watu hao ? Haiwezekani hilo na sio suluhisho lake lazima ujifunze kuishi nao watu hao.
Jitahidi ujue mnapishana sana kwenye kipi kwa sababu sio kweli kwamba mtapishana kwenye kila kitu lazima tu kuna sehemu moja ndio huwa chanzo cha kupishana naye na ukilitambua eneo hilo basi tenga siku moja tafuta eneo tulivu jitafakari ni kwa nini mtapishana? na kwa nini eneo hilo? Anza kutengeneza mbinu za kuishi naye mtu huyo kwenye eneo hilo na moja wapo ya mbinu nzuri ni kutojibana naye sana kwenye eneo hilo jifunze kupuuzia baadhi ya kauli zake , pengine uone ugumu kukaa kimya pindi anapoongea kama tabia yake ilivyo lakini baadaye utazoea tu na itakuwa akiongea mambo yake unajibu machache mengine unamsikiliza.
Mbinu nyingine ni kumpuuza kwenye baadhi ya mambo yake lakini usimuonyeshe kuwa unampuuza bali usifanyie kazi kila tukio lake kwako kwa mfano mmekutana kazini umemsalimia hajaitika au yeye hakusalimii hilo lisikupe msongo wa mawazo kwa kujiuliza kwa nini haitikii salamu zako bali mpuuzie tu kwa sababu ndivyo alivyo na usiache kutabasamu pindi ukikutana naye na wala usilipe kisasi kwa anayokufanyia na hapo itakuwa mwanzo wa wewe kuishi naye mtu huyo.
Mbinu nyingine ya tatu ni kujitahidi unaepuka mazingira ya kukaa na mtu huyo muda mrefu ila isipokuwa pale tu inapobidi kwa sababu za kikazi tofauti na hivyo muepuke mtu huyo kwa kujishugulisha na mambo yako mengine.
Mbinu nyingine ni usiitizame tabia yake kama kikwazo kwako bali muone kama ndivyo aliumbwa hivyo na ukiliweza hili basi usiwe unamuongelea jinsi alivyo mbele ya wengine bali muombee kubadilika kwa sababu tabia yake sio kwamba unaiyona wewe tu bali kuna wengine pia wanaiyona hivyo tabia yake inakuwa kikwazo kwake sio kikwazo kwako wewe kazi yako ni moja tu kujifunza kuishi naye
Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul Kalivubha
+255652134707
Tuesday, 1 February 2022
ELIMU YA PESA
USISUBIRI PESA IPUNGUE NDIO UWEKE NIDHAMU YA MATUMIZI
Matumizi ya pesa bado ni changamoto kwa watu wengi na matokeo yake ni hujikuta katika ukosefu wa pesa mara kwa mara na hii sio kwa waajiwa tu hata waliojiajiri kwenye mambo binafsi bado hujikuta kwenye kipindi kigumu cha ukosefu wa pesa sio kwa sababu haikuwepo la hasha ni kwa sababu ilikuwepo lakini ikatumiwa bila kuzingatia matumizi sahihi kutokana na kipato. Ukipata muda tulivu ukajitafakari utagundua kuwa pindi upatapo pesa matumizi yako yanakuwa juu na hupungua kadri pesa inavyopungua yaani kwa lugha rahisi ni kuwa nidhamu yako ya matumizi ya pesa inaongezeka kadri unavyoishiwa pesa.
Pesa ni nguvu ya kihisia ambapo usipoitawala itakutawala yenyewe kwa kukupa maamuzi mengi na hapo utakosa utulivu hali ambayo itafanya upoteze nidhamu ya matumizi ndio maana mshahara ukiingia unaweza jikuta unafanya manunuzi bila kuangalia ukubwa wa gharama kwa sababu unajua pesa ipo lakini ukianza kusikia mfuko umepwaya ndio utarudisha makini wa matumizi kwa mfano mwanzo ulilipwa laki tano na ilipofikia mfukoni umebaki na laki moja ndio utaanza kuipogia mahesabu hiyo laki moja kuangalia kama itakufikisha mwezi mwingine, je kwa nini hukufikiria hivyo tangu ukiwa na laki tano?
Nidhamu ya pesa ni kuheshimu pato lako kwanza na pili ni kuheshimu matumizi sahihi yaliyo ndani ya kipato chako kama ulipanga kununua kitu cha shilingi mia ndio itakuwa sawa kulingana na kipato chako basi fanya hivyo lakini ulinunua kwa shilingi Mia mbili ujue umekula na pesa ya siku fulani hivyo jiandaye siku hiyo kukosa pesa la sivyo iwe ni dharura ndio tumia lakini kama si dharura yatakiwa ujidhibiti dhidi ya matumizi ya pesa pale tu unapoipata, changamoto ya pesa ni kuwa ukitumia pesa ndogo unaona kawaida tu lakini mwisho wa siku ukijumlisha unakuta kama ungehifadhi ungekuwa mbali sana kifedha hivyo nidhamu ukianza na kuheshimu matumizi yako yaliyo ndani ya kipato chako utakuwa kwenye kiwango kizuri cha kuweka akiba.
Nidhamu binafsi katika matumizi ya pesa inajengwa na lengo kuu ulilonalo la kesho hapo ndio utakuwa unatumia pesa ukikumbuka kesho hivyo utakuwa ukijikumbusha kila kabla ya matumizi ambayo si salama kulingana na kipato chako na utakuwa na nidhamu muda wote, lazima uwe na nidhamu au ukose nidhamu lakini ukubali kupoteza lengo kuu la kesho na njia nzuri nyingine ni kuigawa pesa yako kwa siku utagundua unaingiza shilingi ngapi kila siku na kisha angalia matumizi yako kila siku yanaendana na pato lako la siku? Kwa kuanzia na hapo utajirekebisha kimatumizi na utaheshimu matumizi sahihi ya pesa.
Pesa ikiwa nyingi itakupa upofu uuamini kuwa huwezi kuishiwa hivyo kila matumizi yakujiayo kichwani utayafanya na hapo ndio mwanzo wa kutumia hovyo pesa mpaka baadaye ikipungua ndio itakutoa upofu uone kuwa kuna hatari itokanayo na ukosefu wa pesa kwa sababu pesa uliyonayo haitoshi kukufikisha msimu mwingine wa pesa kumbe kuna kuna nguvu kubwa inatakiwa uwe nayo awali ili kudhibiti hisia za pesa zisikutawale.
Kujua unataka nini pia ni moja wapo wa ujenzi mzuri wa nidhamu ya pesa kwa sababu utajizuia dhidi ya matumizi ambayo sio ya msingi kwako na hayapo ndani ya bajeti yako kwa kipato chako na aina yako ya safari uliyonayo, kutojua nini unataka itakuingiza kwenye matumizi yasiyo sahihi kwa sababu kila utakachokiona kinavutia utahitaji kukinunua.
Mwanasayansi Saul Kalivubha
0652 134707